- Kilimo

Kuanzisha biashara kunahitaji mipango thabiti

Sambaza chapisho hili

Miaka ya hivi karibuni serikali pamoja na wadau wengine wamekuwa na mikakati thabiti ya kuendeleza kilimo na kuwashawishi wakulima kuweka shughuli zao katika mtazamo wa kibiashara.

Waliochukua na kuufanyia kazi ushauri huo kisha kufanya shughuli zao za kilimo kitaalamu kwa mtazamo wa kibiashara leo wanapata faida kubwa. Wana pesa inayoingia mifukoni mwao na kuziba mapengo yote yaliyokuwa yametokea kabla na kupoteza pesa nyingi.

Faida hiyo haiji kirahisi. Kuwa na wazo ni aina gani ya kilimo unayoweza kuifanya kibiashara pekee haitoshi. Huo ni mwanzo tu. Ni lazima kukusanya au uwe na pesa kwa ajili ya kugharamia shughuli hiyo, na mwisho utakapouza bidhaa zako au huduma utakayotoa uweze kupata pesa zaidi. Hapo ndipo wazo la biashara linatekelezeka.

Mpango wa biashara ni nini?

Unapoomba mkopo, ambapo kwa kawaida au mara nyingi mkopeshaji ni benki na taasisi nyinginezo za fedha, utaulizwa mpango wa biashara yako unayokopea fedha hizo. Mpango wa biashara unatoa tafsiri ya malengo yako katika mageuzi ya kibiashara.

Kwa nini unafikiri malengo hayo yatafikiwa, na nini mikakati ya kuyafikia malengo hayo? Kwa bahati mbaya wakulima wengi hawajaelimika katika kufanya shughuli zao za kilimo kibiashara na kuwa na mpango wa biashara. Bila kuwa na mpango wa biashara ni vigumu sana kuweza kumshawishi mtu au taasisi ya fedha kuwekeza katika mradi wako.

Mpango wa biashara hubadilika kulingana na ukubwa wa biashara unayolenga, utaalam utakaotumika, na ni nani walengwa katika mradi huo. Kwa ujumla mpango wa biashara unakuwa na mambo yafuatayo:

Muhtasari

Lengo la sehemu hii ni kutoa mtazamo mzima wa biashara husika na ushirika huo, unaelezea kwa ufupi biashara husika, bidhaa au huduma zitakazojumuishwa, uchambuzi wa soko la bidhaa/huduma hizo kwa ufupi, mikakati ya kupata soko, na pia uchambuzi kwa ufupi ni jinsi gani fedha hizo zitasimamiwa kuahakikisha zinafanya shughuli lengwa.

Sehemu hii ni lazima iwe wazi na ya kueleweka ili kutoa mtizamo mzuri wa biashara unayokusudia. Ni lazima uwe wazi kabisa kuelezea lengo la fedha unazokopa/omba. Muhtasari unaotoa ni lazima kuelezea kwa uhakika kuwa biashara yako itafanikiwa.

Muda mzuri wa kuandika muhtasari ni baada ya kuandika mchanganuo wa biashara na kisha uunganishe mwanzoni mwa mpango wako wa biashara.

Wazo la biashara: Hili hutoa taarifa juu ya bidhaa utakazouza au huduma utakayotoa.

Mpango wa Soko: Hii inajumuisha mambo yote unayofanya kutafuta wateja, kufahamu ni nani watakuwa wateja wako, ni nini wanachohitaji, na namna ya kuwafikia. Sehemu hii itaelezea bidhaa na huduma zako kwa undani.

Itaelezea pia bei za bidhaa au huduma zako, na ni wapi biashara ama ofisi yako itakapokuwa na mbinu utakazotumia kusambaza bidhaa zako na ni jinsi gani utakavyoitangaza biashara yako.

Mfumo wa biashara: Hii inaelezea mfumo wa biashara yako kisheria, mfumo uliochagua unategemeana na faida na hasara ambazo kila sheria inazo. Uchaguzi huu unaweza kuwa wa mtu binafsi, ushirika au kampuni isiyokuwa na kikomo, au ujamaa.

Katika sehemu hii pia unatakiwa uoneshe ni kwa jinsi gani ulivyofikiria mahitaji ya kisheria na ni kwa jinsi gani umeweza kufuata katika utaratibu mzima wa kuanzisha biashara yako.

Usimamizi: Sehemu hii inajibu maswali juu ya kiwango cha taaluma na uzoefu wa wafanyakazi wako, utahitaji wafanyakazi wangapi, na ni kwa namna gani elimu na uzoefu wao utakavyosaidia katika kufanikisha kufikia malengo uliyojiwekea katika biashara yako.

Mipango ya fedha: Unahitaji kuwa na bajeti kwa ajili ya biashara yako. Kwa hiyo sehemu hii itasaidia kuweza kupangilia faida na mtiririko mzima wa fedha katika biashara yako mpya. Hii ina maana ya fedha zinazoingia (mapato) na zinazotoka (matumizi).

Ukishatengeza bajeti ni rahisi kutumia taarifa hiyo kufanya hesabu ya fedha unazohitaji kwa ajili ya kuanzisha biashara yako. Huu unaitwa mtaji, na unatakiwa kuonesha chanzo cha upatikanaji wa mtaji huo. Hii ina maana ya kuonesha ni chanzo kipi kitakachochangia asilimia flani katika fedha hizo zitakazo anzisha biashara yako.

Angalizo

  • Mpango wa biashara ni mwongozo. Kuwa na mpango wa biashara ulio makini na unaokubalika unaweza kusaidia sana kufanikiwa.
  • Kuandika mpango mzuri wa biashara hakukuhakikishii kufanikiwa lakini ni njia moja wapo ya kupunguza uwezekano wa kuanguka kibiashara.
  • Kujaribu huleta mafanikio. Anza kuandika leo na upate uzoefu utakaokuletea mafanikio.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *