- Mifugo, Samaki

Tahadhari za kuchukua nyakati za msimu wa mvua katika ufugaji samaki

Sambaza chapisho hili

Ufugaji wa samaki una kanuni na taratibu za kufuata ili kuendana na mabadiliko ya hali ya hewa. Msimu wa masika ni muhimu kuufuatilia ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

Katika makala hii Mkulima Mbunifu linakuangazia hatua muhimu za kuzingatia wakati wa masika ili kufanya ufugaji samaki wenye tija. Nyakati za msimu wa mvua ni vema kuzingatia hatua zifuatazo ili kuepuka madhara katika mradi wako wa ufugaji samaki;

  1. Hakikisha bwawa lina mfumo mzuri wa kutolea na kutapisha maji. Mfumo huu husaidia bwawa kutojaa maji zaidi na kupelekea samaki kutolewa nje ya bwawa na kusababisha kupungua kwa samaki bwawani hivyo kupelekea kupata hasara.

Mfumo huu hujengwa mapema kabla ya kupandikiza samaki. Sehemu ya chini kabisa huwekwa bomba kwa ajili ya kutolea maji (outlet pipe) na juu hukatwa kwa wastani wa mita moja ambapo maji huishia hapo kisha kufunikwa kwa wavu ili kuzuia samaki kutoroka.

  1. Punguza kiwango au sitisha kabisa ulishaji wa samaki hususani mvua zinaponyesha kwani hali ya joto kwenye maji hupungua na joto la mwili la samaki hushuka pia na hivyo kumfanya samaki kupoteza hamu ya kula na matone ya mvua yanapodondoka humzuia samaki kufuata chakula hicho.

Madhara ya kulisha samaki wakati mvua ikinyesha;

a) Kwa vile samaki hupunguza matumizi ya chakula, chakula hicho huoza na kuharibika na kuchafua maji na kuongeza gharama za ubadilishaji maji kabla ya wakati.

b) Ongezeko la chakula kilichooza ndani ya bwawa, hupunguza hewa safi na kuwa na ongezeko la hewa chafu ndani ya maji na kusababisha samaki kushindwa kupumua na kuwepo ongezeko la vifo vya samaki.

c) Kupunguza ulishaji nyakati za mvua hupunguza kwa kiwango kikubwa gharama za chakula ambazo zinaweza kuepukika na zikatumika baadae wakati kuna uhitaji mkubwa.

  1. Imarisha kingo za bwawa lako, hususani kwa bwawa lililojengwa kwa udongo au katika njia ya maji. Ni vema kukagua na kuimarisha kingo za bwawa ili kuzuia maji yaliyo kwenye mkondo kuingia katika bwawa la samaki.
  1. Kama tahadhari, funika bwawa lako kwa nyavu imara ili mabadiliko yoyote yale yakitokea, kama kuongezeka kwa maji ndani ya bwawa, samaki wako wabaki salama ndani ya bwawa. Jambo la msingi ni kuzingatia kanuni na taratibu za ufugaji zinazoelekezwa na wataalamu.

Kwa maelezo zaidi wasiliana na Musa Saidi wa Fish Farming Service Tanzania kwa simu namba 0718986328.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *