- Mifugo

Fahamu ugonjwa wa minyoo kwa mbuzi na namna ya kudhibiti kwa dawa za asili

Sambaza chapisho hili

Afya ya mbuzi hutokana na lishe bora inayopatikana kwa kulisha majani mabichi, majani makavu, vyakula vya ziada vya kutia nguvu, protini, madini, vitamini na maji safi nay a kutosha ya kunywa.

Usafi wa banda unaojumuisha hori la kulia, vyombo vya kulishia pamoja na ndoo au vyombo vya kunywea maji pia ni sehemu ya kutunza afya ya mbuzi.

Mbuzi anapoachiwa kufanya mazoezi kwa kuzungukazunguka katika banda kubwa lenye nafasi ya kutosha ama kuachiwa huru kwenye uwanja humsaidia kuimarisha afya yake.

Minyoo kwa mbuzi

Ugonjwa wa minyoo ni moja ya tatizo kubwa linalowakumba sana mbuzi huku madhara yake yakiwa ni makubwa hasa kupungua kwa kasi ya kukua na hasa kupelekea vifo kwa wale mbuzi wenye umri mdogo.

Aina za minyoo

  • Minyoo mikubwa ya mviringo inayoishi kwenye tumbo na utumbo.
  • Minyoo midogo ya mviringo inayoishi pia kwenye tumbo na utumbo.
  • Minyoo bapa inayojulikana kama tegu ambayo huishi kwenye utumbo.
  • Minyoo inayoishi kwenye maini.
  • Minyoo inayoishi kwenye mapafu.

Kati ya jamii hizi za minyoo, aina inayosumbua sana mbuzi ni ile ya jamii za mviringo aina kubwa na ndogo.

Namna mbuzi wanavyopata minyoo

Kwa kawaida mbuzi huwa na matumbo manne, na utumbo wa nne ambalo ndilo la mwisho na ambako ndiko chakula huanza kufyonzwa na kuingia mwilini ndiko ambako minyoo hupendelea kuishi na kutaga mayai ambayo hutoka nje pamoja na kinyesi.

Mayai hayo yakitoka kupitia kwenye kinyesi, kama hali ya hewa ikiwa nzuri yaani yenye unyevu huanguliwa kisha minyoo midogomidogo hutokea na kuishi kwa kutumia mvuke au unyevu ulioko kwenye nyasi/majani.

Katika nyakati ambazo hazina jua kali minyoo hiyo hujibanza sehemu za juu za nyasi hivyo mbuzi wanapokula nyasi ambazo bado zina umandi basi humeza minyoo hiyo.

Kwa kuwa mbuzi hatafuni nyasi mara tu baada ya kuzikata basi minyoo hiyo huendelea kuwa hai na kuishi katika utumbo wa nne na hatimaye hutaga mayai ambayo baadaye hutoka na kinyesi kisha mzunguko wa maisha huanza tena.

Dalili zinazoonyesha mbuzi ana minyoo

  • Mbuzi huwa na afya mbaya
  • Manyoya huwa yamesimama na hayapendezi
  • Mbuzi wadogo huharisha
  • Hata ikiwa mbuzi amekonda, basi huonekana kuwa na tumbo kubwa
  • Mbuzi hupungukiwa damu

Namna ya kuzuia minyoo

  • Mbuzi wapewe dawa yam inga dhidi ya minyoo kila baada ya miezi mitatu na hasa wakati wa masika. Kwa watoto wa mbuzi wenye umri kati ya wiki sita hadi miezi mitano wapewe dawa za kinga ya minyoo kila mwezi.
  • Mbuzi wasilishwe kwa kufungwa Kamba mahali pamoja kwa muda mrefu. Kama mfugaji atalazimika kumlisha mbuzi kwa kumfunga kamba, basi abadilishe eneo la kumfunga zaidi ya mara tatu kwa siku na maeneo ya kuchunga yapate nafasi ya kukaa bila mifugo kwa kipindi cha wiki sita.
  • Mbuzi wachungwe kwenye maeneo makubwa na siyo sehemu za karibu na nyumba za watu kijijini.
  • Mfugaji asisubiri mpaka mbuzi augue ndipo aanze kumshughulikia, hakikisha mbuzi anapewa kinga kumlinda kuugua.

Dawa za asili za minyoo

  • Lukina/Lusina: Mbegu za kijani za lukina hutumika kutibu ugonjwa huu, yaani kwa kutwanga mbegu 50 hadi 100 ambazo hazijakomaa kisha kuchanganya na maji na kumpa mbuzi robo kikombe mara mbili kwa siku. Rudia kila baada ya miezi mitatu.
  • Ikumburi (kipare): Majani yake hutumika kwa kutwanga na kuchanganya na maji kisha kumpa mbuzi nusu kikombe mara moja kwa siku na kisha kurudia kila baada ya miezi mitatu.

  • Ndulele (Solanum incanum): Mizizi yake hutumika kwa kutwanga kiasi kidogo kisha kukamua maji yake na kumnywesha mbuzi kama nusu kikombe cha chai.

 

 

 

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

2 maoni juu ya “Fahamu ugonjwa wa minyoo kwa mbuzi na namna ya kudhibiti kwa dawa za asili

    1. Habari,
      Karibu Mkulima Mbunifu na asante kwa kuendelea kutufuatilia na kusoma makala zetu mbalimbali. Kuhusu busta ya ng’ombe ngoja tulifanyie utafiti tuone kama ipo ama lah! Ila kwasasa hatuna

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *