- Kilimo, Mifugo

Ugonjwa wa kichocho na hatari zake kiafya

Sambaza chapisho hili

Ugonjwa wa kichocho umekua changamoto kwa jamii zinazoishi kandokando ya mito, na hasa katika maeneo yenye mashamba ya umwagiliaji. Tafiti zinaonesha asilimia 51% ya watanzania wapo kwenye hatari ya kupata ugonjwa huu hasa maeneo ya ukanda wa Pwani, ukanda wa ziwa Victoria, Tanganyika, Bwawa la nyumba ya Mungu-Mwanga na maeneo mengine yenye mashamba ya umwagiliaji.

Ugonjwa wa kichocho (schistosomiasis/snail fever/bilharzia) ni ugonjwa unaosababishwa na minyoo inayoitwa schistosomes wanaoshambulia sehemu za utumbo na/au kibofu cha mkojo kwa binadamu. Ugonjwa huu unaenezwa na konokono wanaoishi kwenye maji baridi aina ya Biomphalaria (kichocho cha tumbo) na Bulinus (kichocho cha mkojo).

Dalili za ugonjwa ni maumivu ya tumbo, kuharisha, damu kwenye choo au mkojo. Ugonjwa usipotibiwa unaweza kusababisha uharibifu kwenye ini, figo, ugumba, saratani ya kibofu cha mkojo, saratani ya utumbo, pia kusababisha kudumaa kwa watoto.

Ukubwa wa tatizo

Ugonjwa wa kichocho uligundulika kwenye karne ya 19 sehemu za kanda ya ziwa Victoria na visiwa vya Pemba na Unguja.  Miaka ya 1970-1980. Ugonjwa wa kichocho ulisambaa kwa jamii waliokuwa wakiishi karibu na miradi ya umwagiliaji na mabwawa ya kufua umeme kama Nyumba ya Mungu, wilayani Mwanga, Kilimanjaro.

Kwenye mwaka 2000, Tanzania ilikuwa ina idadi ya watu milioni 29.6, kati yao milioni 15.4 (52%) walikuwa wana kichocho cha tumbo na mkojo. Na mwaka 2009, ilikadiriwa watu milioni 19 wana kichocho.

Taarifa za karibuni zinaonesha mnamo mwaka 2012, idadi ya watu wote Tanzania, asilimia 51.5 wana kichocho hii kusababisha watu milioni 43.5 kuwa katika hatari ya kuambukizwa kichoocho.

Kwa taarifa iliyotolewa na Shirika la Afya la Dunia (WHO), mwaka 2015, inakadiriwa watu milioni 207 kote duniani wamepata maambukizi ya kichocho na kati yao asilimia 93 wanatoka chini ya jangwa la Sahara (Sub-Saharan Africa), Tanzania ikiwa ni nchi ya pili ikiongozwa na Nigeria.

Inakadiriwa kati ya watu 4,400 hadi 200,000 hufariki kila mwaka kutokana na kichocho. Kichocho kinapatikana zaidi Afrika, Asia na Amerika ya kusini. Inakadiriwa zaidi ya nchi 70 duniani, zaidi ya watu milioni 700 wanaishi kwenye hatari ya kupata kichocho.

Kwenye nchi za kitropiki, ugonjwa wa kichocho umewekwa nafasi ya pili ukiongozwa na malaria. Ugonjwa wa kichocho ni kati ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele kwenye nchi za kitropiki (Neglected Tropical Disease) haswa nchi zinazoendelea kiuchumi.

Inakadiriwa kwamba, kwenye mwaka 2017 angalau watu milioni 220.8 walihitaji matibabu ya kichocho na kati ya hao, watu milioni 102.3 wameripotiwa kutibiwa. Kundi la watu ambao wako hatarini kupata kichocho ni wakulima wa mashamba ya umwagiliaji, wavuvi na jamii isiyotumia maji safi na salama.

Maambukizi ya ugonjwa wa kichocho

Ili maambukizi yafanyike yafuatayo ni mambo muhimu yawepo: mgonjwa wa kichocho, konokono wa kichocho na mazingira ya  maji baridi. Mgonjwa wa kichocho akijisaidia choo au mkojo, anatoa pia na mayai ya minyoo wa kichocho. Mayai hayo yakiingia kweye maji yanaangulika na kubadilika na kuwa viluwiluwi ambao wanauwezo wa kuingia ndani ya mwili wa konokono husika.

Konokono wa kichocho cha tumbo ni aina ya Biomphalaria na wa kichocho cha mkojo ni aina ya Bulinus. Ndani ya majuma 3-4 viluwiluwi ndani ya mwili wa konokono wanakuwa na kuongezeka, baadae wanatoka wakiwa na maumbo tofauti, hukaa katika hii hali kwa muda wa siku1-2 hai kabla ya kupenya kwenye ngozi ya binadamu na kupitishwa sehemu mbalimbali za mwili kupitia mfumo wa damu.

Binadamu anapata maambukizi akiwa kwenye shughuli zake kama uvuvi, akioga kwenye mto/bwawa/ziwani/mferejini, umwagiliaji, kuogelea, kuvuka mto kwa kukanyaga maji. Basi kimelea kile kikifika kwenye ini anakuwa mnyoo kamili na kuambana kwa pamoja mnyoo dume na jike na kujishikiza kwenye mishipa ya damu kwenye tumbo (kichocho cha tumbo) na kibofu cha mkojo (kichocho cha mkojo) na kutaga mayai 50-300 kwa siku.

 

Athari za ugonjwa wa kichocho

Mwanzoni mtu aliepata maambukizi, atahisi ngozi kuwasha na kupata vipele kutokana na kimelea kuingia mwilini kupitia kwenye ngozi. Baada ya wiki 2-10 mgonjwa atahisi homa, kikohozi, kuharisha hata kukojoa mkojo kwenye damu. Mayai ya kichocho yanaweza kusafirishwa na mfumo wa damu kwenye ubongo, uti wa mgongo, via vya uzazi na kusababisha kupooza na ugumba. Minyoo wa kichocho wanaweza kuathiri ini, figo, wengu, utumbo mkubwa na kusababisha saratani, pia upungufu wa damu mwilini.

Udhibiti wa kichocho

  • Kuboresha njia za maji mashambani, kwa kujengea kingo na kusafisha kwa kuondoa majani. Hii itaruhusu maji kupita kwa kasi ambayo konokono hawezi
  • Kufanya vipimo vya afya kila wakati haswa baada ya mavuno (kwa wakulima wa umwagiliaji) na kupata tiba sahihi ya kichocho endapo kuna maambukizi
  • Kutumia vyoo bora (kutokujisaidia hovyo – mashambani, kwenye mito, mabwawa, ziwani, miferejini, vyanzo vya maji na sehemu maji yametuama kama matindiga)
  • Kufuata ushauri unaotolewa na watalaamu wa afya ya jamii

Kwa maelezo zaidi wasiliana na Lucile Lyaruu, TPRI kwa simu +255754698618

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *