- Kuku, Mifugo

Mikakati ya kupambana na magonjwa ya kuku ili kupunguza hasara

Sambaza chapisho hili

Magonjwa ya kuku huweza kukatiza uzalishaji kwa muda mfupi sana. Mfugaji anafaa kujenga uelewa na uzoefu wake katika kukabiliana na magonjwa mbalimbali ya kuku. Cha muhimu ni kuweka mikakati ya kuzuia na yanapotoka mfugaji achukuwe hatua za haraka ili kupunguza madhara.

Kuku ni mnyama anayefugwa kwa wingi. Karibu kila kaya lina kuku wanaofugwa kwa ajili ya chakula, hii ikiwa ni nyama au mayai, au kuuzwa kwa ajili ya hela ya kaya nyingi na Wafugaji wengi wamekuwa wakiwekeza katika ufugaji wa kuku. Ufugaji huo unalenga kuku wa kisasa au wa kienyeji.

Wakulima hawa wanajenga mabanda, kununua chakula, pamoja na kuku wa kufuga ili kuzalisha nyama na mayai, huku wakitarajia kupata faida kubwa kutokana na uwekezaji huo. Mara nyingi, mradi unapoanza mambo huonekana kwenda sawa, mpaka mfugaji atakaposhtuliwa na mlipuko wa magonjwa ambayo hupunguza uzalishaji wa mayai, ukuaji wa kuku, na hata kuua kuku wengi.

Hii inamrudisha mkulima nyuma sana; anakosa faida, anatumia pesa kwa matibabu, na wengine hukata tama kabisa na kuchana na ufugaji wa kuku.

Kupunguza hatari

Uzoefu wa wafugaji ambao wamekuwa wakifuga kuku kwa muda mrefu unaonesha kwamba kuweka banda katika hali ya usafi, kuwalisha kuku ipasavyo na kuwapatia maji safi, ndiyo njia muhimu za kupambana na magonjwa kama mharo mwekundu, kipindupindu cha kuku, na ndui.

Pia, kutoa chanjo kwa kuku ilikuzuia magonjwa kama sotoka au ndigana na ndui ni mbinu nyingine hasa kwa wale wanaofuga kuku chotara au wa kisasa.

Tenga kuku wageni

Wakati mfugaji anaanza ufigaji, kwa kawaida ananunua vifaranga na kuwalea hadi wakawa wakubwa au ananunua kutoka kwa wakulima wengine, na hata sokoni. Kawa hali zote mbili, kuku hawa wanatoka nje ya shamba la mfugaji.

Pia, mkulima anapotaka kupanua ufugaji, mara nyingi, anafanya vivyo hivyo, aidha kununua vifaranga au kuku wakubwa. Kuku hawa wanaotoka nje ya shamba la mfugaji huenda wakaleta ama kuwa chanzo cha magonjwa na kuwaambukiza kuku wengine ndani ya eneo la ufugaji. Jambo la busara na linalochangia sana katika kuzuia magonjwa ni kuhakikisha kwamba unanunua kuku wenye afya. Jifunze kutambua na kutofautisha kati ya kuku mgonjwa na mwenye afya nzuri.

Pili, hakikisha unawatenga kuku wageni ili wasitangamane na kuku wengine. Waweke kwenye banda ama eneo mbali ili kuzuia maambukizi hasa kwa magonjwa yanayosambazwa kupitia hewa na maji. Watenge kuku hao kwa muda wa wiki mbili kabla ya kuwaweka kwa kuku wengine. Hii itakuruhusu magonjwa ambayo pengine visababishi vimeingia tayari kwenye mwili wa kuku lakini bado kuku hajaonyesha dalili za ugonjwa. Na kama dalili zinaonekana basi mfugaji anaweza kuanzisha matibabu bila kuhatarisha kuku wengine wenye afya.

Unapoenda kununua kuku au vifaranga, hakikisha unanunua kutoka wafugaji wanaotambulika na kutegemewa. Pia, unaweza kutafuta ushauri kutoka afisa wa mifugo na ikiwezekana ambatana na yeye hadi mahali unanunua kuku.

Na unapowaleta mifugo wapya bandani

  • Ondoa matandazo yote, vyombo vya kulishia na kunyweshea; osha kwa maji moto yenye sababuni na kukausha kwenye jua.
  • Ondoa uchafu wote unaoonekana bandani.
  • Safisha banda lote kwa kutumia maji na dawa.
  • Suuza na uache likauke.
  • Puliza dawa ya kuua wadudu.
  • Weka matandazo mapya yalio safi na kavu, kisha weka viombo vya kulishia na kunyweshea.

Makaazi ya kuku

  • Usafi na nafasi ya kutosha kwenye kibanda cha kuku nguzo muhimu katika kuzuia kuzuka na kuenea kwa maambukizi. Hivyo, ni lazima nyumba ya kuku iwe safi na kavu muda wote.
  • Nyumba ya kuku iwe na nafasi za kupitisha hewa ya kutosha ili kuepuka joto na unyevunyevu. Ikiwa nafasi ni ndogo basi kuku hawatapata hewa safi nah ii uchangia magonjwa kuenea kwa haraka.
  • Hakikisha unabadilisha na kuondoa matandazo na takataka zote kwenye banda wakati wote. Matandazo chafu na yenye unyevu huchangia kuenea kwa magonjwa. Matandazo ni faida kwa mkulima kwani matandazo na taka zinaweza kuwa mbolea nzuri ya mboji kwa mimea yako.
  • Fagia banda na kuhakikisha ni safi wakati wote. Weka matandazo mapya mara kwa mara.
  • Weka sehemu za kutosha kuku kupumzikia, viota vya kutosha, na kuweka maji sehemu ambayo ni rahisi kusafisha.
  • Hakikisha unaondoa wanyama kama panya na wadudu nyemelezi kwenye sehemu ya malisho ya kuku kwani wao hubeba vimelea vya magonjwa.

Lishe ni muhimu

  • Wapatie kuku chakula cha kutosha na chenye virutubisho vyote. Unaweza kuwaongezea majani, makombo, nafaka, mchanga laini ili kusaidia umeng’enyaji.
  • Wapatie kuku maji safi muda wote. Wafugaji wengi wameripoti kuwa na matokeo mazuri baada ya kuchanganya dawa ya kuua vimelea kwenye maji ya kunywa.
  • Safisha vyombo vya kulishia na kunyweshea kila siku. Osha, sugua vizuri, kisha suuza kuondoa utando unaobeba bakteria.
  • Nunua chakula kwa wauzaji wazuri na wanaoaminika ili kuepuka minyoo na sumu hatarishi. Wauzaji wengine wanauza chakula ya hali ya chini na kuathiri ukuaji, hasa vifaranga na kuku wa nyama, na uzalishaji kwa kuku wa mayai. Na unapotengeneza chakula cha kuku wako nyumbani, hakikisha unachanganya kwa viwango vinavyofaa.
  • Hifadhi chakula cha kuku katika sehemu kavu isiyo na joto na isiwe kwa zaidi ya miezi mitatu ili kuepuka kuharibiwa na fangasi. Unaweza kuhifadhi kwa muda mrefu.Hii ni kwa wale wakulima wanatengeneza chakula nyumbani.
  • Usiwape kuku chakula chochote kinachoonekana kuoza au kunuka uvundo.

Ukaguzi wa mara kwa mara Kila siku

  • Safisha vyombo vya kulishia na kunyweshea pamoja na viota.
  • Ondoa kinyesi.
  • Waangalie kuku wako kwa makini ili kujua afya na maendeleo yao.

Kwa wiki

  • Ondoa matandazo machafu na kuweka mapya.

Kwa mwezi

  • Angalia uwepo wa wadudu na chawa, kisha utibu kama kuna ulazima.

Utunzaji wa kuku

  • Toa chanjo muhimu kwa kuku ili kuzuia magonjwa kama utakavyoshauriwa na mtaalamu wa mifugo. Chanjo huanza katika wiki ya kwanza (mfano chanjo ya kuzuia sotoka) na inaweza kurudiwa baadaye.
  • Epuka kuweka kuku wengi mahali pamoja. Ni rahisi magonjwa kuenea kwa haraka kuku wanaporundikana.
  • Tenganisha vifaranga na kuku wakubwa (isipokuwa kutoka kwa mama) kwa sababu vifaranga ni rahisi na wepesi sana kushambuliwa na magonjwa.
  • Weka mipaka na madaraja ya sehemu za kuku kuzunguka/ kucheza.

Mbinu nyingine ni;

  • Muone mtaalamu wa mifugo mara uonapoona dalili zozote za kuumwa kwa mifugo wako. Tenga na wapatie tiba au kuwaua na kuteketeza kabisa kuku wagonjwa kuepuka kuenea kwa magonjwa.
  • Ondoa ndege waliokufa mara moja, uwafukie au kuchoma moto. Usile kuku aliekufa. Baadhi ya magonjwa ya ndege yanaweza kuambukizwa kwa binadamu.
Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *