- Mifugo

Je, unawatendea haki kuku wako kulinda afya zao na yako

Sambaza chapisho hili

Kumekuwa na imani potofu kutoka kwa watu wengi ikiwamo mafunzo ya kigeni kuwa ufugaji wa kuku kwenye vibanda vidogo vya chuma visivyowapa nafasi ya kutoka ndiyo ufugaji wa kisasa wenye tija jambo hili ni hatari na ukiukwaji wa haki za wanyama.

Kuku ni aina ya ndege wanaofugwa na binadamu kwa madhumuni mbalimbali. Asili ya ndege hawa kama ilivyo kwa wengine ni kuwa huru, kujitafutia chakula na kufurahia kuruka hapa na pale.

Aina hii ya ndege kwa imekuwa chanzo kikubwa cha ujasiriamali kwa ngazi ya familia katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania. Hali hii imefanya uwepo wa aina mbalimbali za ufugaji ili tu kuhakikisha kuwa wafugaji wananufaika na kupata faida kutokana na kuku.

Kuhakikisha kuwa mfugaji anapata faida ni jambo jema sana kwa kuwa ndiyo lengo la kila anaefanya kazi na kuwekeza kwenye miradi aweze kupata faida.

Jambo muhimu na la msingi wafugaji wanalopaswa kufahamu ni kwamba ndege hawa wanapaswa kutendewa haki kama ilivyo kwa aina nyingine yoyote ya viumbe hai, ikiwa ni pamoja na kupata mahitaji muhimu kama vile chakula, maji, mahali salama pa kuishi na nafasi ya kutosha ili waishi kwa uhuru.

Kuku wanapofugwa kwa namna nyingine mfano kwenye vizimba vidogo huwaondolea uhuru na uasili wao. Kuwafuga kuku kwenye vizimba visivyokuwa na nafasi huathiri afya zao kwa kiasi kikubwa, kusababisha vilema na hata vifo.

Kuku wanapokuwa dhaifu kiafya, kushambuliwa na magonjwa n ahata kufa huathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kiuchumi na kiafya kwa mfugaji. Hii ni kwa sababu humlazimu kutumia madawa mengi kuwatibu kuku isivyotakiwa na dawa hizo mara nyingi ni ghali na hatari kwa afya za walaji.

Hali hii inatamkwa kuwa ni ukatili dhidi ya wanyama. Ni vizuri kuku wakafugwe kwenye eneo lenye uhuru endapo mazingira hayaruhusu kuku hao kufugwa kwa mtindo huria. Ni muhimu kuepuka kufuga kuku katika vibanda vidogo visivyowapa uhuru.

Madhara yatokanayo na ufu­gaji kwenye vibanda visivyo na nafasi

  • Kuku huonekana wenye msongo ambao mara nyingi husababisha kujidonoa au kudonoa vyuma vya viambaza ambavyo huwasababishia maumivu.
  • Ni kinyume cha sheria kwani huwaondolea haki yao ya msingi ya kuishi kulingana na mazingira waliyoumbwa.
  • Kufingiwa kwenye vizimba huathiri maumbile yao kwani husababisha ulemava na aina nyingine ya madhara kama vile kunyonyoka.
  • Vizimba hutoa nafasi ndogo sana kwa kuku, hali inayowaondolea uhuru wa kulala, kuruka na kuchakura.
  • Husababisha upungufu wa virutubisho muhimu mwilini.
  • Husababisha msongo unaombatana na uzalishaji hafifu na mara nyingi vifo.

Je, mfugaji afanye nini?

  • Hakikisha kuku wana banda zuri linalofaa kutumika wakati wote kwa usalama wao.
  • Hakikisha kuna nafasi ya kutosha kwa kila kuku.
  • Wape chakula cha kutosha
  • Kila wakati maji yawemo kwenye eneo lao.
  • Wawekee kuku miti au sehemu za kupanda na kulala nyakati za usiku.
  • Kamwe usishawishiwe kutumia vibanda vidogo kuwafungia kuku.
  • Hakikisha unalinda afya ya mufugo yako kwa kufuata kanuni na sheria.

Endapo mfugaji atazingatia mambo hayo, basi atakuwa ameepukana na ukatili dhidi ya mifugo yake, lakini pia atajiongezea nafasi kubwa ya kupata mayai na nyama iliyo salama bila vimelea vya magonjwa.

Makala hii imeandaliwa kwa kushirikiana na shirika la ustawi wa wanyama Tanzania -EAAW.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *