- Mifugo

Umuhimu wa wakulima kuwa kwenye vikundi

Sambaza chapisho hili

Mimi ni msomaji na mdau wa jarida la Mkulima Mbunifu, ingawa sina kikundi. Napenda kufahamu kuwa ni kwa nini mmekuwa mkisisitiza wakulima kuwe kwenye vikundi, na ndipo wapatiwe huduma za Mkulima Mbunifu, nini umuhimu wa kuwa kwenye kikundi?

Kikundi ni muunganiko wa watu wenye nia/lengo moja katika kutekeleza jambo fulani walilolikusudia kwa faida ya hao walioamua kuwa pamoja.  Lengo kuu la kuwa na kikundi ni kutaka kufanya au kushirikiana kutatua matatizo kwa pamoja.

Vikundi vya wakulima, ni jukumuiko la wakulima na wafugaji wenye nia ya kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo kwa kutumia uwezo na ubunifu wao katika kuhamasisha ari ya wananchi kushiriki kwa pamoja katika kutafakari na kutafuta ufumbuzi wa jambo linalohitaji kutafutiwa suluhu.

Vikundi vinaweza kuwa kiungo muhimu na imara katika kusonga mbele kwa maendeleo ya wanakikundi wenyewe, jamii na Taifa kwa ujumla wake kwa kutumia vikundi katika maeneo yao.

Vikundi vinaweza kusaidia kuongeza ubunifu, ufumbuzi wa mambo mbalimbali na kuongeza msukumo katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wanachama na wananchi wengine.

Mtu mmoja anapofanya kazi peke yake ni vigumu kubadilisha hali fulani. Anaweza akakosa ujasiri wa kuleta mabadiliko, kuchukua hatua au kutoa maoni na kero zake. Badala yake kikundi cha watu wenye nia madhubuti na imani sawa kuhusu hali fulani wanaweza wakafanya mambo makubwa. Kwa kufanya kazi pamoja na kusaidiana; mabadiliko yanaweza kupatikana tena kwa haraka zaidi.

Kufanya kazi pamoja kunasaidia pia kujenga tabia ya kujiamini kama mawakala wa mabadiliko. Umoja pia unarahisisha kupata msaada kutoka nje au ndani ya jamii kuliko msaada huo kutolewa kwa mtu au mwanaharakati mmoja.

Aina na idadi ya wanakikundi

Aina ya  kikundi cha aina gani na wahusika watakua wangapi hutegemeana na lengo kuu la kuunda umoja huo. Kikundi kinaweza kuundwa na watu ambao wanafanya shughuli moja mfano kikundi cha wafuga nyuki, wakulima wa kahawa n.k.

Pia kikundi kinaweza kuudwa na watu wanao fanya shughuli zisizofanana lakini wakatambulika kwa jina moja. Hivyo lengo kuu ambalo litawaunganisha hawa mfano wanataka kufahamika, kupata soko, elimu, kufikiwa kirahisi na wadau nk.

Wazo la kuunda kikundi  hutokana na mchakato wa mawazo ya wahusika wenyewe ili kuunda kikundi imara na thabiti inabidi kuzingatia mambo yafuatayo:

  • Watu wa eneo moja
  • Mnafahamiana vyema
  • Muwe na nia ya dhati kuleta mabadiliko.

Inashauriwa angalau kikundi kianzie na watu watano na kiwe na idadi ya wajumbe ambao haigawiki kwa mbili (namba tasa) hii itasaidia kipindi cha kuchagua viongozi na pia katika kupitisha ajenda za kikundi, ingawa si lazima sana namba iwe tasa.

Kwa ufupi vikundi vina faida zifuatazo:-

  • Kujenga nguvu na utashi wa pamoja (umoja ni nguvu)
  • kurahisisha utendaji wa pamoja
  • Kubadilishana uzoefu (Kutiana moyo)
  • Kuelimishana na kupatiwa elimu kutoka kwa wahisani
  • Kushirikiana katika matumizi ya rasilimali

Tathmini ya aina na msingi wa kikundi

Kikundi kinaweza kuwa chombo kinachojitegemea au kikawa ni sehemu ya kikundi kimoja au taasisi fulani. Uanzishwaji na uendelezwaji wake unategemea sana wanachama wake, hivyo ili kuwa na kikundi chenye sauti na nia moja kuna haja kwa wanachama wake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kikundi kwa hiari na kwa kujituma. Siyo vizuri kwa kikundi kuwa tegemezi kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji na usimamizi wa shughuli zake.

Msaada toka kwa wadau wengine nje ya kikundi usiwe kipaumbele bali kichocheo tu katika kuleta mabadiliko. Ili kuleta mwelekeo mzuri wa vikundi hivi, huna haja ya wanakikundi kufanya tathmini yakinifu kutambua aina ya wanachama walionao.

Kama kikundi kitakuwa na wanachama wenye moyo wa kujitolea na walio tayari kuleta maendeleo ya kweli basi kikundi hakitaishi kwa utegemezi wa msaada kutoka nje hususani kwa wahisani.

Wanachama mchanganyiko na ushiriki wa makundi maalumu.

Kuwa na kikundi chenye wanachama mchanganyiko wajinsia na makundi mbalimbali ya watu kunatoa fursa ya kujenga kikundi imara chenye uwakilishi sawia.

Vikundi vya maendeleo havina budi kuwa na uwakilishi wa makundi mbalimbali ya watu walioko ndani ya jamii kama vile watu wenye ulemavu, wanawake na wajane, maana makundi haya yanahitaji msaada na upendeleo maalumu katika kushirikishwa katika maamuzi na pia katika maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Kujenga mahusiano mazuri

Ni vyema kuwa na mahusiano ya karibu (kiutendaji) na watendaji mbalimbali katika ngazi ya kijiji, kata na wilaya. Ni vyema pia kwa kikundi kuzifahamu sera mbalimbali, sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya vikundi.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Usajili wa kikundi

 

Ili kikundi kifanye mambo yake kwa uhuru na kwa upana zaidi ni vyema kikapata usajili. Usajili unaweza kuwa katika hatua mbili za msingi:

 

 

  1. Usajili katika serikali ya sehemu kinapo patikana

Huu ni utambulisho wa kikundi katika serikali ya sehemu husika mfano kwa afisa mtendaji kwa kueleza ni nini mnafanya kwa nini, viongozi wenu ni akina nani na mnafanyia sehemu gani. Hii ni hatua ya awali ambayo huweza kufanyika kipindi cha awali ambapo kikundi kinaanzishwa au kama kikundi bado hakijakamilika.

 

 

  1. Kupitia kwa msajili wa vikundi na ushirika

Hii ni ngazi nyingine ya usajili ambayo ni kubwa, ambayo hufanyika wilayani. Katika aina hii ya usajili, kikundi kinaweza kuwa kinaanza au kilikwisha anza. Hivyo unapokwenda kuomba usajiri huu kuna mambo ya  msingi ambavyo ni lazima uzingatie:

 

  1. Katiba ya kikundi
  2. Barua ya maombi kutoka ofisi ya kata unayotoka au kwa afisa maendeleo
  3. Mukhutasari ambao unaonesha ni lini kikundi kilikaa na kupitisha azimio la makubaliano ya kufanya usajili
  4. Gharama ya fomu ya maombi, ada na gharama ya usajili gharama hizi hutofautiana kutoka wilaya moja hadi nyingine

Mfumo huu wa kuungana umeweza kua na mchango mkubwa kwa mashirika binafsi na serikali katika kuwasaidia wakulima kwa

  1. Kutoa elimu na vitendea kazi. Serikali na mashirika binafsi wame weza kuwafikia watu wengi kwa njia hii kwa mfano uanzishwaji wa mashamba darasa
  2. Kudhaminiwa
  3. Kutafutiwa masoko na
  4. Kutambuliwa

 

Kwa kuzingatia hayo yote ni dhahiri kuwa wakulima na watu wengine wenye nia ya kupiga hatua katika maendeleo wanaweza kupiga hatua.

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *