- Mifugo

Fuata vidokezo kuhusu uuzaji wa mifugo ili kupata bei ya juu

Sambaza chapisho hili

Wafugaji wengi hawaelewi mienendo ya soko la mifugo. Wanaishia kuuza wanyama kwa bei ya chini wakati wanyama wale wale wangeweza kupata bei nzuri ikiwa mfugaji angekuwa mvumilivu na kuchukua muda kuelewa mwenendo wa soko na kuzingatia kanuni muhimu za uuzaji.

Usifanye mauzo ya wanyama wachache na ya muda mfupi au kushtukiza. Hii ni kwa sababu mauzo yasiyo rasmi ni njia rahisi ya kuboresha upatikanaji na mtiririko wa hela shambani kwa muda lakini inasumbua katika upangaji wa bajeti na kuweka mipangilio ya uzalishaji wa muda mrefu.

Hivyo basi, fanya mpango mahususi wa kuuza mifugo wakati ambapo kuna uhitaji mkubwa katika soko na bei ni ya juu. Pia, uza mifugo kwa pamoja ili upate hela nyingi kwa wakati mmoja. Unapofanya hivi, unapata hela za kuwekeza na kupanua biashara yako ya ufugaji.

Wachuuzi wengi wanapendelea kununua wanyama kadhaa na kuwakusanya pamoja ili kurahisisha usafirishaji kwenda kwenye masoko ya mbali. Ukiwa mfugaji mdogo na una dume mmoja au kondoo wawili basi unatakiwa kuungana na wafugaji wengine.

 

Breeder in body condition score 5

Unganisha juhudi kwa kuunda kikundi

Jambo rahisi kufanya ni kupanga na wafugaji wengine na kuunganisha mifugo wa kuuzwa kabla ya kutafuta au kuwasiliana na mnunuzi. Ni muhimu kuhakikisha kwamba kila mfugaji katika kikundi cha kujumuisha mifugo anakubali tarehe ya kuuza.

Pia, hakikisha kuwa mifugo iliyokusanywa pamoja wapo katika hali nzuri kiafya. Mifugo wachache wagonjwa ama hafifu wanaweza kufanya kundi zima kuonekana duni na kushusha bei, na kuathiri mapato kutokana na mauzo.

Lisha wanyama vizuri wiki au miezi kadhaa kabla ya siku ya uuzaji. Na kabla ya kufanya hivyo, wape dawa za kuwaua vimelea vya ndani (minyoo) na kuwaogesha dhidi ya vimelea vya nje (kupe) ambavyo vinaweza kuathiri mchakato wa kunenepesha dume na mifugo aina nyingine.

Dadisi na kujua bei za sasa za kila kilo ya nyama katika soko kisha uhesabu ni kiasi gani unaweza kupata kwa kila mnyama wako. Njia rahisi ya kufanya hivyo ni kutumia bei ya uzito wa mnyama, ambapo mnyama hupimwa uzito na kunakiliwa mfugaji akiwa hapo.

Kwa kawaida, bei ya mifugo huwa chini sana wakati shule zinafunguliwa Nyakati hizo, wazazi wengi wanawauza mifugo wao ili kutafuta fedha za kulipa karo. Hivyo, uhitaji wa mifugo sokoni ni duni kulingana na idadi ya wanyama wanaoletwa kwenye soko. Kama unauza, uza mapema kabla ya msimu huo wa kufungua shule. Kama unanunua, basi huu ni wakati bora wa kupanua ufugaji wako kwani wanyama wengi wanaletwa sokoni, na kuna uwezekano mkubwa wa kupata wanyama wazuri kwa bei nafuu.

Katika kikundi chako, anzisha timu ya uuzaji ambao watakuwa na jukumu la kutafuta wanunuzi, kufuatilia bei ya sasa na ya baadaye, kujadili na kukubaliana bei kulingana na mwenendo uliopo wa soko. Hii inamsitiri mfugaji kutokana na mfumko wa bei.

Nyama iliyonona

Mifugo wote hawawezi kuwa na thamani sawa. Wanyama wembamba na waliokonda wanauzwa kwa bei ya chini wakilinganishwa na wale wachanga, wenye mwili mkubwa na walionona.

Kuna viwango tofauti vya bei kulingana na umri wa mnyama na hali ya mwili (kama mifupa imefunikwa vizuri kwa nyama na mafuta). Wanyama wembamba au wakubwa watapewa bei ya chini sana kuliko wanyama wachanga au wanene.

Kuna aina tofauti za bei kulingana na umri wa mifugo na hali ya mwili (kifuniko cha mafuta), na mifugo tofauti pia itachukua bei tofauti. Wale wembamba na waliokonda watanunuliwa kwa ajili ya kutengeneza supu ya mifupa. Hivyo, juhudi za kunenepesha wanyama kabla ya kuwapeleka sokoni ni muhimu sana katika kuongeza kipato cha mfugaji.

Chukua hatua

Kuwa na ujuzi wa kuuza kwa kujua hali ya mwili wa mnyama ni muhimu kwa mfugaji. Hata hivyo sio rahisi kwa wafugaji wenye uzoefu mdogo. Hivyo, jifunze ili uepukane na hasara. Unaweza kufanya hivi kwa kushauriana na wafugaji ambao tayari wako na uzoefu, na wako tayari kukufundisha wewe na kikundi chako ujuzi muhimu wa uuzaji. Unaweza pia kuwasiliana na afisa mifugo na uuzaji katika wilaya ama tarafa yako.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *