- Kilimo

Ni muhimu kuelewa magonjwa ya mimea

Sambaza chapisho hili

Tafsiri rahisi ya magonjwa ya mimea ni hii: Ni kuwepo kizuizi, au usumbufu fulani unaosababishwa na magonjwa au viumbe fulani kusababisha vichocheo vya ukuaji wa mimea kutokufanya kazi katika hali yake ya kawaida. Kutokana na sehemu ya mmea kupata usumbufu huo, seli za mmea zinaweza kufa au hata kusababisha mmea kufa kabisa. Jambo hili kwa kawaida husababisha kuathirika kwa kiwango cha mavuno, au kuwa na mavuno yasiyokuwa na ubora.

Magonjwa ya mimea yanaweza kugawanywa katika makundi mawili

  1. Magonjwa yanayosababishwa na vimelea vya nje, au yanayosababishwa na vimelea wengine kama vile fangasi, bakteria, virusi na minyoo inayoshambulia mimea.
  2. Magonjwa yasiyosababishwa na vimelea (yasiyotokana na maambukizi). Dalili zake hutokana na sababu mbalimbali, hii ni pamoja na madhara yanayotokana na madini, kutokuwepo na uwiano wa virutubisho, kukosea wakati wa kuvuna na kuhifadhi, vichocheo vinavyotokana na mazingira, kwa mfano, uchafuzi wa mazingira na madhara yanayotokana na dawa za kuulia magugu.

Magonjwa na udhibiti wake

Magonjwa yote yanayosababishwa na vimelea ni matokeo ya mwingiliano wao na mimea husika, vimelea na sababu nyingine za kimazingira kama vile mwanga, joto, na unyevu. Mwingiliano huu hujulikana kama mzunguko wa magonjwa wa pembe tatu. Endapo sehemu moja wapo katika mzunguko huu itakosekana, basi ugonjwa hautakuwepo.

Mzunguko wa magonjwa

Kimsingi mlipuko wa magonjwa unategemea sababu tatu;

  1. Kiwango cha wadudu wanaosababisha magonjwa wanaokuwepo
  2. Ugonjwa unaweza kuenea kwa kiwango gani
  3. Muda ugonjwa unaoweza kujitengeneza na kuenea

Kwa kawaida kukua na kuwepo kwa mlipuko hutegemea njia zinazofahamika. Katika hatua za mwanzo ueneaji huwa ni wa taratibu. Wakati huo kunakuwepo na kinga hivyo maambukizi yanakuwa ni kidogo. Maambukizi yanapokuwa yameshika kasi, madhara mengine kama vile kutu hutokea mara moja na kuongezeka kwa haraka. Baadaye maambukizi hupungua inapokuwa hakuna tena mmea wa kuunezea ugonjwa, (hapa mimea yote inakuwa na ugonjwa), au kama mazingira hayatatoa ushirikiano kwa ugonjwa husika kuendelea kuenea, au kama msimu wa zao husika utafikia mwisho.

Udhibiti wa magonjwa

Mbinu za udhibiti wa magonjwa, inabidi zilenge yote ambayo yamezungumziwa hapo juu, kuongeza uwezekano wa mimea husika kukua vizuri, kupunguza kiwango cha madhara, kupunguza kasi ya ukuaji na usambaaji wa ugonjwa, kupunguza muda wa uwepo wa maambukizi jambo linaloweza kuchochea ugonjwa.

Kuweka karantini, au kutumia mbegu ambazo hazina maambukizi, au zilizo idhinishwa, itasaidia kuzuia uwepo wa magonjwa.

Mzunguko wa mazao ni moja wapo ya njia nzuri sana za udhibiti wa magonjwa, hii ni kwa sababu aina flani ya wadudu hushambulia na kuathiri aina moja tu ya mazao. Usafi wa mazingira hutegemeana na shughuli za kitaalamu za kilimo zinazolenga kutokomeza au kupunguza vichocheo vya maambukizi kwenye mimea au kwenye shamba. Hii inajumuisha kuondoa na kuharibu mabaki yote ya mavuno ambayo wadudu wanaweza kuishi pamoja na magugu yanayoweza kuwa wenyeji wa wadudu hao.

Uwezo wa mazao kukabiliana na magonjwa unasaidia sana kutokuenea kwa ugonjwa, au muundo wa maambukizi ya ugonjwa hauwezi kuendelea. Sehemu ambayo vichocheo vya maambukizi ni kidogo, huwa madhara ni kidogo na huchukua muda mrefu zaidi kuweza kufikia kiwango cha juu. Katika hali kama hii, uharibifu unatokana na magonjwa unaweza kuepukwa, kwa kuwa mimea inakuwa imefikia sehemu ambayo magonjwa hayawezi tena kuidhuru au kusababisha hasara.

Magonjwa pia yanaweza kupunguzwa au kudhibitiwa kwa kupanda aina ya mazao yenye uwezo wa kukabiliana na magonjwa au yanayovumilia magonjwa, na hali kadhalika kutumia dawa zinazoweza kusaidia kutokomeza wadudu na magonjwa. Kwenye eneo ambalo kuna kiwango kikubwa cha vichocheo vya magonjwa, kupanda aina ya mazao yanayovumilia magonjwa na kutumia dawa za ukungu itasaidia zaidi kupunguza kiwango cha ugonjwa.

Unaweza kubadilisha muda wa kupanda aina fulani ya mazao, ili kukwepa kipindi ambacho huwa na kiwango kikubwa cha mlipuko wa aina fulani ya magonjwa.

Mzunguko wa mazao na kupanda mseto ili kupunguza wadudu hatari

Endapo umepanga kupanda aina fulani ya mazao mara kwa mara, utalazimika kufanya kwa mzunguko. Aina tofauti ya mimea huhitaji kiasi na aina tofauti za virutubisho kutoka ardhini, halikadhalika kiwango cha matumizi hutofautina. Wakati huo huo aina fulani ya mimea huwavutia aina tofauti ya wadudu na magonjwa ambayo baada ya muda fulani hujijenga katika eneo hilo.

Endapo utapanda aina fulani ya zao katika eneo moja mfululizo, aina ya virutubisho ambavyo hutumiwa na zao hilo huisha haraka na hatimae udongo kuchoka na kusababisha mimea kuwa dhaifu, hivyo kutoa urahisi kwa wadudu waliokuwa wanasubiria kuishambulia kupata urahisi. Mzunguko wa mazao ni muhimu kwa kama utasaidia kupunguza madhara. Ni lazima mzunguko wa mazao ufanywe kwa uangalifu, kwa kuwa kuna aina ya wadudu wanaoweza kuishi kwenye mabaki ya mazao yaliyo oza na ambayo hayajaoza.

Baadhi ya mazao kama vile mtama na mahindi yanaweza kupunguza kiasi cha magugu na virutubisho vyake. Ni muhimu kuangalia ni aina ipi ya mzunguko wa mazao ambao umekuwa na ufanisi katika ukanda wa kilimo, katika kuongeza uzalishaji na kusaidia kudhibiti wadudu na magonjwa.

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *