Swali hili limekuwa likijirudia mara kwa mara, kuwa ni kwa nini wakulima wawe maskini?
Kwa watu walio wengi hata wakulima wenyewe, wana majibu mengi sana ambayo wamekuwa wakiyatoa, hasa katika kutetea huko hiyo, huku wakiweka kuwa wao ni watu wa chini na wanaokubaliana na hali hiyo ya umaskini.
Kuna wale ambao watasema kuwa ni maskini kwa sababu ya zana duni zinazotumika katika uzalishaji, wengine watarushia serikali lawama chungu nzima. Na kuna wale wanaodai kuwa ni maskini kwa sababu wananyonywa na wafanyabiashara.
Yote haya yanaweza kuwa ni majibu sahihi, lakini lililokubwa ni kuwa Mkulima, mfugaji, hupaswi kuwa maskini na hakuna sababu ya kuwa maskini. Wakulima na wafugaji ndio wanaotakiwa kuwa matajiri wa kwanza kisha wengine kufuata.
Kinachotakiwa hapa ni wewe kufunguka akili na kufanya mambo kwa kutumia mahesabu na kuondokana na hali ya kufanya mambo kimazoea na kukubali unyonge.
Kuku mmoja wa kienyeji, anauzwa kati ya shilingi elfu kumi na kumi na tano za kitanzania. Ukiwa na kuku mmoja ukamtunza vizuri, ana uwezo wa kutaga akahatamia na kuangua kiwango cha chini kabisa vifaranga 5, lakini kwa kawaida huenda mpaka vifaranga 10. Ndani ya miezi 3 ina maana kuwa kama kuku huyo alitotoa vifaranga 10, una kuku 11, ukiwa na kuku kumi ina maana kuwa utakuwa na kuku 100 zaidi. Kuku hao ukiuza kila mmoja 10,000 ina maana utakuwa umetengeneza shilingi milioni moja.
Ambapo, kama unafuga ng’ombe, baadhi ya maeneo ng’ombe mmoja anauzwa laki tano, na kwingine mpaka milioni moja, kutegemeana na aina na mikoa. Ng’ombe huyu anaeuzwa kwa shilingi laki tano, unakuwa umemtunza kwa muda mrefu zaidi, na endapo alizaliwa wakati mmoja na kuku niliosema hapo awali, kamwe hautaweza kumuuza kwa bei hiyo.
Sasa basi, ni kwa nini usiuze ng’ombe mmoja kati ya ulionao kwa shilingi laki tano, ukanunua kuku 50, baada ya miezi mitatu, wanaweza kuzalishia wengine 500, ambao ukiwauza kwa bei ile ile ya 10,000 watakupatia kiasi cha milioni tano?