- Mifugo

Boresha mikakati ya kutunza ng’ombe wa nyama

Sambaza chapisho hili

Tanzania ina uwezo mkubwa wa ufugaji wa ng’ombe wa nyama jambo ambalo linaweza kupelekea wakulima wadogo kupata fedha ikiwa watafanya usimamizi wa hali ya juu kuzalisha nyama kwa muda mfupi.

Hata hivyo, malisho na maji bado ni changamoto kwa ufugaji wa ng’ombe wa nyama nchini kwani nyasi huwa nyingi wakati wa msimu wa mvua na hupunguka wakati wa kiangazi.

Ili kuwaweka wanyama katika hali nzuri kwa mwaka mzima, wafugaji wa nyama lazima wahifadhi nyasi na aina zingine za malisho na kuweka idadi ya wanyama.

Usimamizi

Waogeshe mara kwa mara ili kuepukana na magonjwa yaenezwayo na kupe pamoja na ndorobo. Uogeshaji unaweza kufanyika kwa kutumia pampu za mgongoni (knapsack sprayers) au kuwatumbukiza katika josho lililotiwa dawa ya kuogeshea.

Wape dawa za minyoo mara kwa mara ili kuhakikisha ukuwaji wao unaendelea vizuri. Wape dawa hii kila baada ya miezi mitatu

Wape ndume namba au alama za utambulisho mara wafikiapo miezi 6 tangu kuzaliwa. Utambulisho unaweza kuwa wa chuma au plastiki chenye nambari kwenye sikio, mikato maalumu katika masikio au chapa katika sehemu maalum za mwili.

Ulishaji

Lengo kuu ya ulishaji wa ng’ombe wa nyama ni kuongeza kasi ya kukua na kuongeza uzito kwa haraka. Mfugaji asitegemee tu malisho peke yake ambayo hayawezi  kukidhi  mahitaji ya lishe hasa katika miezi ya mwisho kabla ya kuuza ng’ombe kwa soko.

Nyasi ni chakula cha gharama ya chini kwa ulishaji wa ng’ombe. Kwa mfumo huria, wapeleke kwa ndume kwa malisho na kama hauna eneo la malisho basi nyasi iliyokatwa na hifadhiwa (hay). Wapate ya kutosha. Kwa kawaida, ng’ombe wanalishwa vipimo sawa na 3% ya uzani wa mwili. Ng’ombe wa kilo 250 atahitaji angalau kilo 9 ya hay. Na kama unamlisha nyasi ya Napier basi atahitaji angalau kilo 50. Pia, ongeza mikunde kama vile desmodium, lusina, au majani ya miti kama kalindra ambazo ni vyanzo vya protini.

Sileji ni chakula chenye nguvu na inaweza kutumiwa baadaya ya ndume kutoka kwenye malisho. Ng’ombe wa kilo kilo 250 atahitaji angalau kilo 20 ya sileji. Uamuzi wa kulisha sileji kwa wanyama wa nyama hutegemea na gharama ya uzalishaji wake. Ikiwa gharama ni ya juu, basi achana nayo.

Lisha chakula cha ziada ili  kukidhi  mahitaji  ya kukua kwa haraka na kujaza nyama kwa muda   wa  miezi  3 – 6  kabla  ya  kuchinjwa. Nunua au fanya mchanganyiko wako mwenyewe shambani kulingana na malighafi. Cha muhimu ni chakula chanzo cha nguvu mwilini. Unaweza kuchanganya ifuatavyo;

Malighafi Kiasi  (Kilo)
Mahindi (iliyosagwa au pumba) 67
Mashudu  ya  alizeti/pamba 20
Unga  wa  soya 10
Chokaa  ya  mifugo 2
Chumvi 1
Jumla 100

 

Kumbuka chakula cha ziada inatumika kunenepesha kabla ya kuuza ili kufikia uzito wa kilo 300-400. Hivyo, hakikisha unanenepesha ndume ambaye amefikisha angalau kili 250. Ndumu huyu atahitaji chakula cha ziada kilo 3-6 kwa siku. Wanyama wanaolishwa kwa njia hii hutoa nyama bora laini, yenye ladha nzuri. Ukilisha chakula cha ziada kwa muda mrefu, gharama itakuwa juu na faida kupungua.

 

Sehemu ya kulishia

Haijalishi ukubwa wa shamba lako, kutumia mfumo maalum wa kulisha itakusaidia kwa njia nyingi hasa unapowalisha ndume wako chakula cha ziada. Ukijenga mabwawa ama chombo cha kulishia, malisho hayatapotea wakati wanapewa, na ng’ombe watazoea baada ya muda. Unaweza kujenga ukitumia mbao, chuma, ama matofali na saruji. Italingana na uwezo wako kifedha. Ukubwa wake itategemea idadi wa ndume unaowalisha.

Kwa kutumia mabwawa ya kulisha, utapata kulisha wanyama kadhaa kwa wakati mmoja na uamue ni nini au ni kiasi gani cha chakula kinaongezwa kwenye chombo hicho ili uweze kudhibiti kiasi ya malisho ambayo wanaweza kula. Zaidi, zitakusaidia kuweka shamba lako likiwa limepangwa na kukurahisishia kuweka rekodi ya ulaji wa ndume wako.

Vifaa vya maji

Ng’ombe wapatiwe maji safi na ya kutosha. Uchafu unaweza kusumbua shughuli za mmeng’enyo wa chakula au kusababisha maradhi. Maji yakiwa baridi sana, ng’ombe watashindwa kunywa ya kutosha. Jenga birika ya kunywa maji ili kupunguza maji kupotea. Upana bora ni karibu sentimita 20. Hii inaruhusu wanyama kunywa kwa urahisi na hupunguza hatari ya wanyama kuanguka ndani ya birika.

Mpango wa afya

Ndume hawapendi kusumbuliwa, kwa hivyo washughulike kwa uangalifu. Kuwa na daktari wa mifugo karibu ili kuwakagua mara kwa mara hasa ndume wapya kabla ya kuchanganya na ndume wengine. Wape chanjo dhidi ya magunjwa sugu katika maeneo yako na dawa dhidi ya vimelea vya ndani kama minyoo. Kupe na ugonjwa wa ndigana ni moja wapo ya tishio kubwa kwa ng’ombe.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

7 maoni juu ya “Boresha mikakati ya kutunza ng’ombe wa nyama

  1. Nategemea kuanza ufugaji wilaya ya Bagamoyo. Huku maji ni ya chumvi chumvi. Je yanafaa kwa ufugaji?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *