- Kilimo

Jifunze kutayarisha mboji kwa kurundika malighafi

Sambaza chapisho hili

Naomba kujua namna ya kuzalisha mboji kwa kurundika takataka ili kutumia kwenye bustani yangu ya mbogamboga (Joyce Evance Dodoma, 0763 772655)

Mbinu ya kutayarisha mboji kwa kurundika hufaa zaidi kufanyika katika maeneo yanayopata mvua nyingi. Katika maeneo yanayopata mvua kidogo mbinu ya kutengeneza mboji kwa kutumia shimo hupendekezwa na ni njia nzuri zaidi.

Ili kufanikisha zoezi la uzalishaji wa mboji kwa njia ya kurundika, ni lazima mkulima kuhakikisha anafuata hatua kwa hatua mbinu za kurundika na kuzalisha .

Hatua za kufuata kuzalisha mboji kwa kurundika malighafi

Kabla ya kuanza kurundika malighafi, chagua mahali palipo karibu na eneo ambalo mboji itakayozalishwa itatumika na hakikisha mahali hapo pamekingwa dhidi ya upepo, mvua, jua na kusababisha mchuruziko wa maji.

  • Pima eneo la mstatili lenye upana wa sentimita 120 kwa urefu wa sentimita 150 au unaweza kulifanya kuwa refu zaidi. Urefu utategemea kiasi au wingi wa malighafi utakavyoweka kwa ajili ya kutengenezea mboji yako.
  • Baada ya kuchimba anza kuweka rundo la malighafu kwa kutanguliza vitu vigumu kama vile mabua ya mahindina vitawi vilivyokatwa kutoka katika majani kama safu ya chini kabisa kwenye shimo.
  • Ongeza safu ya pili ambayo itakuwa na uoto uliokauka kwa mfano nyasi na safu hii iwe na unene wa sentimita 15. Rundo lote linatakiwa kuwa na unyevunyevu hivyo baada ya kupanga safu hii hakikisha nayo unanynunyizia maji.
  • Weka safu ya tatu yenye tope au samadi laini au majimaji ya biyogesi (samadi huwa na viini ambavyo mara nyingi ndivyo husaidia katika uozeshaji).
  • Baada ya kumaliza, nyunyizia jivu katika safu hii kwani jivu huwa na madini muhimu kama potashiamu, kalisi na magnesiamu ambapo husaidia kuzimua aside inayotolewa wakati wa kuozesha hasa pale samadi inapotumika.
  • Ongeza safu ya uoto wa kijani yenye unene wa sentimita 15 hadi 20 na hakikisha unatumia majani ya kijani kibichi hasa kutoka katika miti ya jamii ya mikunde ambayo huwa na kiasi kikubwa cha protini.
  • Baada ya kupanga safu hii, nyunyizia kiasi kidogo cha mboji ya zamani au udongo wa juu, kwani udongo wa juu huwa na bakteria muhimu sana kwa ajili ya uozeshaji.
  • Ongeza safu nyingine kwa zamu ukianza na uoto mkavu, kisha samadi, majimaji ya baiyogesi, majivu, uoto wa kijani na udongo wa juu (hakikisha kila safu ukishamaliza kuweka unanyunyizia maji juu yake).
  • Baada ya kukamilisha rundo, funika rundo lote kwa safu ya juu ya udongo yenye unene wa sentimita 10. Hii safu itasaidia kuzuia virutubishaji vya mimea kupotea kutoka katika rundo la mboji.
  • Funika rundo lote kwa kutumia uoto uliokauka kama vile majani ya migomba ili kupunguza kupotea kwa unyevu kutokana na maji kutoweka kama mvuke.
  • Chukua kijiti kirefu chenye ncha kali kisha ukiingize katika rundo kimshazari ili kipite kutoka juu kwenda hadi chini. Kijiti hiki kitatumika kama kipimajoto chako.
  • Baada ya siku tatu, uozeshaji utakuwa tayari umeanza na ukikivuta kijiti chako nje kutoka katika rundo utakuta kijiti kitakuwa na joto.
  • Vuta kijiti chako nje mara kwa mara ili kuona jinsi gani uozeshaji unavyoendelea. Na kutokana na kijiti hiki, unaweza kujua kiwango cha ukavu au umajimaji ulivyo katika rundo na itakusaidia kuweka unyevu unaotakiwa lakini si umajimaji.

Kupindua malighafi

Baada ya kipindi cha majuma mawili hadi matatu, pindua rundo, na usiongeze kitu au malighafi ya aina yeyote isipokuwa maji tu. Pindua rundo ikiwa kipimajoto kitakuwa cha ubaridi au kikiwa na chembechembe nyeupe kwa nje hii inaonyesha kuwa uozeshaji umesimama.

Upinduaji wa rundo ni muhimu kwasababu utasaidia katika kuchanganya safu mbalimbali na kuharakisha uozeshaji na kuufanya uenee kote katika rundo.

Mboji huwa tayari baada ya muda gani

Baada ya majuma manne mboji itakuwa tayari lakini pia angalia hali ya joto ili kuwa na uhakika. Ikiwa kijiti kina joto mara unapokivuta nje basi bado rundo linaendelea kuoza na mboji haiku tayari kwa matumizi.

Mboji iliyotayari huwa na harufu ya udongo mbichi na huwa haina nyasi, samadi wala majani kwani vyote vimekwisha kuozeshwa na kuchanganyika vyema.

Mboji yako inapokuwa tayari, unaweza kuanza kuitumia shambani au kuihifadhi kwa kufunka kwa kutumia majani ya migomba au karatasi ya plastiki laini kwa ajili ya matumizi yajayo.

Muhimu

Hakikisha rundo kwa ajili ya mboji haliwi kavu sana na wala lisiwekwe maji mengi kupindukia.

Usipanue mstatili kwa zaidi ya sentimita 120 kwasababu utahitajika kufanya kazi kwenye mboji bila kukanyaga juu yake.

Katika maeneo yenye mvua nyingi ni bora kutayarisha mboji katika rundo juu ya ardhi na kwenye maeneo makavu ni vyema kutengeneza mboji kwa kurundika kwenye shimo.

Hakikisha hayo mabua na matawi ya majani yamekatwa katwa ili kuwezesha hewa kuzunguka kwa urahisi kwenye tabaka hilo na ukimaliza kupanga nyunyizia maji.

Nyunyiza maji kwenye rundo pale unapogundua kuwepo kwa ukavu hasa baada ya siku tatu, na ikiwa mvua imenyesha usiweke tena maji katika rundo hilo.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *