- Kilimo

Fursa ya kibiashara kutokana na zao la alizeti

Sambaza chapisho hili

Alizeti ni zao maarufu katika maeneo yenye mvua za wastani mfano Mkoa wa Singida, Dodoma, Manyara na Simiyu. Zao hili limekuwa maarufu sana kutokana na mafuta yake kupendwa na watu wengi kwa sababu hayachanganywi na kemikali yoyote.

Katika miaka hii miwili, Mafuta ya alizeti yameonekana kupanda bei kutoka fedha za kitanzania shilingi 3000/= kwa lita hadi 5500/= huku dumu la lita 20 likipanda bei hadi kufikia Tsh. 100,000/=.

Hii ni kutokana na ukosefu wa mvua za kutosha zinazohitajika kustawisha zao hili lakini pia ni fursa katika kilimo, ambapo wakulima wanatakiwa kuangalia uhitaji sokoni.

Mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa uzalishaji

  • Andaa shamba kwa kuzingatia kanuni
  • Chagua aina bora ya mbegu inayovumilia magonjwa, wadudu na inayotoa mazao bora ili kupata mafuta mengi

Jinsi ya kupanda alizeti

Mkulima anashauriwa kuzingatia vipimo yaani sentimita 45 shimo hadi shimo kwa mbegu moja moja na sentimita 60 kwa mbegu mbilimbili inategemea hali ya mbegu lakini pia nafasi katika ya mstari mmoja hadi mwingine ni sentimita 60 hadi 75.

Kuweka mbolea

Rutubisha udongo kwa kutumia mbolea za mboji na samadi ili kupata mazao mengi na bora.

Palizi

Alizeti kitaalamu inapalizi mbili palizi ya kwanza ni pale alizeti ilipoota na palizi ya pili ni baada ya wiki 6 hadi 8 inategemea na hali ya mvua na shamba.

Kupunguza miche

Mkulima anashauriwa kupunguza miche baada ya palizi kuepusha kuikata na kubaki na miche inayotakiwa.

Kudhibiti wadudu na magonjwa

Alizeti hushambuliwa na magonjwa ya majani, mizizi na masuke ambayo husababisha upungufu wa mavuno. Hivyo ni muhimu kuyadhibiti ili kupata mavuno mengi na bora. Pia ndege hupunguza mavuno kwa kiasi cha asilimia 50 au zaidi. Njia ya kudhibiti ndege ni kwa kuwafukuza na kupanda mbegu zinazokomaa mapema.

Maandalizi kabla ya kuvuna

Kagua shamba kuona kama alizeti imekomaa na alizeti hukomaa katika kipindi cha miezi mitatu kwa wastani au kupandwa wakati huo punje huwa na unyevu wa asilimia 25 ni muhimu kuvuna alizeti mapema ili kuepusha mashambulizi ya panya, mchwa na ndege waharibifu’’

Dalili ya alizeti iliyokomaa

Suke hubadilika rangi kutoka manjano na kuelekea kuwa nyeusi.

Maua vya pembeni mwa suke hunyauka na hubadilika rangi kutoka rangi ya manjano na kuwa ya kahawia

Uvunaji, ukusanyaji na ubebaji

Ukipata shamba zuri ekari moja ya alizeti huweza kukupatia kati ya magunia5-10 kutegemeana na aina ya mbegu uliyotumia na pia namna shamba lako ulivyolihudumia.

Uvunaji

Masuke ya alizeti huwekwa kwenye vikapu ambavyo hutumika kusomba alizeti ndani ya shamba kisha alizeti hufungwa kwenye magunia na kusafirishwa hadi nyumbani tayari kwa kukausha.

Kukausha

Kuna hatua mbili za kukausha alizeti kukausha masuke na kukausha mbegu za alizeti

  • Kukausha masuke: masuke hutandazwa kwenye kichanja bora katika kina kisichozidi sentimita 30 ili yaweze kukauka vizuri. Vilevile huweza kutandazwa kwenye maturubai, mikeka au sakafu. Lengo la hatua hii ni kukausha masuke ya alizeti ili kurahisisha upuraji

Upuraji

Upuraji hufanywa baada ya kuhakikisha kuwa masuke ya alizeti yamekauka vizuri, masuke ya alizeti hupurwa kwa kutumia mikono ambapo mbegu hutenganishwa kwa kupiga masuke taratibu kutumia mti ni muhimu kupiga masuke taratibu ili kuepusha kupasua mbegu. Pura kwenye kichanja bora, mikeka au maturubai

Ukaushaji mbegu

Mbegu za alizeti hukaushwa juani kwa kutandazwa kwenye vichanja bora maturubai, mikeka au akafu safi. Tandaza mbegu katika kina kisichozidi sentimita 4 ili ziweze kukauka vizuri.

Lengo la hatua hii ni kukausha mbegu baada ya kupurura ili kufikia kiwango cha unyevu kinachotakiwa kwa hifadhi salama ambacho ni asilimia 8.

Kupepeta na kupembua

Hatua hii hufanyika ili kuondoa takataka kama vile mawe, mapepe na mbegu zilizooza au kupasuka wakati wa kupura hupepetwa kw kutumia nyungo au mashine zinazoendeshwa kwa mikono au injini

Kuhifadhi

Alizeti iliyopurwa huhifadhiwa katika vihenge, na kwenye magunia. Magunia yapangwe kwenye chaga kwa kupishanisha. Ili kurahisisha kazi ya kukagua ghala, acha nafasi ya mita moja kutoka kwenye ukuta ziba sehemu zote za ghala ili kuzuia panya kuingia.

Panya hupenda sana kutafuna punje za alizeti hivyo husababisha upungufu mkubwa wa punje ambao husababisha upotevu wa asilimia 30 kwa kipindi cha miezi 3 ya hifadhi asilimia ya upotevu inaweza kuwa kubwa.

Kwa mawasiliano zaidi wasiliana na Hamisi Samade kwa namba 0756712003 Itigi Singida au Mkulima mbunifu (MKM) kwa simu namba 0717266007 Arusha Tanzania.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *