- Mifugo

Unaweza kulima giligilani kukuza uchumi na pato kwa haraka

Sambaza chapisho hili

Kilimo cha Giligilani (Coriander) ni mradi mkubwa unaojitosheleza kukuza maisha ya mkulima kutokana na sababu kuwa zao hili la biashara huchukua muda mfupi toka kuotesha hadi kuvuna.

Zao hili linalotumika kama kiungo cha chakula katika mapishi ya vyakula mbalimbali kama nyama, supu au mchuzi linafaa kulimwa wakati wowote na katika maeneo mengi ya Tanzania hususani mikoa ya Mbeya na Iringa.

Aidha, kutokana na uhitajika mkubwa kutoka kwa watumiaji, pamoja na kugundulika kuwa lafaa kuoteshwa katika maeneo mengi ya nchi, basi limeifanya soko la zao hili kukua kwa kasi na kusababisha kilimo chake kupanuka kwa haraka sana siku hadi siku.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Aina za giligilani.

Kuna aina kuu mbili za giligilani ambazo ni giligilani fupi na ndefu. Aina zote hizi zinatumika kwa wingi na zinauzika katika masoko yote yaliyopo mikoani mwetu.

Giligilani fupi: Aina hii ni nzuri sana kwa mkulima yeyote anayetaka kulima kwa lengo la kuvuna mbegu. Hii ni kutokana na sababu kuwa, inatoa maua ikiwa fupi sana, inakomaa kwa haraka na mbegu zake ni nyingi. Aina hii si nzuri sana kwa kilimo cha kuvuna majani.

Giligilani ndefu: Hii ni aina ya giligilani ambayo ni bora sana kwa ajili ya kilimo cha kuvuna majani lakini pia mbegu zake hufaa kwa viungo. Aina hii hurefuka zaidi kabla ya kutoa maua na mbegu zake ni chache sana.

Hali ya hewa

Giligilani husitawi katika maeneo yote ya Tanzania, yenye joto lisilozidi nyuzi 20C hadi 25C (Kwenye mwinuko wa kuanzia mita 1000 hadi 1800). Pia husitawi katika maeneo yenye nyuzi joto zaidi ya 25C kwa kulima wakati wa mvua ambapo joto huwa limepungua. Hata hivyo, mikoa ya Mbeya na Iringa ni maeneo mazuri zaidi kulima zao hili kulingana na hali ya hewa ya ubaridi katika msimu wote wa mwaka.

Udongo

Zao hili linasitawi katika udongo wa aina yeyote lakini husitawi vizuri zaidi katika udongo wa tifutifu (Loam soil) na wa kichanga (Sand soil).

Utayarishaji wa shamba

Baada ya kutayarisha mbegu, hakikisha shamba lako limelimwa vizuri, limewekwa maji na lina mbolea ya kutosha. Mboji ni mbolea inayofaa zaidi katika shamba kwa ajili ya mavuno mengi na yenye ubora. Baada ya siku mbili toka kumwagiliwa, litifue tena kwa kutumia rato, kisha lisawazishe vizuri kuondoa mabonde na tayari kusia mbegu za giligilani.

Uoteshaji

Uoteshaji wa giligilani hutegemea sana umekusudia kuvuna nini au ni aina gani ya giligilani unaotesha. Kumbuka kuwa, giligilani hazisiwi katika kitalu bali huoteshwa ama kusiwa shambani moja kwa moja.

Uoteshaji wa kuvuna majani(giligilani ndefu)

Kama umekusudia kuvuna majani ni lazima uoteshe giligilani ndefu na unatakiwa kusia kama unavyosia mbegu za mchicha lakini hakikisha mbegu za giligilani hazitarundikana sana.

Uoteshaji wa kuvuna mbegu(giligilani fupi)

Ikiwa umekusudia kuvuna mbegu bila shaka unatakiwa kuotesha giliglani fupi ambayo utaweka mbegu katika mashimo. Umbali wa shimo hadi shimo liwe sentimita 10-15 na umbali kati ya mstari na mstari iwe ni sentimita 20.

Kuchipua

Giligilani huanza kuchipua kuanzia siku ya 8 hadi 15 toka kuoteshwa. Hakikisha katika siku 12 za mwanzo unamwagilia mazao yako kila baada ya siku mbili na baada ya hapo unaanza kumwagilia kila wiki mara mbili au tatu. Ikiwa mvua inanyesha, usimwagilie kabisa.

Kukomaa na kuvuna

Giligilani hukomaa vizuri baada ya siku arobaini (mwezi na siku kumi) na hapo huwa tayari kwa kuvunwa, japo wengine huanza hata kuvuna baada ya siku 23

Kama ni za kuvuna majani, hakikisha unaanza kuvuna kabla ya kuanza kutoa maua au mara baada ya kufikia urefu wa sentimeta 20. Hakikisha unang’oa wakati wa asubuhi kwa kung’oa mche pamoja na mizizi yake kisha kuziosha  ili kuondoa udongo wote. Baada ya hapo, zifunge kulingana na soko husika kisha peleka sokoni tayari kwa kuuza.Usikate mizizi yake.

Ikiwa unakusudia kuvuna mbegu, hakikisha mbegu zimekomaa kwa kubadilika rangi na kuwa kahawia. Ng’oa miche na rundika mahali pasipokuwa na maji ama unyevu kwa muda wa siku saba kisha zipige polepole hadi mbegu yote iachie katika majani, pepeta na paki tayari kwa kuuza.

Magonjwa na udhibiti

Giligilani tofauti na mazao mengine mara nyingi halisumbuliwi na magonjwa kabisa. Ni mara chache sana kushambuliwa na ugonjwa wa ukungu ambao husababishwa na wingi wa maji hasa linapooteshwa wakati wa mvua kubwa na wakati wa baridi kali.

Hakikisha unamwagilia kwa kiwango cha wastani huku ukiepuka kuotesha wakati wa mvua kubwa na wakati wa baridi kali.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *