- Kilimo

Ujue mmea wa mnazi pamoja na kanuni za kilimo bora cha zao hili

Sambaza chapisho hili

Minazi ni zao la biashara nchini Tanzania ambalo hulimwa na kustawi zaidi ukanda wa pwani ya Tanzania. Mikoa kama Lindi, Mtwara, Pwani, Dar es salaam, Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba, pia kwa uchache Minazi hulimwa kwenye mikoa ya Mbeya, Kigoma na Tabora.

Aina za minazi

Kuna aina kuu tatu za Minazi inayolimwa hapa Tanzania nayo ni (i) Minazi Mirefu ya asili (East African Tall) (ii) Minazi mifupi ya Kipemba (Malaysian Yellow Dwarf) (iii) Minazi Chotara (hybrid) inayotokana na kuunganisha chavua za Minazi mirefu na minazi mifupi ya Kipemba.

Upandaji

Ilikupata mazao yaliyo bora na mengi ni vema kuzingatia yafuatayo;

  • Kuchagua mbegu nzuri na kubwa kwa umbile yenye kuzaa sana.
  • Chagua eneo zuri la kupanda, eneo lenye udongo wa kichanga, pasipo na mwinuko na pasiwe na mwamba karibu wala udongo wa mfinyanzi.
  • Kupanda mapema kwa kuzingatia kalenda ya mvua kwa msimu, panda kwenye kipindi cha mvua za kwanza.

Kuandaa shamba

Ondoa visiki kwenye shamba jipya kwa kuving’oa na kuvirundika pembezoni mwa shamba.

  • Tibua shamba lote, pima shamba kwa ajili ya kuchimba mashimo.
  • Chimba mashimo kwa umbali wa mita 9 kwa mita 9 kwa minazi Mirefu na mita 7 kwa 7 kwa Minazi mifupi na chotara.
  • Andaa mashimo yenye kipimo cha sentimita 60 kwa 60.
  • Changanya udongo wa juu na samadi au mboji kisha rudishia shimoni. (Zingatia kuwa mbolea ya samadi ya ng’ombe isiyopoa si mzuri kwenye mashimo ya kupanda minazi kwani huvutia mazaliano ya mchwa).
  • Panda miche ya Minazi iliyooteshwa kitaluni kwako au kununua kwa mawakala au wakulima wanaootesha miche, chagua miche yenye umri wa kutosha yaani majani 5 na hii maana yeke mnazi utakuwa tayari una umri wa miezi 5, inaaminiwa kuwa mnazi unatoa majani (kuti moja) kila mwezi.

Palizi

Palizi kwenye zao la Minazi ni kitu muhimu sana cha kuzingatia. Palilia kwa kulima visahani kwa kipenyo cha mita 1 hadi 2 kutegemeana na umri wa mche/mti.

Palizi inasaidia mmea kutopata mashambulizi ya baadhi ya wadudu kama vile mchwa. Majani yakikauka ni kivutio kikubwa cha moto wa msituni, Mnazi mkubwa ukiungua moja ya madhara yake ni kukosekana na mavuno kwa mwaka husika. Mnazi ulioungua moto huchukua takribani mwaka mmoja ili kuanza kuzaa tena.

Uwekaji wa matandazo (mulch) kwenye Minazi kwa kutumia majani au nyasi kavu ni hatari kwa mashambulizi ya mchwa na pia ni mazalia ya wadudu Chonga wa Minazi.

Mazao mchanganyiko

Ili kupunguza gharama za palizi kwenye shamba la minazi inashauriwa kuwa ni vema apande mazao mchanganyiko jamii ya mikunde kama vile Kunde, Karanga, Njugu, Upupu na pia waweza kupanda Mahindi au Alizeti kwa miaka minne (4) ya mwanzo.

Mavuno

Minazi mirefu huanza kutoa mavuno mwaka wa 5 na 6 ambapo Minazi Mifupi na ile Chotara hutoa mavuno kuanzia mwaka wa 4 na 5. Kwa wastani Mnazi uliotunzwa vizuri hutoa Nazi kati ya 25 hadi 40 kwa mavuno ya mara moja na unatakiwa kuvuna baada  ya miezi Minne.

Kudhibiti wadudu na magonjwa

  • Magonjwa

Minazi haina magonjwa mengi ya kusumbua mmea, bali ugonjwa pekee wenye kuuwa Minazi ni ugonjwa wa Nyong’onyea, ambao kitaalamu hujulikana kama leathal disease. Ugonjwa huu ni wa hatari sana na hauna tiba, ugonjwa wa Nyong’onyea hushambulia minazi mikubwa kwa kuozesha sehemu ya mcha au kilele cha Mnazi na na kufa kabisa.

Dalili zake ni majani kuwa njano ikianza na majani machanga kisha kuenea majani yote, kubadilika rangi majani kutoka njano na kuwa kahawia na kisha kukauka na kudondosha chini sehemu ya juu, wakati huo mnazi unakuwa tayari umeshaathirika na kufa.

Ugonjwa huu ni wa kuambukiza kutoka Mnazi mmoja hadi mwingine kwa njia ya hewa, wadudu na wanyama, hakuna dawa iliyogundulika kudhibiti ugonjwa huo na njia mzuri ya kukinga ni usafi wa shamba na kuondoa kwa kuikata na kuichoma moto minazi yote itakayoonyesha dalili ya kuugua.

 Alama kubwa ya maeneo yaliyoshambuliwa na ugonjwa huo ni kuonekana kwa miti mingi ya minazi iliyokufa na kubaki kama nguzo za umeme au simu, baadhi ya maeneo ya vijiji vya wilaya ya Kilwa na Mafia unaweza kuona hali hiyo.

Wadudu waharibifu

  • Mchwa; Mchwa ni miongoni mwa wadudu waharibifu kwenye zao la Nazi. Mchwa huanza kushambulia nazi zikiwa kitaluni kwa kutafuna magubi ya nazi au ngozi ya nje na kuuwa mche, tumia dawa za kudhibiti mchwa na pia majivu yanasaidia sana. Mchwa pia hushambulia miche iliyopandwa shambani na kuweza kuua kabisa, mche mkubwa kuanzia miaka 4 haidhuriki na mdudu huyu.
  • Mdudu Faru wa minazi; Mdudu huyu ni mkubwa saizi ya kidole gumba cha mtu mzima, ana rangi ya kahawia au wekundu uliofifia, ana meno makali ya kutafuna majani ya mnazi pia umbile lake ni kuwa ana pembe iliyopinda kwa juu sawa na pembe ya mnyama Faru na kitaalamu anajulikana kama Rhinoceros beetle.
Mdudu Faru wa minazi (Rhinoceros beetle).

Mdudu huyu huzaliana kwenye mabiwi yaliyopo shambani, au kwenye miti na magogo yaliyokauka na yenye dalili ya kuoza.

Mdudu huyu hutaga mayai humo na mayai yakishaanguliwa wadudu wakubwa huruka na kutua kwenye minazi kwa ajili ya kupata chakula ambapo hushambulia kilele cha mche wa mnazi, hukitafuna na hatimaye mnazi waweza kufa kabisa.

Minazi ya umri wa kati waweza kuona dalili ambapo kuna lapu lapu za mnazi nchani zikiwa zimetolewa nje ya mti na makuti yakaliwa yatakuonesha alama ya mkato kama vile yamekatwa kwa mkasi. Wadudu hawa wana tabia ya kuruka nyakati za usiku kwa ajili ya kuzaliana (mating) na kuhama mnazi  mmoja hadi mwingine.

Kwa maelekezo Zaidi, wasiliana na; Issaya Jackson Mtambo, Mratibu, Shirika la Uwezeshaji wa Maendeleo ya Jamii (SOCEI) P.O.BOX 106 Masasi. Simu namba +255(0)786 651 106 // 0717 236 800 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

8 maoni juu ya “Ujue mmea wa mnazi pamoja na kanuni za kilimo bora cha zao hili

  1. Machapisho katika ukurasa huu Yana msaada mkubwa Sana haswa haswa kwa mtu ambae Hana uelewa kabisa juu ya Aina fulan ya kilimo. Hivyo ninashauri “mahesabu ya mavuno pamoja na Bei za masoko ziwekwe wazi pamoja na uwanda wa soko la zao husika uwekwe wazi, ili kuvutia wawekezaji wa ndan na nje pamoja na kuendeleza shughuli za kilimo biashara na uzalishaji wa ajira zaidi ” . Asante

    1. Habari Bw. Fikiri

      Tunashukuru sana kwa mawazo mazuri lakini pia kwa kuendelea kufuatilia na kusoma makala mbalimbali za Mkulima Mbunifu. Tumelipokea wazo lako na tutalifanyia kazi.

      Karibu sana Mkulima Mbunifu

      1. Ahsante kwa elimu ya kilimo Cha minazi, naomba kufahamu hakuna mnazi ambayo huchukua muda mfupi Kama miaka 2 au 3 tangu kupanda Hadi kuvuna?

        1. Habari,

          Karibu Mkulima Mbunifu na asante kwa kuendelea kufuatilia na kusoma makala mbalimbali za jarida hili
          Kuhusu minazi ya muda mfupi, ngoja tulifanyie kazi tutakujibu mara baada ya kupata jibu sahihi.

          Karibu

    1. Asante kwa elimu ya kilimo cha nazi, naomba kujua nazi yenye sifa zipi inaweza kuoteshwa? (Kufanywa mbegu) na namna ya kuiandaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *