- Mifugo

Ufugaji wa ndani wa kuku wa asili na banda bora la kufugia

Sambaza chapisho hili

Katika toleo lililopita tulielezea kwa undani kuhusu ufugaji wa kuku wa asili pamoja na mifumo ya ufugaji ikiwa ni mfumo huria na nusu huria. Katika toleo hili tutaangazia mfumo wa ndani na banda la kuku.

Mfumo wa ndani ni mfumo ambao kuku hujengewa banda rasmi na hufugwa wakiwa ndani huku wakipatiwa chakula na maji.  Kuku kufanyiwa huduma nyingine muhimu wakiwa humo bandani kwa muda wote wa masha yao.

Kwa mfumo huu, kuku huwekwa kwenye mabanda ambayo sakafu hufunikwa kwa matandiko ya makapi ya mringa, takataka za mbao (randa), maganda ya karanga au majani makavu yaliyo katwakatwa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Faida zake

  • Mfumo huu unahitaji eneo dogo la kufugia hivyo ni mzuri kwenye maeneo yenye uhakika wa ardhi.
  • Uangalizi wa kuku ni mzuri na rahisi na pia ni rahisi kuhakikisha ubora wa chakula.
  • Hakuna haja ya kufagia vinyesi vya kuku kila siku.
  • Kuku wanakuwa wanakingwa na hali ya hewa na maadui wengine.
  • Ni rahisi kukinga na kutibu maradhi ya kuku lakini pia uwekaji wa kumbukumbu ni rahisi.
  • Ni rahisi kudhibiti upotevu wa kuku, vifaranga na mayai.

Hasara zake

  • Uwezekano wa kuku kudonoana na kula mayai ni mkubwa kama utunzaji utakuwa duni.
  • Uwezekano wa kuku kuhatamia mayai bila mpangilio ni mkubwa.
  • Kuna gharama za ujenzi wa banda na ulishaji, pia inahitaji nguvu kazi.
  • Kuku watakosa mionzi ya jua ambayo ni muhimu sana kwa kuwapatia vitamin D.
  • Ni rahisi ugonjwa kuenea kwa haraka unapoingia kwenye kundi.

Muhimu: Kutokana na uwezo mdogo wa uzalishaji kimaumbile, kuku wa asili hawataleta tija kwa mfugaji iwapo atatumia mfumo huu.

Uboreshaji wa mfumo huu

Hakikisha utunzaji mzuri wa matandiko na usafi wa banda ili kupunguza unyevunyevu na joto kali ndani ya banda.

Kuku wawe na nafasi ya kutosha, mita moja za mraba hutosha kuku watano hadi nane.

Maandalizi ya ufugaji wa kuku wa asili

Ili kuweza kufuga kuku wa kienyeji kwa faida, ni vyema kufanya maandalizi ya awali yatakayo kuwezesha kuzalisha kuku walio bora.

Maandalizi hayo yanajumuisha utayarishaji wa banda kulingana na idadi ya kuku utakao wafuga. Uchaguzi wa kuku bora na uandaaji wa vifaa vya kulisha na kutagia, pamoja na uwiano wa kuku ndani ya banda.

Banda bora la kuku wa asili

Ni muhimu kuwajengea kuku banda bora ili wapate kujikinga na mvua, baridi, wezi na wanyama.

Banda la kuku linaweza likajengwa kando au nyuma ya nyumba ya kuishi.

Eneo la banda la kuku liwe ni eneo ambalo; Linafikika kwa urahisi, lisituamishe maji na lisiwe na mwelekeo wa upepo mkali.

Banda la kuku linaweza kujengwa kwa kutumia rasilimali za misitu zinazo patikana kwa urahisi kwenye eneo husika.

Vifaa muhimu katika ujenzi wa banda ni pamoja na miti, nyasi, mabati, makuti, fito, udongo, mabanzi, saruji na vifaa vingine mbalimbali vya ujenzi.

Sifa za banda bora la kuku

  • Liwe na paa imara lisilovuja na sakafu isiwe na nyufa au mipasuko.
  • Kuta zisiwe na nyufa kama umetumia tofali (zisilibwe au zipigwe lipu) kwani nyufa ni maficho ya wadudu kama viroboto, utitiri, chawa nk.
  • Hakikisha banda lina madirisha ya kutosha kupitisha hewa
  • Liwe na uwezo wa kuingia mtu wa kufanya usafi na huduma nyingine muhimu.
  • Banda liwe na ukubwa (nafasi) inayolingana na idadi ya wastani wa kuku 10-15 kwa mita moja mraba kwa kuku wanaofugwa huria, ili wawe na nafasi ya kulala tu wakati wa usiku.
  • Kwa kuku wanaofugwa kwa mfumo wa nusu ndani nusu nje wanastahili eneo la mita moja mraba kwa kuku 4 – 5 ili kuruhusu nafasi ya vyombo vya chakula na maji.

Kuchagua kuku wa kuendeleza kizazi

Mafanikio zaidi katika kuchagua kuku wa kuendeleza kizazi yatapatikana iwapo uchaguzi na uchambuzi wa kuku wanaozaliwa utafanywa mara kwa mara.

Ni vizuri kufanya uchaguzi ili kupata kundi la kuku litakalofaa kwa sifa zote katika uzalishaji. Sifa hizo ni pamoja na kupevuka haraka, kutaga mayai mengi, kuwa na uzito mkubwa na nyama nyingi kwa umri mdogo.

Ufugaji bora utazingatia kuchagua kuku wenye sifa nzuri na kuwaacha waendelee na uzalishaji na wanaosalia wauzwe au wachinjwe waliwe.

Sifa za kuzingatia wakati wa kuchagua mitetea

  • Wawe na umbile kubwa na wenye uwezo wa kutaga wakiwa na umri mdogo (miezi 6).
  • Wawe na uwezo wa kustahimili magonjwa na waweze kukua haraka.
  • Kuku wawe na uwezo wa kutaga mayai mengi (zaidi ya 15 kwa mtago mmoja (clutch), kuhatamia na kuangua vifaranga wengi na kuwalea.

Sifa za kuzingatia wakati wa kuchagua majogoo

  • Jogoo bora, awe na umbo kubwa, miguu imara na yenye nguvu.
  • Awe na kucha fupi, mwenye nguvu na machachari au mchangamfu.
  • Jogoo awe na upanga/kilemba kikubwa, uwezo wa kuitia chakula mitetea na tabia ya kupenda vifaranga.

 

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *