- Kilimo

Kitunguu swaumu kinafaa kufukuza wadudu

Sambaza chapisho hili

Hii ni njia nyingine bora na salama, ambayo mkulima anaweza kutumia kwa ajili ya kufukuza wadudu shambani, bila kusababisha madhara ya yoyote.

Lengo la kuandaa mchanganyiko huu wa Kitunguu swaumu ni kuwafukuza wadudu wasishambulie mimea shambani. Matumizi ya kitunguu swaumu husaidia kupunguza wadudu shambani  na kupunguza matumizi ya kemikali za sumu hivyo kusaidia kulinda afya ya walaji pamoja na kuhifadhi mazingira.

Kuna aina mbalimbali za wadudu wanaoweza kufukuzwa kwa kutumia kitunguu swaumu. Wadudu hao ni pamoja na: Kimamba, inzi weupe, vidukari, panzi na viwavi.

Angalizo: Ni muhimu kuwa waangalifu, kwa kuwa mimea inahitaji wadudu kwa ajili ya uchavushaji, kitunguu swaumu hukimbiza nyuki pia, hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa unapulizia wakati wa jioni sana au usiku.

Unaweza kutengeneza mchanganyiko wa kitunguu swaumu kulingana na mahitaji yako. Hapa tuchukulie mfano wa utengenezaji wa lita 100:

Mahitaji:

  • Kilo 16 za kitunguu swaumu
  • Mililita 400 za mafuta ya kupikia
  • Gramu 350 za sabuni (Sabuni ya kijani au njano inafaa)
  • Lita mia moja (100) za maji

Namna ya kuandaa

  • Saga, au twanga kitunguu swaumu, weka kwenye chombo cha plastiki chenye mafuta ya kupikia na maji ya kutosha kufunika kitunguu swaumu.
  • Changanya sabuni na maji kiasi, kisha yaliyobaki mimina kwenye mchanganyiko wa vitunguu swaumu na mafuta.
  • Chuja kwa kutumia kitambaa kizito au blanketi.

Baada ya kuchuja, unaweza kutunza kwenye chenye mfuniko na uanze kutumia baada ya siku 15. Unatakiwa kutengeneza mchanganyiko wa siku 15 tu na si zaidi. Ili kuwa na matokeo mazuri zaidi, andaa mchanganyiko unaoweza kutumika kwa wiki moja tu.

Kiwango cha matumizi

  • Tumia mililita 11 za mchanganyiko wa kitunguu swaumu kwa lita moja ya maji.
  • Nyunyiza kila baada ya siku 4-7
  • Punguza kiasi cha mnyunyizo kama wadudu siyo wengi, au kadri wanavyopungua

*Mchanganyiko huu hutumika kwa aina zote za mazao ya mbogamboga na matunda.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *