- Kilimo

Wafahamu nzige na jinsi ya kuwadhibiti

Sambaza chapisho hili

Nzige huvamia bustani, shamba na ana uwezo wa kuharibu vibaya kabisa. Katika (matukio mengi) nzige hudhibitibiwa na viuatilifu ambazo ni kemikali sumu za kuua wadudu, ambazo si rafiki na mazingira kwani vinauwezo wa kuua viumbe wengine, pia hatari kwa binadamu. Kutumia hatua mbadala na asili kusaidia kudhibiti idadi yao ni vema.

Nzige wa jangwani ni miongoni mwa wadudu wa aina ya panzi wenye papasi (antenna) fupi walioko katika familia kibaolojia ya Acrididae

Wadudu hao wanajulikana kutokana na uwezo wa kubadili tabia na kutengezeza makundi makubwa ya nzige wakubwa au makundi ya tunutu (watoto wa nzige).

Makundi haya huwa makubwa na kuwa na uwezo wa kuruka umbali mrefu. Jina la kitaalamu la nzige wa jangwani ni Schistocerca gregaria.

Wanapokuwa wengi hujikusanya katika makundi makubwa na kusafiri umbali mrefu hata nje ya jangwa. Kutokana na wingi wao, jeshi la nzige linaweza kuhatarisha usalama wa chakula kama wasipodhibitiwa mapema.

Kuna aina takribani kumi za nzige, moja wapo ni hawa nzige wa jangwani. Nzige wa jangwani hufanya uharibifu katika mazao kuliko nzige wa aina yoyote ile. Nzige hawa  huunda makundi ambayo yanaweza kuruka hadi kilomita 150 kwa siku.  Wanauwezo wa kula chakula sawa sawa na uzito wao wenyewe. Nzige mmoja anauzito unaokaridiwa kua gramu mbili (2gram). Ikiwa uvamizi haujagundulika na kudhibitwa wanaweza kuunda kundi kubwa linaloweza kuleta athari mbaya kwa usalama wa chakula.

Maisha ya nzige

Nzige wa jangwani wanaweza kuishi kwa miezi mitatu mpaka minne wanaweza kuishi hata zaidi ya hapo kutegemeana na hali ya hewa na hali ya ikolojia. Mzunguko wa maisha ya nzige wa jangwani una hatua tat yaani yai, tunutu na nzige mkubwa. Mayai huanguliwa baada ya wastani wa kama wiki mbili, tunutu hukamilika baada ya kupitia hatua tano hadi sita kwa kipindi cha siku 30-40. Nzige mkubwa hupevuka ndani ya wiki tatu hadi tisa lakini mara nyingi ni ndani ya miezi miwili – hadi mitatu.

Mpaka sasa hakuna ushahidi wa moja kwa kwaamba uvamizi wa Nzige wa jangwani hutokea kila baada ya kipindi fulani maalum. Ifamike tu kwamba uvamizi wa nzige ulikuwepo toka enzi za zamani. Katika karne ya 20 uvamizi wa nzige ulitokea miaka ya 1926 hadi 1969 na mwaka ‪1986-1989 na karne hii ya 21 sasa tunashuhudia uvamizi huu hasa katika maeneo ya pembe ya Afrika.

Chakula cha nzige

Nzige wamejaliwa taya zenye nguvu sana, zinazomruhusu kukata na kutafuna chakula chochote laini na kigumu kilicho mbele yake. Muundo wa uwazi katika mdomo wake hauruhusu wadudu hao kula nekta ya mimea, bali anaweza tu kutafuna mimea na kwa kweli mimea yoyote inafaa kwa lishe yake.

Nzige hula kwa kutegemea ukuaji wao. Walio wengi hula kwa kiasi na hawasababishi uharibifu mkubwa. Ulaji huo unamruhusu kula zaidi ya nusu kilo ya wiki katika maisha yake yote.

Hata hivyo, nzige wanapokuwa katika makundi, hamu yao ya kula huongezeka kwani wadudu hao hulazimika kula kila wakati chakula kingi ili kuishi. Ikiwa nzige hawazidi kujiongezea chakula, mara nyingi hupoteza uwezo wa kuishi kwa kupata kiu na kukosa protini.

Nzige wakiwa kwenye makundi huharibu mimea yote iliyo karibu nao. Kwa wakati mmoja wadudu hao hula hadi nusu kilo ya majani kwa siku kutegemea na idadi yao. Ikiwa chakula kitakwisha, wadudu hubadilika na kuanza kulana wao kwa wao. Hamu hiyo ya kula hutegemea kiwango cha joto.

Je utawatambuaje nzige wa jangwani na panzi

Ni muhimu mkulima kufahamu tofauti kati nzige na panzi ili kutambua hatari mapema kabla ya kutokea. Nzige wa jangwani huwa na miguu ya nyuma mikubwa kuliko panzi wa kawaida. Miguu yao, huwawewezesha kuruka kwa umbali mrefu kuliko panzi wa kawaida. Hata hivyo unaweza kuwagundua kwa rangi, kwani rangi ya panzi wa kawaida mara nyingi ni kahawia, lakini sifa kubwa ya Nzige ni uwezo wao wa kuwa katika makundi, tabia ambayo haipo kwa panzi, pia uwezo wa kuruka kwa umbali mrefu.

Je, nzige wanaweza kudhibitiwa vipi?

Nzige hushambulia mazao kwa haraka na wakati mwingine hula mimea yote, wakati mwingine huharibu ovyo ovyo. Idadi ndogo ni rahisi kudhibiti, nzige wakubwa wanaohama ni ngumu kudhibiti lakini hatua za kuzuia zinaweza kuchukuliwa kupunguza upotezaji wa chakula.

Ili kukabiliana na mawimbi ya nzige wa jangwani kemikali za oganofosfeti imekua ikitumika kupitia vinyunyuzio vilivyofungwa kwenye magari au kwa kunyunyizia angani. Hata hivyo njia hii sio salama kwa mazingira, viumbe hai na pia binadamu.

Pamoja na kwamba tafiti zinaendelea kufanyika ili kubaini njia salama kudhibiti wadudu hawa bila kuathiri mazingira na viumbe hai wengine. Mkulima unashauriwa kufanya yafuatayo iwapo utaona dalili ya nzige shambani kwako.

  1. Ukiona Panzi shambani na umesikia kuna mlipuko wa nzige katika maeneo mengine. Mkamate na ubaini ni aina gani ya panzi, unaweza kufika kwenye ofisi za kijiji ama kuwasiliana na afisa kilimo katika eneo lako kwa utambuzi.
  2. Iwapo nzige wamevamia bustani au shamba lako basi unashauriwa kuwasumbua kufukuza na kupiga kelele.
  • Nyunyiza unga wa ngano. Unga wa ngano unaweza kusababisha nzige kufa kwa njaa kwa kufanya unga wa ngano kunata kwenye mdomo wao na hivyo kushindwa kutafuna. Nyunyiza kiasi kidogo cha unga wa ngano katika jani la mmea kwani nzige waanza kula unga huo na mwishowe kufa kwa njaa.
  1. Harufu ya kitunguu saumu inaweza kuzuia panzi na wadudu wengine waharibifu. Ili kutengeneza dawa ya vitunguu saumu, chukua balbu za vitunguu saumu mbili, changanya na vikombe 10 vya maji pasha moto hadi mchanganyiko huo uanze kuchemka. Acha Mchanganyiko huo ukae usiku mzima. Asubuhi unachuja na kunyunyizia katika mmea.
  2. Tumia mchanganyiko wa mafuta ya mwarobaini, sabuni na maji. Kama inavyoelezwa hapo chini.

Jinsi mafuta ya mwarobaini yanavyofanya kazi kudhibiti Nzige wa jangwani

Mafuta ya mwarobaini ni kinga ya kikaboni, yenye nguvu ya kuua wadudu kwenye bustani, ni njia pendekezi ya kudhibiti wadudu anuai bila kuathiri udongo na mimea. Mafuta haya hayana athari kwa ndege, mamalia, nyuki na mimea mingine.

Mafuta ya mwarobaini huvunjika haraka na hayaachi mabaki ya kudumu hivyo kuyafanya kuwa kiuatilifu salama na bora kwa mimea. Azadirachtin, moja ya vitu kwenye mafuta ya mwarobaini, ndio inayofanya kazi zaidi na hufanya kazi iliyokusudiwa ya kudhibiti wadudu. Hufanya kazi ya kutibu, kuua na kufukuza wadudu wengi hatari kwa mimea.  Inapunguza uwezo wa mdudu kula mazao. Inaingilia kabisa mfumo wa hormone za wadudu kwa kufanya iwe ngumu kwao kukua na kuzaa.

Mafuta ya mwarobaini yanaweza kutengenezwa kua chembechembe, unga au mkusanyiko wa kioevu. Inahitaji kuchanganywa na maji kabla ya kunyunyizia kwenye mmea. Kwakua mafuta na maji hayachanganyiki kwa urahisi, hivyo utaongeza sabuni ya kuua wadudu kwani itasaidia kutengeneza mchanganyiko mzuri kisha pulizia kwenye mmea.

Mafuta ya mwarobaini

  1. Mimina vijiko 2 (vya chai) vya mafuta ya mwarobaini kwenye bafta ya kunyunyizia
  2. Miminia gallon moja ya maji.
  3. Ongezea matone 7 hadi 10 ya sabuni ya kuoshea. Sabuni inasaidia mafuta kushikamana na mmea.
  4. Changanya mchanganyiko huo kwa kutumia kijiko cha kuchanganyia. Ikiwa dawa yako inazaidi ya lita 4, unaweza kuongezea kichocheo; uwiano wa vijiko 2 (vya chai) vya mafuta ya mwarobaini na kwa lita moja na maji ibaki hivyo.
  5. Shinikiza hewa kwenye kinyunyizo kwa kupampu kutumia kishikizo mara kadhaa.
  6. Nyunyizia eneo lako muda wa asubuhi, wakati nzige wakiwa ardhini
  7. Rudia kufanya hivi kila asubuhi mpaka nzige wote watoweke.

Kwa maelezo zaidi wasiliana na Juma Mwinyimkuu,Kituo cha Afya ya Mimea Kanda ya Kaskazini,Arush  kwa simu namba 0782689198 barua pepe:allymmm@yahoo.com

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *