- Kilimo Biashara, Mifugo

EMAS: Kirutubishi chenye matumizi mengi kwa mkulima

Sambaza chapisho hili

Mlima bora ni yule anayetumia malighafi sahihi ili kuzalisha mazao mengi yenye tija na salama kwa chakula.

EMAS ni nini?

EMAS Effective Micro Organisms Active Solution ni namna nyepesi ya kutengeneza bakteria wazuri ama rafiki kwa njia ya kimiminika ambacho ni rahisi kutumia na pia ni salama.

Mahitaji

  • Maziwa Fresh lita 10
  • Maji ya mchele lita moja
  • Molasesi lita 10
  • Hamira vijiko 3 vya chakula
  • Maji safi lita moja
  • Glovu
  • Mwiko
  • Jagi la plastiki
  • Ndoo mbili za plastiki zenye mifuniko
  • PH mita

Utengenezaji

  • Chukua lita moja ya maji ya mchele
  • Weka kwenye jagi la plastiki
  • Funika vizuri weka sehemu yenye kivuli kwa siku saba
  • Chuja kupata maji (chukua maji ya juu tu).
  • Chukua maziwa freshi lita 10 yaliyokamuliwa chini ya masaa manne, kisha yaweke kwenye ndoo ya plastiki na changanya na lita moja ya maji ya mchele
  • Koroga vizuri kwa mwiko kisha funika isipitishe hewa na weka ndani ya nyumba sehemu yenye utulivu na pasiwe na mwanga wa jua. Acha kwa siku saba.
  • Mara baada ya siku saba vaa glovu kisha funua ndoo kwa utaratibu na utaona matabaka matatu, juu utapata siagi, katikati maji na chini maziwa mtindi.
  • Chuja vizuri kupata maji kisha changanya na molasi yaani lita 10 ya maji kwa 10 ya molasi.
  • Weka hamira kidoga kisha koroga na funika vizuri na kuweka sehemu yenye kivuli kwa muda wa siku saba.
  • Baada ya siku saba, funua ndoo kisha pima EM ili kujua iwapo inafaa kwa matumizi. Kipimo kinatakiwa kusoma kati ya 3.2 mpaka 3.8 hapo utapata EM ambayo ni hatua ya awali muhimu. EM hiyo inauwezo wa kukaa mwaka mmoja bila kuharibika.
  • Baada ya kupata EM lita moja, Molasi lita moja na 18 za maji kisha funika vizuri na hifadhi sehemu yenye kivuli kwa siku saba zingine.
  • Baada ya siku saba tayari utakuwa umepata EMAS tayari kwa matumizi na haitakiwi kukaa zaidi ya mwezi mmoja. Hivyo basi, EMAS ni mchanganyiko wa EM, Molasi na maji.

Matumizi

Mchanganyiko wa EMAS mililita 10 ukichanganywa na maji lita 15 hutumika kwa kazi zifuatazo;

  • Kunyunyiza kwenye banda la mifugo ili kuondoa harufu, wadudu wanaoruka na bakteria wabaya.
  • Kuogeshea mifugo ili kuwaepusha na kupe, viroboto na papasi.
  • Kuchanganya kwenye chakula cha mifugo.
  • Kuweka nje ya mlango wa kuingilia kwenye banda kanyaga kabla ya kuingia bandani.
  • Kuchanganya kwenye maji ya kunywa ya mifugo.
  • Kunyunyuzia shambani ili kuurutubisha udongo.
  • Kunyunyuzia kwenye mmea dhaifu kuupa afya na kuustawisha (kama busta).
  • Hutumika kwenye bwawa la samaki.
  • Kunyunyiza kwenye eneo lenye kinyesi cha mifugo ili kuzuia harufu.

 

Tahadhari

Iwapo mtumiaji wa EMAS atashindwa kuzingatia vipimo hivyo kuna athari mbalimbali zinazoweza kujitokeza na kusababisha hasara ni pamoja na;

  • Ardhi kushindwa kurutubisha mazao.
  • Mmea kutostawi na kuleta matokeo chanya.
  • Kukaribisha wadudu na kutoa harufu mbaya kwenye banda la mifugo.
  • Kusababisha minyoo na maradhi ya tumbo kwa mnyama iwapo atakunywa maji yenye EMAS.

Ushauri

Maji ya EMAS yakishakorogwa kwa matumizi, yatumike ndani ya saa 24 tu. Ndoo yenye EMAS ifunikwe vizuri wakati wote.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *