Katika mazungumzo na vikundi vya wakulima, mmoja wa wakulima walioshiriki katika mkutano wa kubadilishana mawazo kuhusu kilimo hai kama mbinu moja ya kilimo endelevu utafiti, alisema; “Kilimo hakilipi bili tena, na unajua haiwi rahisi.”
Kauli hii ya mkulima huyu inaibua haja ya kufanya kilimo kuwa na maana kwa wakulima. Kwamba wanapofanya kazi wanachuma kutokana na jasho lao, yaani, jinsi ya kubaki katika kilimo wakati ambapo uchumi wa kilimo unashuka. Hii ni pamoja na athari za mbadiliko wa tabia nchi zinazoleta changamoto na kutokuwa na uhakika.
Tunaweza kufanya nini kuboresha hali ya sasa?
Kwa bahati nzuri, kuna fursa kupitia kujifunza kwa ushirikiano. MkM imejifunza hili kusambaza gazeti kupitia vikundi vya wakulima. Katika kujifunza kwa ushirikiano, watu au vikundi vya wakulima hufanya kazi pamoja ili kujenga maarifa. Hii inatokana na nadharia kwamba kujifunza kwa ushirikiano inaruhusu wakulima kujenga maarifa kuhusu masuala mbadala ya kilimo yanayowahusu kimaisha na katika uzalishaji wao.
Kwa mfano, wakulima wanapopokea jarida na kusoma makala kuhusu mada kama vile ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, wanajiuliza nani kati yao tayari anawafuga ng’ombe na anatumia mbinu gani katika usimamizi wa shughuli hii na anapata manufaa gani. Pia, anakumbana na changamoto gani na ni mbinu gani anatumia kupambana na changamoto hizo. Wakulima wanajadili kisha wale wanaojihusisha na ufugaji wanakwenda kufanyia mbinu zile majaribio katika mashamba yao. Vile vile, wanamtembelea mkulima ili kujifunza zaidi na kuona vile mambo yanafanywa moja kwa moja.
Katika mfano huu, hatua zifuatazo zinajitokeza: Soma, eleza, changanua, weka kipaumbele, tenda, leta matokeo au maoni.