- Mifugo

Punda anahitaji kutunzwa kama mifugo mingine

Sambaza chapisho hili

Punda ni mnyama anayefugwa na wengi lengo likiwa kutumika kutoa msaada wa nguvu kazi nyumbani hasa kwa kuwa njia nzuri ya kubebea mizigo.

Mnyama huyu ambaye hutumiwa hasa na kina mama na watoto wa jamii ya kimasai na nyinginezo kwa ajili ya kubebea maji, kuni, majani, kupelekea mizigo sokoni na shughuli zote zile za nyumbani amekuwa hana thamani kama waliyonayo wanyama wengine wafugwao kama ng’ombe.

Wafugaji wengi wameshindwa kuwatimizia punda mahitaji yao ya msingi kama vile malazi mazuri pamoja na lishe. Aidha, wamekuwa wakiwabebesha mizigo mara kwa mara bila kuwapumzisha na hata kuwabebesha mizigo mizito kupita uwezo wao. Kwa kufanya hivyo, ni kupoteza haki za msingi za mnyama huyu.

Misingi bora ya utunzaji wa punda.

Ili punda awe na afya na nguvu siku zote, ni lazima apate vitu vifuatavyo:

Chakula bora: Punda anatakiwa kula nyasi au pumba za mahindi, pumba za ngano, mashudu ya pamba au alizeti.

Maji: Ni lazima kuhakikisha punda anakunywa maji ya kutosha muda wote ambao hafanyi kazi.

Banda: Hakikisha punda ana banda safi na bora la kupumzikia akiwa hafanyi kazi na kulala wakati wa usiku. Banda hilo liwe limeezekwa vyema kumkinga na mvua, jua na upepo mkali.

Umri na Kazi: Usimbebeshe mizigo wala kuvuta mkokoteni punda mwenye umri  chini ya miaka mitatu.   Usimfanyishe punda kazi nzito sana na kwa punda mwenye mimba zaidi ya miezi minane au ambaye hajafikisha miezi mitatu toka kuzaa, asifanyishwe kazi yeyote.

Dawa na chanjo: Kama ilivyo kwa mifugo mingine, ni muhimu kuwasiliana na wataalamu ili punda apatiwe chanjo pamoja na kutibiwa kwa usahihi pindi anapokumbwa na magonjwa.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *