- Mifugo

Soko na utayarishaji wa mazao ya nguruwe

Sambaza chapisho hili

Kwa muda mrefu na katika makala tofauti, MkM imeeleza kwa undani namna nzuri ya uzalishaji wa nguruwe bora, pamoja na lishe yake na mambo kadha wa kadha yanayohusiana na nguruwe. Katika makala hii utapata kufahamu kuhusiana na soko na namna ya utayarishaji wa mazao.

Soko la mazao yatokanayo na nguruwe ni sawa na soko la mazao mengine yaliyo sokoni na linafuata mfumo wa soko huru. Uhitaji na upatikanaji wa mazao yatokanayo na nguruwe husababisha mabadiliko ya bei sokoni, hivyo kuathiri kiwango cha uzalishaji.

Ubora wa nguruwe na mazao yake (nyama na mafuta) hutegemea kwa kiasi kikubwa utunzaji wa nguruwe. Hata hivyo, ubora wa mazao hayo, huweza kuharibika kwa haraka na kusababisha hasara kwa mfugaji, endapo taratibu za utayarishaji na hifadhi ya mazao hayo hazitafuatwa.

Uuzaji wa Nguruwe

Nguruwe wanaweza kuuzwa wakiwa hai au kama nyama baada ya kuchinjwa. Uuzaji wa nguruwe hai unaweza kufanyika katika umri na uzito tofauti. Kwa Mfano, baada ya kuachishwa kunyonya, wanaokua na wakubwa.

Nguruwe wanaweza kusafirishwa kutoka eneo moja kwenda eneo jingine. Mambo ya kuzingatia wakati wa kusafirisha nguruwe ni kama yafuatayo;

  • Chombo cha kusafirishia kiwe na nafasi na kiweze kupitisha hewa ya kutosha.
  • Nguruwe wasipewe chakula saa 12 kabla ya kuwasafirisha.
  • Nguruwe wasafirishwe wakati wa jua kali, wamwagiwe maji ya baridi kabla na wakati wa kuwasafirisha.
  • Wawekewe matandazo/ matandiko, kuwe na kivuli na kusiwe na utelezi.
  • Kuta za bodi ya gari ziwe ndefu ili wasiweze kuruka.
  • Usichanganye nguruwe wakubwa na wadogo wakati wa kusafirisha.
  • Usisimamishe chombo cha usafiri njiani wakati unasafirisha nguruwe.
  • Nguruwe wasafirishwe kwa uangalifu.

Matayarisho kabla ya kuchinja

Wafugaji walio wengi, wamekuwa wakichinja nguruwe majumbani. Hii inatokana na kutokuwepo kwa mfumo rasmi wa machinjio ya nguruwe. Mchinjaji anapaswa kuzingatia utaratibu utakaomuwezesha kupata nyama bora na salama kwa ajili ya matumizi ya nyumbani au kuuza.

Mfugaji anashauriwa kumuandaa nguruwe kabla ya kumchinja kwa kufanya mambo yafuatayo;

  • Nguruwe agongwe kichwani au ashtuliwe kwa umeme, ili apoteze fahamu kidogo, kisha aning’inizwe kwa Kamba na achinjwe kichwa kikiwa kimeelekea chini.
  • Damu ikingwe kwa ajili ya matumizi mengine.
  • Nguruwe aning’inizwe kwa muda kuhakikisha damu imetoka yote.
  • Maji ya moto yatumike kuondoa manyoya kwa kukwangua na kisu.
  • Tumbo lipasuliwe ili kutoa vitu vya ndani kama vile mapafu, maini na utumbo.
  • Nyama ikaguliwe na mtaalamu wa mifugo kabla haijauzwa au kuhifadhiwa. Hii itasaidia kuhakikisha usalama wa nyama kwa mlaji.
  • Nyama isiyofaa kwa matumizi ya binadamu, ichimbiwe chini au iteketezwe kwa moto.

Kulinda ubora wa nyama

Ili nyama iweze kumfikia mlaji ikiwa katika hali ya ubora, inategemea utayarishaji  wa nyama na uhifadhi kabla ya kuuzwa.

Nyama inaweza kuuzwa mara baada ya kuchinjwa au kuhifadhiwa sehemu ya baridi kama jokofu au chumba cha baridi.

Nyama inayouzwa mara baada ya uchinjaji inashauriwa kuning’inizwa kwenye sehemu ya baridi na yenye mzunguko wa hewa ya kutosha na iliyokingwa na wadudu kama vile inzi.

Nyama ifungwe kwenye vifaa maalumu na kuwekewa maelekezo kama uzito, tarehe ya kuchinja na ya mwisho wa kutumia.

Mtayarishaji azingatie usafi na utaratibu mzuri wa kutayarisha nyama ili kulinda ubora wa nyama.

Nyama inaweza kuuzwa nzima au ikiwa katika vipande vipande kutegemeana na mahitaji ya soko. Mafuta yanaweza kutenganishwa na nyama kufuatana na mahitaji ya soko.

Usindikaji wa nyama ya nguruwe

Nyama ya nguruwe huharibika haraka hasa katika sehemu za joto, hivyo huhitaji kusindikwa na kuhifadhiwa haraka kwa kutumia njia sahihi.

Usindikaji wa nyama ya nguruwe ni muhimu kwa ajili ya kuongeza muda wa nyama kukaa bila kuharibika na kupoteza ladha na thamani ya nyama.

Nyama ya nguruwe inaweza kuhifadhiwa kwa kukaushwa kwa kutumia moshi, chumvi, jua na jokofu.

Matumizi ya njia hizo hutegemea tabia ya watumiaji, upatikanaji wa vifaa na ujuzi.

Usindikaji kwa kutumia chumvi

Usindikaji wa nyama ya nguruwe unaweza kufanyika kwa kutumia chumvi, sukari na vitu vingine kama vile Saltpetre.

Chumvi ni muhimu zaidi katika usindikaji na inatakiwa iwekwe katika kiwango kinachotakiwa ili kulinda ladha ya nyama na kutoifanya kuwa ngumu.

Sukari hutumika kuongeza ladha na ubora wa nyama na pia kupunguza ugumu unaosababishwa na chumvi. Saltpetre husaidia kulinda rangi nyekundu ya nyama na husaidia katika hifadhi na kuikausha nyama.

Mfano wa namna ya kuhifadhi nyama ya nguruwe kwa kutumia chumvi:

  • Kilo 45 za nyama, chumvi inayohitajika ni kilo 3.2
  • Sukari kiasi cha kilo 0.9 na
  • Saltpetre gramu 56.

Mchanganyiko huu unaweza kuwekwa moja kwa moja kwenye nyama au ukayeyushwa kwenye lita mbili za maji na kutumbukiza nyama.

ANGALIZO: Chumvi ya ziada itabidi ioshwe na nyama hiyo na kukaushwa kwenye moshi.

Makala hii imetayarishwa kwa ushirikiano na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dar Es Salam/Dodoma.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

1 maoni juu ya “Soko na utayarishaji wa mazao ya nguruwe

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *