- Mifugo, Usindikaji

Unaweza kusindika ngozi kiasili kupata bidhaa bora

Sambaza chapisho hili

Usindikaji wa viwandani unahitaji mitambo mikubwa, maeneo makubwa nguvu kazi kubwa, malighafi nyingi. Hivyo inahitaji mtaji mkubwa. Njia hii pia inahitaji kemikali za viwandani hivyo sio rafiki kwa mazingira.

Usindikaji wa asili  ni rahisi kwani malighafi za uchakataji hupatikana katika mazingira yanayotuzunguka. Njia hii inashauriwa sana kwa wajasiriamali wadogo wadogo ambao hawana mitaji mikubwa na unaweza kuchakata ngozi moja kwa siku. Njia hii pia ni rafiki kwa mazingira na afya ya jamii.

Usindikaji wa ngozi kwa njia ya asili

Ngozi husindikwa kwa ajili ya kuifanya kutokuharibika au kuiongezea ubora ili kuweza kutengenezea bidhaa mbalimbali kulingana na uhitaji katika jamii.

Usindikaji wa ngozi kwa njia ya asili hutegemea uwepo/upatikanaji wa malighafi ziliopo katika eneo husika kwa ajili ya kusindika.

Mahitaji

Ili kusindika ngozi, malighafi zinayohitajika ni pamoja na maji, magadi soda, sabuni, chokaa, chumvi, siki, mafuta, papai na ngozi.

Vifaa

Kisu cha kutolea manyoya, ndoo, karai/beseni, mbao, meza, misumari isiyoshika kutu na fremu ya kukaushia ngozi.

Namna ya kusindika

Vipimo hivi ni vya kuchakata ngozi Tano (5) za Mbuzi

  • Baada ya kupata ngozi safi na mbichi iliyotoka kwa mnyama, anza kusindika kwa kuloweka moja kwa moja (masaa 8) kwenye kimiminika cha chokaa (Lita 50 za maji, na chokaa kilo 2).
  • Toa ngozi kwenye kimiminika cha chokaa, na weka juu ya mbao manyoya yakiangalia chini, na anza kuonda nyama kwa kutumia kisu maalumu cha kuchunia.
  • Baada ya kutoa nyama, weka ngozi katika mchanganyiko wa pili wa chokaa na acha kwa muda wa siku 2. Kwa kila siku, ondoa ngozi kwenye maji na koroga maji kisha rudisha tena ngozi ndani ya maji. Baada ya siku hizi mbili ngozi itakuwa haina manyoya tena.
  • Toa ngozi kwenye maji na tengeneza mchanganyiko mwingine wa chokaa kisha weka ngozi ndani ya mchanganyiko huo kwa muda wa siku 2. Utakuwa ukitoa mara mbili kwa siku ili kukoroga maji na kisha kurudishia ngozi ndani.
  • Kama nywele bado hazijatoka zote, baada ya kutoa ngozi kwenye maji ya chokaa, ilaze kwenye ubao kwa sehemu ya nywele kuangalia juu kisha anza kutoa nywele kwa kutumia kisu maalumu cha kuchunia. Kuwa makini wakati wa zoezi hili ili makali ya kisu yasiweze kukata na kuharibu ngozi yako.
  • Baada ya kuondoa nywele zote, safisha ngozi kwa maji safi ya baridi ili kuondoa chokaa, fanya zoezi hili kwa kuosha na kumwaga maji mpaka chokaa itakapoisha kabisa.
  • Ngozi ikishakuwa safi, tengeneza mchanganyiko wa juisi ya limao (lita 10 za maji kwa lita 0.2 ya juisi ya limao) kisha dumbukiza ngozi ndani na acha kwa muda wa saa 12.
  • Ongeza maji moto kidogo katika kimiminika cha kuondoshea chokaa kisha, katia vipande vidogo vidogo vya papai bichi nusu kwenye mchanganyiko huo kisha baada ya masaa 2 ngozi itakuwa imelainika.
  • Toa ngozi kwenye maji kisha anza kuparuza ili kuondoa baadhi ya sehemu yenye nywele fupi zitakazokuwa zimesalia, mabaka meusi, vipele pamoja na masalio ya chokaa.
  • Baada ya kuparuza, tengeneza mchanganyiko wa lita 6 za maji na gramu 600 za unga wa magome ya mti, kisha dumbukiza ngozi katika mchanganyiko huo. Acha katika mchanganyiko huo kwa muda wa siku 7 huku ukikoroga mchanganyiko mara chache kwa siku.
  • Toa ngozi katika mchanganyiko wa magome ya mti kisha safisha kwa maji safi na weka juu ya meza huku tabaka la nyama likiangalia juu tayari kwa ajili ya kupaka mafuta.
  • Chukua gramu 120 za mafuta kisha chemsha kufikia nyuzi joto za sentigredi 60°C, katia katia sabuni gramu 80 katika lita 0.6 za maji kisha chemsha maji mpaka kufikia nyuzi joto za sentigredi 60°C, kisha changanya mchanganyiko wa mafuta na sabuni huku ukikoroga.
  • Chukua brashi safi na laini au kitambaa kisha anza kupaka mafuta katika sehemu ya juu ya ngozi ya tabaka la nyama.
  • Ngozi yako ipo tayari kwa ajili ya kuwambwa. Iwambe ngozi katika fremu ya mbao, kisha pakaa mafuta kiasi na anika juani kwa kuisimamisha fremu, au katika sehemu yenye upepo kiasi lakini hakuna vumbi.
  • Ngozi itachukua siku 1 hadi mbili kukauka toka kuwambwa. Baada ya hapo, ngozi ipo tayari kuuzwa ama kutengenezea bidhaa kama vile mabegi, viatu, pochi, mikanda, bangili nk.

Kwa mawasiliano zaidi wasiliana na Faraja  kutoka  Natural Maasai leather, kwa simu namba 0752838223

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *