- Mifugo

Mikakati rahisi ya kupanua ufugaji wa kuku

Sambaza chapisho hili

Ufugaji wa kuku unaweza kumpa mkulima mapato makubwa. Hii inawezekana ikiwa mfugaji mdogo wa kuku atapanua kiwango na idadi ya kuku anaowafuga.

Kuku ni mnyama maarufu na anayefugwa sana nchini Tanzania. Karibu kaya nyingi zinafuga kuku, kwa ajili ya nyama yake yenye ladha nzuri, mayai, pia ni ishara muhimu ya kitamaduni katika baadhi ya jamii.

Je, mbona ni ngumu kuongeza kipato kutoka kwa mnyama huyu mwenye umaarufu mkubwa hivi ambaye bidhaa yake inathaminiwa na kuhitajika?

Wakati mfugaji anajikuta katika wakati mgumu na uhitaji wa haraka wa pesa, kuku ndiye mnyama wa kwanza kuuzwa. Hata wakati mwingine, mgeni wa muhimu akifika kutembelea familia, maranyingi kama kuku wapo, huchinjwa na kufanywa mboga. Hivyo, idadi ya kuku kwa mfugaji inapungua au kukosa kuongezeka. Inakuwa changamoto kukuza ufugaji wa kuku na kufanya biashara yenye tija na kupelekea kukata tamaa. Katika hali kama hii hasa vijijini, inakuwa vigumu kwa mfugaji kutoka kwenye hali wa umaskini.

Fursa katika ufugaji wa kuku

Kuna fursa ya kutoka kwenye uzalishaji mdogo na kwenda hatua-kwa-hatua kwa uzalishaji mkubwa, ambao inaleta mapato makubwa na kuhakikisha usalama wa chakula na kujitosheleza kwa chakula. Hii inaweza kufanikiwa ikiwa wafugaji wadogo wa kuku watapanua viwango na saizi ya mifugo yao.

Ongeza idadi ya kuku

Unahitaji kuongeza idadi ya kuku wako ili iwe na maana kibiashara. Gharama ya kuwatunza kuku inashuka idadi yao inapopanda.

Chagua na kuwatenga kuku wa hali nzuri wa kuzaa, kukalia na kutotoa mayai. Usiuze kundi hili la kuku, badilisha tu jogoo. Wakizeeka ama uwezo wao wa kutaga ukienda chini, unawauza ama kuwabadilisha. Hii inahakikisha unakuwa na mayai ya kutosha kila wakati, na vifaranga wapya kila wakati.

Mara nyingi, wafugaji ambao wanaanza huwa wanatilia mkazo sana makazi ya kuku. Wajenga nyumba za gharama kubwa, mwishowe, hawana pesa za kununua kuku kuanza ufugaji, ama wananunua na kushindwa kuwatunza.

Unapoanza zingatia kuongezeka kwa idadi, sio kwenye nyumba za gharama kubwa. Unaboresha makazi pole pole unapojenga idadi ya kuku wako.

Ikiwa una nafasi, unaweza kuweka ua na kutenga sehemu ya kuku kutembea mchana. Hii inawapa nafasi ya kukula vitu vya kijani kibichi (vitamini) na wadudu (protini), changarawe (nzuri kwa mmeng’enyo wa chakula), na kinyesi chao kinarutubisha udongo. Baadaye, wanarudi kwenye makazi yao ambapo wanapata chakula cha nyongeza kilichotengenezwa nyumbani au kilichonunuliwa madukani.

Ingawa, chakula kinachozalishwa shambani kinapendekezwa kwa kuku asili. Inaweza kuwa mchanganyiko wa nafaka ya mahindi na chanzo cha protini kama soya.

Boresha kila kizazi

Boresha kundi lako kwa kutumia jogoo wa hali ya juu na walioboreshwa. kuzaliana na ndege waliochaguliwa kwa uangalifu na bora. Faida ya kutumia jogoo walioboreshwa ni kwamba utakuwa unaingiza sifa za kukua haraka na mayai makubwa. Anza na kuku jike wa msingi wenye afya na nguvu.

Weka jogoo mmoja na kuku jike kumi. Ukiweka jogoo zaidi basi kuku wako watazidiwa, watafukuzwa kote, watachoka na usumbufu unaathiri kukua kwao na afya kwa ujumla. Kuwa makini kutambua ishara za kupandana kupita kiasi; majeraha, kupoteza manyoya ya nyuma, mabawa, na nyuma ya kichwa. Ukiona haya, punguza idadi ya jogoo.

Dhibiti magonjwa

Kuku hushambuliwa na magonjwa na husababisha hasara kubwa katika ufugaji wa kuku. Ugonjwa wa kutisha zaidi ni Kideri/Mdondo (Newcastle). Punguza uwezako wa maambuzi ya magonjwa kwa kuwapa kuku lishe bora, weka makaazi safi, na kufuata utaratibu wa chanjo. Pia, wape kuku dawa ya miyoo, la sivyo, chakula unachowapa kitakuwa cha kulisha vimelea.

Ikiwa mfumo wa ufugaji huria, wape dawa ya minyoo kila baada ya mwezi moja, na katika mfumo wa nusu huria au ndani wape dawa ya miyoo kila baada ya wiki 6-8. Pia, nyunyiza majivu au chokaa au dawa za kuua wadudu kila mara unapofanya usafi wa banda.

Tenga kuku wapya kutoka nje ya shamba lako kwa angalau wiki mbili. Kwa njia hii, unalinda kuku wako kutoka kwa vimelea ambavyo vinaweza kuletwa kutoka shamba zingine.

ANGALIZO: Kukizuka maambukizi ya magonjwa, ondoa na kuchoma au kuzika kuku wote waliokufa.

Kuwa na daktari wa mifugo karibu kwa ajili ya mashauriano kila wakati unapoona dalili au kushuku kuku wako ni wagonjwa.

Ungana na wafugaji wengine

Pengo moja kubwa katika kukuza sekta ndogo ya kuku nchini ni vikundi, mashirika na majukwaa ya wafugaji kuku dhaifu. Mashirika ya wakulima yaliyopo yameundwa vibaya, viongozi ambao hawana maono na uzoefu wa kibishara, na uwezo wa kujenga na kudumisha makundi.

Ungana na wafugaji wengine ili kuweka mifumo thabiti ya kuzalisha kuku wa hali ya juu. Hii itawawezesha kufikia soko za mbali, kununua chakula cha kuku kwa wingi na kwa bei ya jumla. Mnaweza kutengeneza chakula cha kuku, na kununua malighafi kwa bei ya chini. Pia, kuna nafasi ya bishara ya kuuza chakula cha kuku mlichotengeneza au malighafi kwa wafugaji wengine katika eneo lako na kwingineko. Hii itaongeza njia za kikundi kupata faida.

Wekeza faida

Usiuze kuku mmoja mmoja. Uza kuku wengi mara moja ili upate pesa ya kufanya jambo la maana. Uza wakati bei katika soko iko juu kabisa. Fuatilia soko la kuku ili kujua mfumuko wa bei. Hii itakuwezesha kuepuka hasara. Jambo la muhimu ni kuwekeza sehemu ya faida kwa kuongeza idadi ya kuku, kuboresha malisho, makazi na dawa za chanjo, na matibabu ikiwa magonjwa yatazuka.

Unaweza kutumia mapato kutoka kwa mayai kulipa gharama za kila siku za kuendesha ufugaji, na pesa kutoka kwa mauzo ya kuku kupanua biashara yako ya kuku. Hakikisha tu, hauli kuku anayetaga yai la dhahabu. Utakuwa unazika biashara yako.

Chukua hatua

Je, wewe ni mfugaji wa kuku? Ni mikakati gani unatumia kupanua ufugaji wako na kuongeza mapato? Wasiliana nasi ili tuwashirikishe wafugaji wengine uzoefu wako.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *