- Mifugo

Ufugaji wa ng,ombe wenye tija

Sambaza chapisho hili

Naomba ushauri, nina ng’ombe mmoja ambaye namfuga ndani. Amezaa uzao wa kwanza ndama dume. Kwa sasa, ninapata lita 10 kwa siku. Ng’ombe ana uzito wa kilo 400. Gharama za utunzaji ni 70%. Nifanye nini ili awe na tija?

Faida zinazotokana na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa zinatokana na kujumuisha mambo mawili muhimu; aina ya ng’ombe na utunzaji wake.

Utunzaji huchukua kiasi cha asilimia themanini (80%) ya mradi wa ufugaji.

Bila matunzo sahihi, hata ng’ombe ambaye angetoa maziwa mengi, atatoa kiasi kidogo sana. Miongoni mwa mambo muhimu kwa mfugaji ni kuahakikisha kuwa anatumia gharama ndogo na kuzalisha kwa wingi, ili kuongeza faida.

Lisha malisho bora

Kwa kiasi kikubwa, malisho yanayotumika kulishia ng’ombe ni kama

vile Matete, Guatemala, nyasi, na mimea jamii ya mikunde kama vile lusina, desmodiamu na mengineyo.

Ni muhimu kwa mfugaji kuhakikisha kuwa anazalisha malisho shambani kwako ili kupunguza gharama ya kununua.

Hakikisha kuwa unakata majani na kuyaacha yanyauke kwa siku moja

kabla ya kuwalisha ng’ombe. Kwa kuwalisha ng’ombe majani makavu, husaidia kupunguza uwezekano wa kuvimbiwa na kuongeza unywaji wa maji. Kata majani kiasi cha sentimita 2.5 kisha walishe ng’ombe kwa kuwawekea kwenye kihondi. Hii inasaidia majani hayo kubaki safi wakati wote na kuepusha upotevu. Ng’ombe wa maziwa wanahitaji kilo 40-70 za malisho bora kwa siku. Gawanya na uwalishe mara mbili kwa siku, inapendekezwa iwe asubuhi na jioni.

Hakikisha wakati wote unawalisha ng’ombe mchanganyiko wa majani na jamii ya mikunde. Kata majani yanayozidi na uhifadhi kwa ajili ya matumizi ya wakati wa kiangazi. Mfugaji mzuri, atakuwa na akiba ya chakula kwa ajili ya ng’ombe wake kinachoweza kutosheleza kwa kipindi cha miezi sita.

Mabaki ya mazao: Haya ni pamoja na mabua ya mahindi, mpunga, ngano, ulezi na kadhalika. Mabaki haya kwa kawaida yana kiwango kidogo sana cha virutubisho, hivyo ni muhimu kuchanganya na molasesi au urea.

Changanya lita 1 ya molasesi na lita 3 za maji, kisha weka kwenye mabua yaliyokatwa vizuri kwa usiku mzima kabla ya kuwalisha ng’ombe. Ili kuwa na ufanisi mzuri zaidi, mchanganyiko huo wa mabua unaweza kuvundikwa kwa wiki tatu kabla ya kutumika. Urea inaweza kusababisha madhara, hivyo inashauriwa wafugaji kabla ya kuitumia wawasiliane na mtaalamu wa mifugo aliye karibu naye ili kupata ushauri na maelekezo zaidi kabla ya kuitumia.

Virutubisho: Ni vizuri ng’ombe wakapatiwa virutubisho vya ziada na vyenye ubora ili kuziba nafasi ya virutubisho ambavyo havikupatikana kutoka kwenye malisho. Virutubisho hivyo vinaweza kununuliwa kutoka kwenye maduka maalumu yanayouza vyakula vya mifugo au mfugaji kutengeneza mwenyewe. Hii inategemeana na upatikanaji wa malighafi zinazohitajika.

Mfano wa chakula kinachotengenezwa nyumbani na kuwa na resheni nzuri ya virutubisho ni ule wenye 70% ya viini vya kutia nguvu, na 30% protini na madini mengine yanayohitajika.

Protini inahitajika kuwepo kwa ajili ya kuziba pale ambapo kulitokea upungufu. Vinginevyo, kama inawezekana wafugaji wapeleke lishe wanayotaka kuwapa mifugo maabara ili kuwa na uhakika wa kiwango cha protini kilichopo.

Ng’ombe anaweza kuzalisha kilo 7 za maziwa kwa siku anapopatiwa malisho yenye ubora, bila kuongeza virutubisho vingine, ili mradi tu kuwepo na madini kamili. Nyongeza ya kiwango hicho ni lazima kifidiwe kwa kumpa kilo 2 za virutubisho kwa kila kilo 3 ya maziwa itakayoongezeka juu ya kila 7 za awali.

Muda wa kulisha: Wafugaji walio wengi, huwapa ng’ombe virutubisho kipindi anapokamuliwa tu. Hata hivyo, ng’ombe huzoea hali hiyo na endapo hakuna virutubisho, basi hupunguza maziwa. Hivyo, lisha ng’ombe wako baada ya kukamua. Kamwe usihusishe virutubisho na ukamuaji. Endapo unafanya hivyo, basi fanya hilo kila wakati unapokamua. Gawanya virutubisho mara mbili; kulisha asubuhi na jioni, kutegeana na ni mara ngapi ng’ombe hukamuliwa kwa siku.

Wakati unapomuandaa ng’ombe kuzaa, mlishe virutubisho kila siku,

kwa kipindi cha miezi miwili kabla ya kuzaa. Lisha virutubisho vya ziada

kilo 2 kwa siku mwezi wa kwanza na uongeze mpaka kufikia kilo 4 kwa ng’ombe kwenye mwezi wa 2, hasa kwa mtamba ambaye bado anakua.

Na, lishe hii huenda sambamba na majani yenye ubora.

Madini: Mpatie kila ng’ombe walau gramu 100 za madini ya ng’ombe yenye uwiano mzuri kwa siku kwa ajili ya kulamba. Kwa kawaida, inapendekezwa kuwapatia ng’ombe wanaokamulikwa gramu 100 mara mbili kwa siku kila wanapokamuliwa.

Aina nyingine za madini zinaweza kuchanganywa na malisho, wakati jiwe linaweza kuning’inizwa ng’ombe walambe wakati wamepumzika.

Maji: Maji ni muhimu kwa Maisha ya mifugo, lakini bado wafugaji walio wengi huwa hawazingatii jambo hili muhimu. Kila kilo moja ya maziwa huwa na gramu 870 za maji. Endapo ng’ombe hatapata maji ya kutosha, hatazalisha maziwa ya kutosha.

Maji ni lazima yawepo zizini muda wote.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *