- Mifugo

Fahamu afya ya mnyama ili kumkinga na magonjwa

Sambaza chapisho hili

Wanyama walio wengi wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na kukosa msaada kwa wakati pale maradhi yanapowakumba.

Katika Makala zilizopita tuliandika juu ya sifa za mnyama mwenye afya na katika toleo hili tumeona vyema kurudia kuchapisha mada hii ili kuwasaidia wafugaji wengi ambao mara nyingi wamekuwa wakipoteza wanyama kwa ghafla bila kujua tatizo limetokana na nini.

Mfugaji mzuri anatakiwa kujua nini kwa mifugo yake

Mfugaji yeyote anahitajika kutambua tofauti kati ya mnyama mwenye afya na mgonjwa. Sehemu kubwa ya kufahamu dalili za ugonjwa ni kujifunza namna ya kuangalia dalili hasa za mnyama mgonjwa.

Dalili za mnyama mgonjwa mara nyingine mfugaji huweza kugundua kuwa afya ya mnyama wake siyo nzuri kabla ya kuelewa kwa uhakika kiini hasa cha kasoro hiyo.

Inaelekea kuwa kuna hali flani inayojengwa na mnyama ili kumfanya mfugaji ahisi kuwepo kwa tofauti hata kama mnyama hawezi kuwasiliana ana kwa ana na binadamu ili kuonyesha mahali hasa penye maumivu mwilini mwake.

Ili kumsaidia mtaalamu wa mifugo kuelewa kasoro iliyoko, itasaidia iwapo mfugaji atajifunza na kufahamu jinsi ya kuchunguza kasoro zinazoweza kutokea kwa wanyama wake.

Mfugaji anatakiwa kujifunza na kuelewa sifa mbalimbali anazokuwanazo mnyama mwenye afya nzuri.

Sifa za mnyama mwenye afya nzuri ni zipi?

  • Mfugaji anaweza kuchunguza hali ya kujengeka kwa mwili wa mnyama wake, yaani kuona kama ni mkondefu kupita kiasi au ana uzito unaokubalika.
  • Mnyama anatakiwa kuchunguzwa kuona kama ana utulivu wa kawaida na kama anatumia vyema milango yake ya fahamu, kama vile kuona, kusikia sauti au kelele.
  • Mnyama pia anatakiwa kuchunguzwa kuona kama ana uwezo wa kusimama, kutembea, kupumua bila shida na bila kutoa sauti isiyo ya kawaida kwenye mapafu.
  • Hali kadhalika, mnyama anatakiwa kuchunguzwa kuona kama ana uwezo wa kukichukua na kukitembeza kiwiliwili chake bila kuonyesha maumivu na vilele vile kuchanganyika bila shida na wanyama wenzake.
  • Mnyama hatakiwi kuwa na vidonda au michubuko kwenye ngozi na manyoya yake yanatakiwa kuwa laini na yenye kung’aa.
  • Aidha, mnyama anatakiwa kuwa na uwezo wa kula vizuri na kucheua bila shida yeyote.
  • Masikio ya mnyama yanatakiwa kuwa katika hali ya wepesi wa kutaka kusikiliza na pua yake haitakiwi kuwa kavu bali yenye vitone vidogovigodo vya unyevu.
  • Ikiwa mnyama ana mimba kubwa, hali hiyo ya mimba inatakiwa kuonekana na kufahamika kwa uhakika.
  • Wakati wa kupima joto la mnyama kwa kutumia kipimajoto, mnyama ataonekana kuwa na joto la kawaida kama afya yake ni nzuri. Mnyama mwenye afya nzuri anatakiwa kuwa na idadi sahihi ya mapigo ya moyo kwa kila dakika.
  • Ni lazima mnyama mwenye afya avute na kutoa pumzi kwa kasi ya kawaida. Mnyama mwenye afya nzuri, hatakuwa akihema haraka mno au polepole kupita kiasi.
  • Haitakiwi mnyama mwenye afya nzuri kutoa ute au usaha machoni, masikioni, puani, mdomoni, njia ya kutolea mkojo au kutoka kwenye tundu lingine lolote lililopo mwilini mwake.
  • Haitakiwi pia mnyama mwenye afya kutoa harufu isiyo ya kawaida kutoka kwenye sehemu yeyote tajwa hapo juu yenye matundu.
  • Wakati mnyama akiwa kwenye harakati za uyeyushaji wa chakula, ni lazima tumbo (rumen) lionyeshe kutembea tembea mara mbili au tatu hivi kwa dakika. Kama huwezi kuona mienendo hiyo ya tumbo, unaweza kuisikiliza kwa kutumia ngumi kubonyeza upande wa kushoto wa tumbo.
  • Kiwele cha mnyama mwenye afya hakitakiwi kuwa na vipele au uvimbe usio wa kawaida. Aidha kiwele hicho hakitakiwi kuwa na joto kupita kiasi au rangi isiyo ya kawaida.
  • Chuchu za kiwele zinatakiwa kuwa imara, zisizokuwa na uvimbe, mipasuko wala vidonda. Kama ni mnyama anayekamuliwa, ni lazima atoe maziwa meupe kwa urahisi bila ng’ombe kuonyesha maumivu.
  • Mnyama mwenye afya ni lazima awe na uwezo wa kutoa mkojo na kinyesi bila shida yeyote. Ni lazima pia mkojo utakaotolowa uwe wa kawaida, wenye rangi ya njano kidogo na kadhalika kinyesi kiwe cha kawaida kisichokuwa laini mno, au kigumu sana na kisiwe damu na kutoa harufu mbaya.
  • Mnyama mwenye afya nzuri huwa na maji ya kutosha mwilini mwake na kwa ajili hiyo hataonyesha dalili za kushiwa maji mwilini.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *