- Mifugo

Utupa (Tephrosia vogelii) Mmea wenye faida nyingi kwa mazingira na wanyama

Sambaza chapisho hili

Utupa ua kitaalamu Tephrosia vogelii ni mti mdogo wa jamii ya mikunde, wenye mizizi yenye vifundo vyenye bakteria maalumu wenye uwezo wa kubadili hewa ya Nitrogeni iweze kutumiwa na mmea kama nishati inayohitajika kwenye ukuaji wake.

Utupa unaweza kupandwa kwa ajili ya kuboresha na kurutubisha udongo, kuni, kuua wadudu washambuliao mazao yaliyohifadhiwa na wadudu warukao (wanaoshambulia mazao wakati wa ukuaji).

Tahadhari: Mmea huu ni sumu kwa samaki na umekatazwa kwa matumizi kwenye baadhi ya nchi za ukanda wa kitropiki. Hii ni kutokana na sumu inayopatikana kwenye majani na mbegu (Rotenone).

Urutubishaji wa udongo

Majani na mbegu za utupa vimebeba kiasi kikubwa cha virutubisho, hasa naitrojeni  na kaboniki ambayo ni muhimu sana kwa ukuaji wa mmea.

Mti huu ukikatwa majani yake baada ya kuoza hutumika kuongeza rutuba katika udongo. Pia yanaweza kutumika kama mbolea ya kijani.

Vilevile, inatumika kuongeza rutuba mbalimbali kwenye udongo na hasa katika kilimo mseto kwa maendeleo endelevu ya mimea. Utafiti umeonesha ina uwezo wa kufanya ongezeko la asilimia thelathini (30%) ya virutubisho vya udongo, hivyo kuleta tija ya mavuno mengi asilimia kati ya (23-26). Pia utafiti umebaini matumizi ya Utupa yameweza kudhibiti wadudu waharibifu kwa asilimia 46.2-52.2.

Ukusanyaji wa mbegu

Kukusanya mbegu za Utupa, inatakiwa uchukue (brown pods) mbegu zilizokomaa moja kwa moja kutoka mtini. Baada ya kukusanya mbegu ambazo hazijamenywa hakikisha unaanika juani kwa siku mbili hadi tatu (2-3) ili zaikauke vizuri. Kisha zichambue  na kupembua.

Utunzaji wa mbegu: Mbegu zikaushwe angalau kwa siku tatu hadi nne (3-4) zikiwa chini ya kivuli. Haina haja ya kuzikausha kama zitapandwa/kuoteshwa ndani ya miezi miwili baada ya kuvunwa.

Mbegu zinaweza kutunzwa zaidi ya mwaka mmoja, kama zimehifadhiwa kwenye mfuko au chombo kisichopitisha hewa na pasipo na unyevu, katika hali ya ukavu.

Upandaji wa utupa

Utupa unaweza kuoteshwa kwa mistari au bila mpangilio. Upandaji kwajili ya matumizi ya mbolea ya kijani, inashauliwa umbali nafasi ya 40cm X 40cm, mbegu 2-3 kwa shimo; na upandaji kwenye kingo za shamba itumike nafasi ya 1.5m kati ya shimo moja na lingine. Ikiwa shamba ni kubwa la hekari nyingi, andaa mbegu za kutosha ili kurudishia zitakazoshindwa kuota. Upandaji katika mistari, inashauriwa kuandaa kiasi cha 5kg/ha au kupanda kwa kusia andaa 8-13kg/ha.

Mbegu zinaweza kupandwa katikati ya mahindi pia kwenye matuta. Ni muhimu eneo lisiwe tindiga/majimaji kwavile Utupa haustahimili eneo. Mmea huu unatakiwa kupandwa mwanzo wa masika au katikati ya kipindi cha mvua. Kama unapanda pamoja na mahindi unaweza kupanda kwa pamoja au baada ya wiki chache mahindi yakishaota hadi katikati ya kipindi cha mvua ili kuhakikisha mmea unapata mvua ya kutosha. 

Fuko, Panya wa shambani (Mastomys Natalensis) and Panya wa nyumbani (Rattus Rattus) Utupa ni mmea muhimu sana katika kudhibiti panya waharibifu wa mazao na mazingira.

Mmea huu umebeba sumu ambayo inawaathiri panya. Sumu hiyo hutambuliwa na panya kwanjia ya harufu kwavile panya ni wanyama hodari katika kugundua harufu. Mmea hutoa harufu ambayo sio rafiki kwa panya.

Sumu hiyo imesambaa katika maeneo yote ya mmea. Isipokuwa kwenye mizizi yam mea huu harufu hiyo hutoka kwa wingi, hivyo kumfanya panya akimbie kutoka kwenye eneo/shamba unapopatikana Utupa.

Mazao muhimu ya kupanda pamoja na utupa

Mazao jamii ya mizizi pia ya nafaka. Hii ni kutokana  na kwamba mazao haya hushambuliwa zaidi panya. Mbali na mazo ya mizizi na nafaka mazo mengine ambayo yanayoweza kutoharibiwa na panya kwa kutumia Utupa ni mazao ya migomba na miwa.

Mizizi ya mmea huu inatoa harufu mbaya hivyo harufu hiyo humfanya panya kushindwa kustahimili kuendelea kuishi(kula na kuzaliana) kwenye eneo husika.

Harufu hiyo humuhamisha, endapo atakula kutokana na sumu iliyomo  kwenye mmea huo itamsababishia kufa hivyo hawawezi kula mizizi wala majani ya mmea huo.

Kuhifadhia mazao yaliyo stoo

Majani ya Utupa yanaweza kutumika katika kuhifadhi mazao ya nafaka na mikunde mfano maharagwe. Chukua  majani mabichi kisha yakaushe kwenye jua. Saga kwa mashine au ponda majani makavu kuwa unga.

Ukichanganya gramu 100 ya huo unga na mahindi au maharage uazuiya wadudu wanaopekecha na kutoboa mazao(weevils, borer & bruchids). Hii ib ani imara kwa muda wa miezi mitatu(3). Baada ya muda huo zoezi lirudiwe (weka tena unga wa utupa). Hakikisha unaosha vizuri mazao yaliyokuwa yamehifadhiwa na unga wa Utupa kabla ya kutumia mazao kwajili ya chakula.

Kuwakinga mifugo

Saga au ponda majani mabichi ya Utupa, changanya na maji lita tano(5) kwa kilogramu 1  kupata juisi kisha waoshe mifugo kwa mchanganyiko huo.

Hii tiba itaondoa kupe waliong’ang’ania ngozi ya mnyama. Sumu ya Utupa (Rotenones) ni hatari kwa nguruwe, hivyo umakini mkubwa unahitajika wakati wa kufanya hili zoezi kama unatibu nguruwe.

TAHADHARI: Zingatia kuwa Utupa ni hatari sana kwa viumbe kama binadamu, samaki, wanyama wa kufugwa na waporini. Utupa unapotumika hakikisha kujikinga ngozi au tumia glavu kama itawezekana.

Osha mikono kwa umakini ukitumia sabuni mara tu baada ya kumaliza shughuli ya kuweka kwenye mazao au kuosha wanyama. Usitumie Utupa kuulia samaki au kutupa katika vyanzo vya maji. Mmea huu hauruhusiwi katika nchi nyingi. Pia haufai kwa matumizi ya moja kwa moja kwa binadamu na wanyama kwa chakula.

Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana na Neema Mwakisambwe kwa simu +255764 646516

 

 

 

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *