- Kilimo

Mkulima avumbua dawa ya asili ya kutibu ugonjwa wa mnyauko

Sambaza chapisho hili

Uzalishaji wa mbogamboga umekuwa maarufu nchini, hasa kutokana na uhitaji wake wa kila siku. Hii ni kutokana na jamii kupata uelewa juu ya umuhimu wa ulaji wa mbogambga kwa afya ya mwili.

Aidha, upatikanaji wa soko ndani na nje ya nchi pamoja na uzalishaji kuwa rahisi, umepelekea wakulima wengi kujikita katika kilimo hiki.

Hata hivyo, kilimo hiki kimekua na changamoto ya magonjwa mbalimbali. Wakulima wa kilimo hai, hujikita kutumia malighafi asili kutengeneza dawa mbalimbali zinazosaidia kutibu magonjwa ya mimea. Vile vile kutengeneza virutubishi vinavyosaidia ukuaji wa mimea yenye afya.

Ugonjwa wa mnyauko umekuwa ukiwasumbua wakulima wa mbo-gamboga, na kusababisha we-ngine kukata tamaa kabisa na hata kuamua kuacha kilimo hiki. Wengine wamejitahidi kutafuta suluhisho la ugonjwa huu kwa kutumia malighafi asili.

Bi. Neema Mwendo [56], mkulima mjasiriamali na mkazi wa Shirinjoro Mkoani Kilimanjaro ameweza kugundua dawa ya asili ya kupambana na ugonjwa wa mnyauko. Dawa hiyo pia imetumika kama mbolea ya asili. Dawa hii ameweza kutumia kwenye shamba lake la mbogamboga na kupata mafanikio mazuri.

Bi. Mwendo anasema kuwa ‘’Mimi ni msindikaji wa mlonge na mara nyingi nilipokuwa nikiandaa bidhaa zangu, ule uchafu uliosalia nilichukua na kuweka chini ya mti jambo ambalo baadaye niligundua kuwa eneo lile la mti lenye uchafu wa mlonge majani yalikuwa yakiota kwa wingi’’.

Aliongeza kuwa, mara baada ya kuona hivyo aliamua kuanza kutumia kuweka kwenye mimea shambani na aliweza kuona matokeo mazuri na kugundua kuwa mlonge ni mbolea nzuri kwa ajili ya shamba.

Bi. Mwendo aliongeza kuwa, baadaye kwenye eneo lilelile la mti alilokuwa akimwaga mabaki ya mlonge na mkojo wa ngombe kama uchafu lakini cha ajabu ni kuwa majani yaliongezeka kasi ya kuota na yalikuwa yenye afya sana.

Baada ya hapo ndipo akaamua kuanza kutengeneza mchanganyiko wa unga wa mlonge pamoja na mkojo wa ng’ombe kwa ajili ya kurutubisha mimea kama mbolea lakini cha ajabu aligundua kuwa ugonjwa wa mnyauko uliokuwa ukishambulia mimea yake haukuwepo tena hivyo akagundua hiyo ni dawa kwa ajili ya ugonjwa huo.

Namna ya kutengeneza dawa ya asili ya kuua mnyauko

Mahitaji

Ili kutengeneza dawa hii ya asili ambayo pia ni mbolea hai kwa ajili ya mimea, unahitajika kuwa na unga wa mlonge, majivu na mkojo wa mifugo.

Namna ya kutengeneza

  • Chukua majani ya mlonge kisha anika juani mpaka yakauke
  • Mara baada ya kukauka, twanga ili kupata unga unga
  • Pima unga wa mlonge kiasi cha lita 20
  • Changanya na majivu kiasi cha sado moja yaani kilo 4
  • Weka mkojo wa mifugo kiasi cha lita 5
  • Changanya vizuri kuhakikisha malighafi zote zimechanganyika kisha peleka moja kwa moja shambani.
  • Weka katika kila mmea kwa kuuzungushia kidogo kidogo

Kutengeneza busta ya asili

Busta hii hutumika kupiga kwenye mimea ya mbogamboga na husaidia kuongeza uzalishaji.

Malighafi zinazohitajika ni pamoja na;

  • Unga wa mlonge kilogramu 5
  • Majivu kilogramu 4
  • Mkojo wa mifugo lita 5
  • Maji lita 60
  • Changanya malighafi yote katika chombo kimoja kisha weka kwenye pampu na nyunyizia mboga zako.

Kwa maelezo zaidi wasiliana na Bi. Neema Mwendo kwa simu namba 0752 630001

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *