- Mifugo

Jinsi ya kutega nyuki wakubwa kuingia kwenye mzinga

Sambaza chapisho hili

Ufugaji wa nyuki ni moja ya miradi mikubwa inayofanywa na wafugaji wengi kwa lengo la kujipatia kipato. Ufugaji huu umekuwa ukihusisha ufugaji wa nyuki wadogo na wakubwa kupta asali, nta, sumu pamoja uuzaji wa mizinga.

Wafugaji wengi wamekuwa wakikwama kupata nyuki katika mizinga yao pindi wanapokamilisha utengenezaji wa mizinga kutokana na kukosa maarifa ya utegaji nyuki ili waingie ndani ya mzinga.

Utegaji wa nyuki

Ili kutega nyuki waingie na kuishi ndani ya mzinga kunahitajika utaalamu wa hali ya juu sana ambapo wafugaji wa nyuki wanatakiwa kufahamu. Wapo ambao hukwama kutega na kujikuta wakipoteza fedha nyingi kukodi watu kuwasaidia kutega mizinga yao ili nyuki waingie kisha wao kuanza tu kufuga.

Aidha wafugaji wapya pia wengine wamekuwa wakitega bila kupata mafanikio kutokana na kukosa ujuzi huu, hivyo basi kupitia makala hii wataweza kujifunza namna ya kufanikisha utegaji na nyuki kwa ufasaha na kwa urahisi.

Hatua za utegaji

Mara baada ya kukamilisha utengenezaji wa mizinga yako, isafishe na kuhakikisha haina uchafu wala unyevu ndani yake kisha;

  • Chukua nta ya nyuki kisha iyeyushe kwenye chombo kwa kuichemsha na uweke kwenye mchirizi ya viunzi (fremu) ya mzinga.
  • Chukua majani aina ya malumba/manuka kisha sugulia kuta za ndani ya mzinga wako na ondoa mabaki ya majani ili kuacha mzinga ukiwa safi.
  • Chukua kigae au kipande cha bati na weka mkaa unaowaka moto kicha chukua vipande vya nta na majani hayo (malumba) na uyachome kufukiza ndani ya mzinga.
  • Funika vyema mzinga na ikiwezekana ziba njia ya kutokea nyuki kwa muda ili moshi unaofukiza uweze kuene ndani ya mzinga, kisha baada ya moshi kuisha funua mzinga na utoe moto ulioweka kufukiza.
  • Chukua mzinga na tundika juu ya mti au eneo maalumu ulilochagua nyuki waingie.
  • Hakikisha wakati wa kutundika mzinga mlango wa mzinga unakuwa mashariki au magharibi.
  • Tega mizinga ya nyukia kuanzia miezi ya Agosti hadi Aprili (Machi na Aprili ndiyo vipindi vizuri zaidi kwa upataji makundi ya nyuki).
  • Kagua mizinga kila mara ili kutambua kama nyuki wameingia ndani hakikisha hakuna wadudu kama buibui kwani wanaweza kusababisha nyuki kutoingia ndani ya mzinga ama kuingia na kutoa.

 

 

Usitege kwa kutumia vitu hivi

Baadhi ya wafugaji kutokana na kukosa maarifa hutega mizinga kwa kuweka vitu ambavyo husababisha wadudu wengine kuwahi kuingia kabla ya nyuki hivyo mzinga kukosa nyuki. Hivyo wakati wa kutega mzinga;

  • Usitege mzinga kwa kuweka asali
  • Usipake mafuta ya samli
  • Usiweke masega

Ukipaka asali huwavutia sisimizi au siafu ambao hufuata utamu wa asali na ikitokea wakaingia ndani ya mzinga kabla ya nyuki basi tambua nyuki hawatoingia ndani.

Ukiweka masega ndani pia haifai kwani yanaweza kusababisha kuzaliana kwa vipepeo haraka na hivyo kuwakwamisha nyuki kuingia.

Zingatia

Pamoja na kukamilisha utegaji wa mizinga ni lazima uhakikishe unachagua eneo ambalo ni mapito ya nyuki, hivyo kabla ya kuweka mizinga eneo unalotega hakikisha unaangalia na kuona nyuki wanapita eneo hilo kwa safari zao za kawaida.

  • Weka mizinga katika eneo la vichaka vyenye miti ya maua
  • Tundika mizinga juu ya miti kiasi cha urefu wa mita 150 hadi 200 kwenda juu.
  • Funga mizinga vizuri kuhakikisha hautaanguka iwapo kutatokea namna yoyote.
  • Uning’inize mzinga upande kidogo ili kuupa mteremko kutoruhusu maji ya mvua kutuama na kuingia ndani ya mzinga.
  • Kama eneo hilo lina upepo mwingi mlango ukae kukinzana na uelekeo wa upepo.
  • Paka grisi nyaya ulizotumia kutundikia mzinga kuzuia sisimizi kuingia ndani ya mzinga.

Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana na mtaalamu na mfugaji wa nyuki na mwandishi wa makala hii Bw. Fredrick Katulanda kwa namba+255622 642620.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

2 maoni juu ya “Jinsi ya kutega nyuki wakubwa kuingia kwenye mzinga

  1. Nimependa makala ya Nyuki,hata hivyo nataka kujua ufanisi wa mizinga inayowekwa kwenye mabanda

    1. Habari.
      Karibu sana Mkulima Mbunifu. Hii inategemea na mizinga yenyewe wewe unachukulia wapi ama imetengenezwaje?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *