- Mifugo

Zuia ndama kuhara kutokana na unyweshaji maziwa

Sambaza chapisho hili

Muda wa kumlisha au kumnywesha ndama unatakiwa uwe sawa kila siku na joto la maziwa lisibadilike, liwe hilohilo kila siku. Aidha, unyweshaji wa maziwa sharti ufanywe katika hali ya usafi ili kuondoa uwezekano wa ndama kuharisha au kupata ugonjwa wa pneumonia na magonjwa mengine.

Tahadhari za kuchukua wakati wa kumnywesha ndama

  • Hakikisha maziwa unayomlisha ndama hayajazidi kiwango kinachostahili ndama kulisha kwa siku na isiwe tofauti na siku zingine
  • Ndama ni lazima anyweshwe maziwa mapema kadri iwezekanavyo mara baada ya kukamua. Kwa kufanya hivyo utaondoa uwezekano wa bakteria kupata nafasi ya kuzaliana ndani ya maziwa wakati yakiwa kwenye ndoo na kuleta madhara kwa ndama.
  • Ndoo au chombo cha kunyweshea maziwa visafishwe vizuri kila baada ya kutumika kwa kutumia maji safi ya baridi na sabuni na tena rudia kwa maji moto ili kusaidia kuangamiza vijidudu.
  • Chombo kikishaoshwa kianikwe juani ili kikauke na kisha kiwekwe mahala pasafi panapofaa tayari kwa kutumia kwa wakati husika. Chombo hicho kitumike kwa ajili ya kunyweshea ndama tu na kisitumike kwa kazi nyingine.

Nini cha kufanya kama ndama ameanza kuharisha?

  • Iwapo ndama ataanza kuharisha, acha mara moja kumnywesha maziwa mpaka pale atakapopona.
  • Badala ya kumnywesha ndama maziwa, mnyweshe maji safi na salama yenye uvuguvugu na ikiwezekana weka chumvi kidogo au glucose.
  • Hakikisha maji unayomnywesha ndama kwa wakati huo ni ya kutosha kwani maji ni muhimu sana kutokana na ukweli kuwa kinachosababisha kifo cha ndama wakati wa kuharisha ni kukosekana kwa maji mwilini.
  • Kama imethibitishwa kuwa kinachomfanya ndama kuharisha si unyweshaji wa maziwa mengi kupita kiasi basi apewe dawa za viua bakteria yaani antibiotic.
  • Wafunze ndama kula vyakula na malisho makavu wakiwa na umri wa majuma mawili ili kuwasaidia wasiharishe. Unaweza kumpa vyakula vya kusindika kwenye mdomo au kuweka kidogo kwenye ndoo au chombo mara tu anapomaliza kunywa maziwa kwenye chombo hicho.

Kiasi sahihi cha maziwa kwa ndama

Ili ndama aweze kukua kwa kasi ya wastani inapendekezwa apewe viwango vifuatavyo vya maziwa kufuatana na umri wake;

  • Katika umri wa majuma mawili tangu kuzaliwa, inashauriwa ndama aanze kunyweshwa maji na kupewa kiasi kidogo cha vyakula vya kusindika pamoja na malisho.
  • Ndama anaweza kulishwa mara 2-3 kwa siku katika kipindi cha juma la kwanza tangu kuzaliwa na halafu mara 2 kwa siku hadi atakapoachishwa maziwa akiwa na umri kati ya miezi miwili hadi minne kufuatana na lishe anayopata.
  • Unaweza kumpatia ndama hadi 50% ya maziwa ya kiasi kinachopendekezwa lakini kwa uangalifu ili kuzuia kuharisha. Haishauriwi kumnywesha ndama maziwa kidogo kuliko kiasikinachopendekezwa na kila ndama anatakiwa kupata lita 300 za maziwa kama kiwango cha chini kabisa tangu kuzaliwa hadi kuachishwa maziwa.
  • Wafugaji pia wanaweza kuwapa ndama maziwa mengi kwa muda mfupi kisha kuwaachisha au kuwapa maziwa kidogo kwa muda mrefu huku wakiwalisha nyongeza ya vyakula vya kusindika. Njia zote hizi ni sawa na hazina madhara kwa ndama.
  • Pia, ndama wanaweza kulishwa maziwa maalumu ya unga ambayo hukorogwa kwenye maji kama mfugaji atakuwa na uwezo na yanapatikana.

Kwa maelezo zaidi, wasiliana na mtaalamu wa mifugo Dkt Linus Prosper kwa simu +255756663247

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *