- Mifugo

Tumeamua kufanya kilimo hai kwa ajili ya afya zetu

Sambaza chapisho hili

“Kulima na kuzalisha kwa njia ya kilimo hai ni sehemu ya maisha yetu ya shuleni kwa ujumla. Tunafahamu madhara ya matumizi ya kemikali za viwandani, hivyo tumeamua kuzalisha kwa njia za asili ili kujikomboa kutokana na kemikali hizi” Mwl. Thomas Kaniki (Mkuu wa shule ya sekondari Makomu).

Mwalimu Kaniki anaeleza kuwa, kwa kufanya utunzaji wa mazingira waliweza kuanzisha uzalishaji wa mbogamboga, upandaji wa miti ya mbao, na miti ya matunda kwa njia ya kilimo hai.

Pia anasema kuwa, kuzalisha kwa misingi ya kilimo hai kunahusisha matumizi ya eneo dogo, matumizi ya mboji, biogas na mbolea ya baioslari.

Kilimo hai kilianza lini

Bw. Suleiman ambaye ndiye mwalimu msimamizi wa mazingira anasema kuwa, walifanikiwa kufanya kilimo hai baada ya kuanzisha kikundi cha malihai mwaka 2015, ambacho mpaka sasa kinahusisha wanafunzi 80 kutoka ngazi tofauti.

Hata hivyo wanafunzi wote shuleni wanajumuika pamoja katika ufanyaji wa kazi shambani.

‘’Kupitia kikundi cha malihai, tulilazimika kuzalisha mboga za majani ambazo tunazitumia hapa shuleni kwaajili ya chakula cha wanafunzi wote.  Matunda yanatumiwa na wanafunzi lakini pia mboga zinapozidi tunawapa wanafunzi wapeleke majumbani na wakati mwingine watu waliotuzunguka wanapata si mboga tu hata miche ya miti mbalimbali” alisema Suleiman.

Kwanini kilimo hai

Bw. Kaniki, mkuu wa shule anasema kikubwa ni kuzalisha chakula kilicho salama, kupunguza gharama za chakula kwa wazazi, kuhifadhi mazao kwa njia za asili bila kutumia madawa ya viwandani. Pia kutumia mazao yaliyozalishwa katika shamba la shule, kuwepo kwa mbogamboga za aina mbalimbali pamoja na kuwashugulisha wanafunzi katika miradi ambayo hata wakimaliza shule wanaweza kuendeleza majumbani kwa urahisi.

Changamoto

Mkuu wa shule anasema kuwa, kilimo hai hakina changamoto isipokuw, hali ya hewa ikibadilika ndipo kunakuwa na changamoto. Kuhusu wadudu, wanatumia dawa za asili kudhibiti hata hivyo tunaomba wadau wa kilimo hai kama Mkulima mbunifu kuendelea kutoa elimu hii ikiwezekana kwa vitendo kuongeza uelewa.

Kuhusu Mkulima Mbunifu

Bw. Alawi anasema kuwa, ni mwezi miezi saba tu umepita toka tulipoanza kupata nakala za Mkulima Mbunifu, tumehamasika hasa kuhusu mbogamboga. Kupitia jarida hili tutaendelea kuzalisha kwa wingi kwani walimu na wanafunzi wamekua wakisoma na kufuatilia makala mbalimbali zinazopatikana humo.

Pia tumehamasika na elimu ya ufugaji wa kuku, ufugaji wa sungura hivyo ni mategemeo yetu miradi mbalimbali tutaianzisha kupitia elimu inayotolewa kwenye jarida hili.

Sayuni Ulomi

“Kwa kutumia biogas tunayoihudumia sisi wanafunzi, tunapata moto wa kupikia chakula hapa shuleni, mbolea kwa ajili ya mbogamboga na kirutubishi cha mboga kinachotokana na bioslari”.

Editha Gelfi

“Tunatumia matuta ya michimbuo miwili, ambazo zinaturahisishia kupambana na magonjwa ya mbogamboga, pia kuzalisha mboga za aina mbalimbali katika eneo moja”.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *