Mboji ni sehemu ya viumbe (mabaki ya mimea na wanyama) ambayo imeozeshwa kwa muda mrefu ili kusazwa na viumbe vidogo vidogo. Sehemu za vitu kama majani, matunda na mabaki ya mboga hutengeneza mbolea ya mboji.
Vipande vya vitu au sehemu za viumbe mara nyingi huwa vimejazwa nyumbani au shambani bila mpangilio wowote. Hivi vinaweza kutumika kutengenezea mboji lakini itachukua muda mrefu kabla ya kuoza, na hivyo rutuba yake kupotea.
Ikiwa muda utatengwa kuandaa mbolea matokeo yatakuwa mazuri na ya kufaa. Mabaki kutoka shambani na jikoni yanatumika katika kutengenezea mboji.
Kumbuka: Mboji iliyotunzwa vyema huwa na rutuba nzuri kwa mimea inapotumiwa shambani. Mboji huchemka hata kiasi cha kuua magonjwa ya mimea na mbegu za magugu.
Namna ya kutengeneza mboji
Ili kutengeneza mboji, kusanya vitu na vifaa vinavyohitajika katika utengenezaji wa mboji ambayo ni;
- Majani mengi mabichi/kijani na makavu. Majani jamii ya mikunde ni mazuri sana kwani hutengeneza kirutubishi cha naitrojeni kwa wingi.
- Mabua ya mahindi au vitawi vya miti.
- Udongo wa kawaida wa juu.
- Samadi, mbolea yoyote ya wanyama au mboji ya zamani .
- Majivu au vumbi la mkaa.
- Maji
Vifaa visivyofaa kuwekwa kwenye mboji
- Sehemu za mimea ambazo zimenyunyiziwa dawa ya kuwaua wadudu (viuatilifu)
- Vipande vya nyama kwa sababu vinavutia panya na wadudu wengine.
Hatua za utengenezaji
- Chagua sehemu karibu na eneo ambalo mboji itaenda kutumika na ambapo kuna hifadhi ya kutosha kukinga dhidi ya upepo, jua na mvua.
- Katakata majani yawe madogo madogo ili yaweze kuoza haraka. Tengeneza msingi kama mita sita (6) urefu na upana wake mita 2 kwa kutumia majani magumu kama matawi/vijiti. Hii itahakikisha maji yanatiririka na hewa ina zunguka vizuri. Hakikisha kuna nafasi ya kutosha kufanyia kazi kwenye biwi bila kulikanyaga.
- Weka sentimita 10 ya majani ambayo hayaozi haraka kwa mfano mabua vya mahindi au mimea mibichi/kijani.
- Weka sentimita 10 ya vifaa ambavyo huoza haraka kwa mfano maganda ya mboga na matunda.
- Weka sentimita 2 ya samadi(mbolea hai ya wanyama), mabaki ya mbolea ya zamani kama yaweza kupatikana.
- Weka udongo wa juu sentimita 10 kutoka kwenye shamba ambalo hulimwa.
- Majivu na mkojo vyaweza kunyunyuziwa juu ili kufanya biwi/lundo kuoza haraka.
- Nyunyizia maji kwenye biwi mpaka lilowe.
- Rudia mpangilio huu kuanzia namba nne (4) mpaka lundo lifike mita moja (1.m) hadi moja na nusu (1.5m) kwenda juu isipokuwa vijiti/matawi ya kwanza.
Zingatia
- Biwi/lundo cha mboji linatakiwa lifunukwe ili kupunguza/kuzuia mvuke ama mvua nyingi ambayo hubeba rutuba kutoka kwenye mbolea. Weka gunia, nyasi ama matawi ya ndizi yaliyokauka.
- Kila tabaka/kunjo/safu yafaa kupangwa kuanzia kwenye ukingo ili lundo la mbolea lisiporomoke.
- Namna nyigine ya kuzuia lundo kuporomoka ni kwa kuweka vipande vya mbao kando ya biwi. Wavu wa nyuzi za chuma utafanya biwi kukauka.
- Katika sehemu zenye ukavu mwingi. Mianzi iliyo na mashimo husaidia kufanya hewa kuingia na kuzunguka kwa urahisi.
Mboji iliyoiva hubadilika rangi na kuwa ya hudhurungi, tifutifu na hunukia vizuri.
Muhimu
Samadi kutoka kwa mifugo na mabaki ya mimea ni nzuri sana katika kutengeneza mbolea ya mboji.