- Kilimo Biashara, Samaki, Usindikaji

Namna bora ya uchakataji na uhifadhi wa samaki ili kuzuia wasiharibike

Sambaza chapisho hili

Ufugaji samaki kwa sasa umeshika kasi kutokana na ulaji kuongezeka taktibani katika maeneo yote ya nchi.

Ili kuhakikisha kuwa mfugaji anaweza kufanikiwa katika hatua zote za ufugaji mpaka hatua ya kupeleka bidhaa yenye ubora ni muhimu sana kuzingatia uhifadhi.

Kwanini uhifadhi wa samaki

Samaki kama viumbe vingine visipohifadhiwa vizuri na katika utaratibu maalumu wa kitaalamu, ni rahisi sana kuharibika na kuoza hivyo kumpelekea mfugaji kupata hasara.

Ikiwa mfugaji ametumia kipindi cha miezi sita mpaka saba katika ufugaji kisha akavuna samaki wale lakini akashindwa kufuata taratibu na kanuni bora za uhifadhi basi ni hakika kwake atakutana na changamoto mpya ya uharibifu jambo ambalo pengine hakuweza kutegemea kama linaweza kutokea.

Ili kuepukana na changamoto hii, Mkulima Mbunifu itakuelimisha nini cha kufanya mara tu unapovuna samaki ili kuweza kuwa na bidhaa yenye ubora unaohitajika sokoni.

Nini cha kufanya

Kwanza, hakikisha umelenga soko hasa ni wapi, wateja gani unaotaka kuwauzia. Mfano, kuuza mwenyewe reja reja yaani mara tu unapovuna au kuvua bwawani unamuuzia mteja moja kwa moja.

Njia ya pili ni kwa kuwauza wote kwa mara moja, yaani unafanya tangazo la kuvuna ukiwaeleza wateja kuwa siku fulani nitauza samaki hivyo unawaalika wanunuzi waje shambani kunuanua mara tu unapovua.

Njia ya tatu ni kuuza samaki kwa kupeleka sokoni mwemyewe yaani unavuna na kuwapaki kwenye vyombo na kisha kupeleka sokoni moja kwa moja. Hii inaweza kuwa aidha kupeleka na kuwauza wakiwa wabichi au kuvuna na kukausha kisha kupeleka sokoni.

Katika kipengele cha kulenga soko ni vyema kukumbuka kuwa ufugaji samaki umetofautiana sana kulingana na ukubwa wa bwawa na idadi ya samaki wanaofugwa mathalani kuna wanaofuga samaki 100 wengine 10,000 na hata zaidi.

Aidha wengine wanafuga sato na wengine wanafuga kambale hivyo katika hatua zote hizo kuna umuhimu mkubwa sana wa kutambua kama una idadi ndogo au kubwa ni kwa namna gani utahakikisha samaki wanabaki na ubora mpaka kufika sokoni.

Kwa wafugaji ambao wamefuga na lengo kuu la kuuza kidogo kidogo tunawashauri kuhakikisha kuwa wanaepuka unavuaji wa mara kwa mara yaani kuingia ndani ya bwawa kila saa kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kupelekea michubuko kwa samaki wengine wakati unavua kwa kutumia  nyavu.

Kwa mfano; amekujawa mteja wa samaki anahitaji kilo moja unaingia bwawani na kuvua, halafu baada ya nusu saa anakuja mteja mwingine unaingia tena kwenye bwawa unavua, kitendo hicho cha mara kwa mara kinaweza kupelekea vifo pia kwa samaki wengine au kuharika pasipokujua hivyo inapelekea kupunguza ubora na kiwango ulichokusudia kuuzia samaki wako.

Njia salama ya kulinda ubora wa samaki

Njia bora na pekee ambayo ni salama na yenye kuhakikisha kuwa samaki wanakua na ubora, ni kama bwawa lako ni kubwa hakikisha unakuwa na neti maalumu ya kuwahifadhia ambayo kwa kitaalam inaitwa Happanet.

Neti hii inashonwa kwa ukubwa maalum kulingana na nafasi ya bwawa, kwa mfano; bwawa likiwa na ukubwa wa mita 10 kwa mita 10 unaweza kushona au kununua nyavua yenye ukubwa wa mita tano kwa tatu kusha unafunga ndani ya bwawa kwa ajili ya kuvunia samaki.

Kwa mfano, kama bwawa lina sama 500 unavuna samaki 200 kisha unawaweka ndani ya hiyo neti nah apo itakurahisishia mteja anapokuja unanyanyua tu neti na kutoa samaki hivyo wale 300 wa kwenyewe bwawa wanakuwa hawaguswi tena.

Kwa kufanya hivyo mteja atapata kilicho bora huku mfugaji akiwa amefanya uhifadhi wa gharama nafuu sana kulinganisha na uhifadhi wa kwenye jokofu au barafu hususani katika idadi hiyo na aina ya wateja kwa reja reja.

Matumizi ya jokofu pia ni sawa ila gharama ya nishati ni kubwa lakini pia endapo nishati hiyo inakosekana uwezekano wa kuharibika ni mkubwa pia.

Hakikisha wakati wa kuvuna samaki unakuwa na vifaa vya kutosha vya kuhifadhia mara baada ya kuvua samaki na ni vyema sana kuwa na barafu pindi unapovuna na kuwahifadhi ndani ya mabeseni ili samaki hao wasiharibike haraka.

Toa mautumbo ya samaki ili wasiharibike. Utoaji wa mautumbo ya samaki husaidia sana kuhakikisha kuwa samaki wanabaki katika ubora mkubwa na kufika sokoni bila kuharibika kwa mautumbo hupelekea kuharibika kwa haraka sana.

Pia, waweza kuwa na usafiri maalumu wenye kuzalisha barafu hasa kwa ajili ya usafirishaji wa mbali zaidi.

Dalili za samaki kuanza kuharibika

Mashavu ya samaki kuanza kubadilika rangi kuwa na nyekundu iliyofifia sana.

Nyama ya samaki kutokurudi juu tena kirahisi hasa pale unapombonyeza

Samaki kuanza kutoa harufu

Samaki ambae bado hajaharika kwenye mashavu au matamvua yake yanakuwa na rangi nyekundu kabisa na ukimbonyeza nyama yake hurudi juu au kwa lugha nyingie haibonyeziki.

Njia kuu za uchakataji wa samaki na umuhimu wake

  • Kupunguza kasi ya kuharibika na kuzuia upotevu wa viasili.
  • Kulinda usalama na afya ya mlaji.
  • Kurefusha kipindi cha kutumika na utunzaji wa mazao yaliyochakatwa.
  • Kuongeza thamani ya zao na kuzalisha bidhaa mbalimbali kulingana na matakwa ya mlaji.
  • Kurahisisha uhifadhi na usambazaji.
  • Kuboresha ladha ya aina ya bidhaa

Mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa uchakataji

Ili kufanya uchakataji wa samaki, ni muhimu kuhakikisha una vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya uchakataji ili kuweza kufanya uzalishaji bora wa bidhaa.

Vitu vinavyohitajika

  • Eneo maalum linalokusudiwa kwa ajili ya uchakataji.
  • Vifaa au malighafi kwa ajili ya kazi husika.
  • Hali ya afya na usafi wa wahudumiaji.
  • Upatikanaji wa maji safi na salama.
  • Kuweka mfumo wa udhibiti wa taka ngumu na maji taka.
  • Eneo la kuhifadhia malighafi na bidhaa.
  • Upatikanaji wa aina ya vifungashio.
  • Uzio kwa ajili ya kudhibiti wanaoingia na kutoka katika eneo la uchakataji.

Muhimu:

Kama uchakataji utafanyika eneo la shambani ni muhimu sana kuzingia usafi katika hatua zote za uchakataji.

Aina za uchakataji

Kukausha kwa jua

Njia ya kuchakata samaki kwa kutumia nishati ya jua hufanyika kwa lengo la kuondoa maji, vimelea na ili visilete uharibifu wa samaki.

Faida

  • Gharama ya nishati hii ni rahisi.
  • Husaidia kupunguza gharama za ujazo
  • Hurahisisha ubebaji na ufungashaji.
  • Gharama ya vifaa vinavyohitajika aghali sana.

Changamoto za kukausha kwa jua

  • Haitumiki wakati wa kipindi cha mvua au mawingu
  • Inahitaji eneo kubwa la uchakataji
  • Unahitaji muda mrefu kukamilisha uchakataji.
  • Unahitaji idadi kubwa ya watendaji.
  • Kuongeza gharama ya kuandaa vichanja.

Kukausha kwa chumvi

Njia hii ya kuchakata samaki kwa kutumia madini ya chumvi husaidia pia kuondoa maji na kuondoa vimelea na kuvifanya visilete uharibifu wa samaki.

Faida

  • Huhitaji eneo dogo tu la kufanyia kazi.
  • Gharama ya kuthibiti muingiliano ndani ya eneo la uchakataji ni ndogo.
  • Huongeza ladha na madini katika aina ya zao.
  • Haitegemei sana hali ya hewa.
  • Hupunguza kasi ya ukuaji wa vimelea vinavyopelekea kuharika kwa samaki.

Kukausha kwa moshi

Njia ya kuchakata samaki kwa kutumia moshi ni ili kuondoa maji na vimelea kisha kuvifanya visilete uharibifu wa samaki.

Faida

  • Inahitaji eneo dogo la kufanya uchakataji.
  • Haitegemei hali ya hewa kuwezesha uchakataji.
  • Inaongeza muonekano na rangi ya kuvutia katika bidhaa.
  • Inaongeza muda wa kuhifadhi na utunzaji wa bidhaa.

Kukausha kwa kukaanga

Hii ni njia ya kuchakata samaki kwa kutumia mafuta ya kula kwa kukaangia ili kuondoa maji na kuondoa vimelea na kuvifanya visilete uharibifu wa samaki.

Faida

  • Inaongeza ladha ya aina ya bidhaa.
  • Inahitaji eneo dogo la kufanya uchakataji.
  • Haitegemei hali ya hewa kuwezesha uchakataji.
  • Inaongeza muonekano na rangi ya kuvutia katika bidhaa.
  • Inaongeza muda wa kuhifadhi na utunzaji wa bidhaa.
  • Gharama ya upatikanaji wa nishati ni ndogo.
  • Inahitaji muda mfupi kukamilisha uchakataji.

Kugandisha na kupoza kwa kutumia barafu

Hii ni njia kuu ya uchakataji katika kuhifadhi samaki wakati unajiaanda kupeleka sokoni.

Faida

  • Inahitaji muda mfupi kukamilisha uchakataji.
  • Inalinda uasili wa bidhaa.
  • Unaweza kusafirisha umbali mrefu.

Ukizingatia haya kwa kushirikiana na mtaalamu kwa ukaribu zaidi unaweza kufanikiwa zaidi na kuepukana na changamoto ambazo ulikuwa unakutana nazo wakati unapokaribia kuvuna samaki wako.

Kwa maelezo zaidi wasiliana na Musa Saidi Ngametwa kutoka Acquaculture Investment 0718 988628

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *