- Mifugo

Fahamu vyakula bora ambavyo unaweza kulisha kuku

Sambaza chapisho hili

Mkulima Mbunifu limekuwa mara kwa mara likichapisha taarifa za kina kuhusu ufugaji bora wa kuku, ikiwa ni pamoja na matunzo yake. Mara nyingi makala hizo zimekuwa zikilenga kuku wa asili na namna ya kukabiliana na changamoto zinazowakumba wafugaji.

Hatua kwa hatua makala hizo zimeweza kuwasaidia wafugaji na hatimae kuwa na ufanisi. Katika muktadha huo huo, makala hii itamsaidia mfugaji kuweza kutambua ni aina gani ya vyakula ambavyo anaweza kulishia kuku na ambavyo havitakiwi.Moja ya changamoto kubwa katika ufugaji wa kuku ni gharama za chakula. Hii ni kutokana na vyakula vinavyozalishwa maalum kwa ajili ya kuku kuwa na gharama kubwa na mara nyingine upotevu wa chakula hicho kuwa mkubwa kutokana na muundo wake.

Kutokana na hali hiyo, wafugaji wamekuwa wakitafuta njia mbadala za kulisha kuku, hali ambayo kwa kiasi fulani imesababisha ulishaji kuwa holela.

Ili kuepukana na hali hiyo ni muhimu mfugaji kufahamu ni aina gani ya vyakula anapaswa kulishia kuku na vile ambavyo havitakiwi.

 

Vifuatavyo ni aina ya vyakula ambavyo mfugaji anaweza kulishia kuku;

  • Ndizi zisizo na maganda. Hakikisha unamenya ndizi hizo kwani maganda hayafai.
  • Kabichi, chainizi, spinachi, mchicha, mnavu, majani ya maboga, majani ya kunde, dengu na majani ya maharagwe.
  • Karoti mbichi na majani yake.
  • Mahindi, mtama, ngano, uwele, shayiri na ulezi.
  • Nyama na mifupa: Mifupa na nyama ipikwe na kukaushwa vizuri. Usiwalishe kuku nyama mbichi.
  • Vyakula vya baharini kama vile dagaa. Chemsha na kukausha. Vyakula hivi mara nyingi huwa na vimelea vya magonjwa kama vile Salmonella enteritidis hivyo ni vyema tukachemsha.
  • Parachichi, tufaa(apples), pears, zaituni, maboga, tikiti maji n.k. Usiwape kuku mbegu za tufaa na zaituni kwani zina kiwango kidogo cha cyanide ambayo ni sumu kwa kuku.
  • Minyoo na funza. Zalisha aina hii ya wadudu kwani ni chanzo kizuri cha protini kwa kuku.
  • Pilipili; pamoja na kuwa sehemu ya chakula lakini pia hutumika kama dawa.
  • Pumba za mahindi, mpunga, ngano. Pumba za mpunga zisizidi asilimia 12 ya chakula.
  • Mabaki ya chakula. Yawe safi na yasiyooza, yasiwe na ukungu, mafuta na chumvi nyingi.
  • Mashudu ya pamba, alizeti
  • Machicha ya nazi
  • Njegere, dengu, kunde, njugu, karanga na ngwara.
  • Viazi mviringo/ viazi vitamu/ magimbi. Vipikwe na kukaushwa ili kuondoa sumu ndani yake. Epuka maganda ya kijani yana sumu nyingi.
  • Mihogo: Usiwape kuku mihogo mibichi wala iliyokaushwa. Loweka kwenye maji siku 3-5 kuondoa sumu katika mihogo kisha kausha na uwape kuku.
  • Mchele: Unaweza chemsha au kuwalisha ukiwa mbichi hivyo hivyo. Unaweza wapa punje ama maji yaliyooshea mchele. Usizidi asilimia 20 ya chakula
  • Maharagwe: Yawe mabichi au yaliyopikwa na siyo makavu. Najua wengi tumesikia soya kwa chanzo cha protini lakini pia inapaswa kufanywa hivyo

ZINGATIA: Vyakula vingine vinahitaji uchakataji mdogo ili kuku wapewe. Uzembe na kutojali huweza kusababisha hasara. Kumbuka aina moja ya vyakula inaweza wakapewa wanyama wengine wasiwe na madhara. Hii inategemea na uimara wa mifumo ya utoaji sumu mwilini. Mfano nguruwe anaweza kulishwa maganda ya viazi mviringo asipate madhara. Japo hata kwa nguruwe huwa inashauriwa yapikwe.

Kuepusha magonjwa kwa kuku zingatia mambo haya yafuatayo

  • Safisha vyombo vya kulishia na kunyweshea kila siku.
  • Osha, sugua vizuri, kisha suuza kuondoa utando unaobeba bakteria.
  • Kuku wanahitaji wapewe chakula cha kutosha na chenye virutubisho vyote.
  • Unaweza kuwaongezea majani, makombo, nafaka, mchanga laini, au maganda ya mayai.
  • Wapatie kuku maji safi muda wote.
  • Wafugaji wengi wameripoti kuwa na matokeo mazuri baada ya kuchanganya dawa ya kuua vimelea kwenye maji ya kunywa.
  • Nunua chakula kwa wauzaji wazuri na wanaoaminika ili kuepuka minyoo na sumu hatarishi.
  • Usiwape kuku chakula chochote kinachoonekana kuoza au kunuka uvundo.
  • Hifadhi chakula cha kuku katika sehemu kavu isiyo na joto na isiwe kwa zaidi ya miezi mitatu ili kuepuka kuharibiwa na fangasi.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

4 maoni juu ya “Fahamu vyakula bora ambavyo unaweza kulisha kuku

    1. Hi, thank you for your message and thanks for keeping follow up and reading MkM magazine content.
      Yes, you will and are mostly welcome

    2. Nimewahi soma sehemu nyingine wakisema – mchele lazima upikwe kidogo ndipo uwape kuku. kuna sababu walitoa- kwamba mchele mbichi unaweza kuvimba ndani ya tumbo la kuku.

      1. Habari,

        Hatuna uhakika na habari hiyo ila tutalifanyia kazi kujua kama ni kweli na unaleta shida gani

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *