- Mifugo

Wataalamu wanashauri nyama isioshwe

Sambaza chapisho hili

Nyama ni miongoni mwa vitoweo vinavyopendwa kwa sababu ya ladha yake nzuri na wingi wa viini lishe. Nyama ni chanzo kizuri cha protini na madini ya chuma na kwa sababu hiyo, kuna ongezeko kubwa la matumizi yake mijini na vijijini.

Miongoni mwa changamoto zinazoambatana na matumizi ya nyama kama kitoweo, ni usafi na usalama wake kwa afya ya watumiaji.

Usafi na usalama wa nyama huathiriwa na mazingira duni ya ufugaji, machinjio yasiyozingatia kanuni za afya, usafirishaji wa nyama katika magari machafu, maduka yasiyozingatia viwango vya uuzaji na ukataji pamoja na watayarishaji wa nyama wasiozingatia kanuni za afya.

Kutokana na mazingira hayo pamoja na kuchafuliwa kwa nyama, watu wengi huamua kuosha kwa kuamini kuwa kufanya hivyo kunaifanya iwe safi na salama kabla ya kuipika, kuichoma au kuikaanga jambo ambalo wataalamu wa masuala ya afya ya jamii wanabainisha kuwa, kuosha nyama ya aina yoyote ni swala lisilokubalika kiafya. Hii ni kutokana na ukweli wa kisayansi kuwa uoshaji wa nyama unasambaza magonjwa.

Utafiti unasemaje

Utafiti uliofanywa katika manispaa ya Morogoro mwaka 2010 na 2011 ulibaini kuwa, nyama ni moja ya vyanzo vya magonjwa ya maambukizi kwa binadamu.

Katika utafiti huo ulioongozwa na Erick V.G. Komba na wenzake kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), kwa kishirikina na watafiti wengine kutoka katika Chuo Kikuu cha Sayansi za Afya Muhimbili (MUHAS), kulibainika mambo mapya, ambayo jamii ya sasa inahitajika kuyazingatia ili kuweka afya zao sawa. Hii ni kutokana na kugundua kuwa nyama inaweza kubeba aina mbalimbali za vimelea vya magonjwa.

Wataalamu wanasema kuwa, watu wengi wanafikiri ni lazima waoshe nyama, lakini kwa kweli hakuna haja ya kufanya hivyo kwani utafiti unaonyesha kuwa kuosha nyama ni jambo linaloweza kusambaza bakteria hatari ndani ya jiko lako au katika sehemu za kuandalia chakula.

Aidha, kuosha nyama kwa maji yanayotiririka, kunaweza kusambaza vimelea vya magonjwa kwa umbali unaofikia futi tatu.

Hakuna sababu za kisayansi zinazoendana na fikra kuwa kwa kuosha nyama unaifanya kuwa salama, usalama wa nyama unapatikana kwa kupika tu, kuiosha ni jambo linalofanya mlo kuwa hatarishi.

Mbali na nyama kuwa na vimelea vingine vya magonjwa, uoshaji wa nyama unaweza kusambaza zaidi bakteria aina ya Campylobacter jejune na Salmonella wanaosababisha maradhi ya kuharisha, kuhara damu na homa ya matumbo.

Bakteria hawa wanaweza pia kusababisha uvimbe wa maungio, matatizo ya macho, uvimbe wa njia ya mkojo, kuharibika kwa ujauzito na ugonjwa wa kupooza. Hali hii inaweza kuwa mbaya zaidi kwa watoto wadogo, wanawake wajawazito, wazee wenye umri zaidi ya miaka 65, watu wenye upungufu wa kinga mwilini na wagonjwa wenye tatizo la saratani.

Nini kifanyike

  • Ili kuhakikisha kuwa nyama haiwi chanzo cha matatizo ya afya ya jamii, ni busara wasambazaji, waandaaji na walaji wa nyama wakazingatia kanuni za usafi na usalama wa nyama kama zinavyoelezwa na wataalamu wa afya.
  • Wataalamu kutoka SUA wanashauri kuwa, ni vyema sana jamii ikapata elimu na maelekezo ya kutosha kutoka kwa maofisa wa afya ambao wameelimishwa kikamilifu juu ya usalama na usafi wa nyama.
  • Aidha, uzingatiaji wa utoaji wa elimu ya kutosha kwa wadau wote juu ya mazingira na maandalizi mazuri ya nyama kuanzia uchinjaji, usafirishaji, uuzaji.

Hii itasaidia walaji kutokuosha nyama kwani wengi wao wanadai kuwa, wanaosha kutokana na sababu kuwa wanaponunua nyama madukani mara nyingi zinakuwa na uchafu wa aina nyingi kama vile mchanga, udongo, vipande vya miti na makaratasi hivyo wasipoosha watakula uchafu.

Pia, kutokana na sababu kuwa sehemu wanazokatia kwenye mabucha ni magome ya mit, wakati wa kukatakata nyama vipande vinajishika kwenye nyama hiyo hivyo walaji wanalazimika kuosha.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *