- Mifugo

Nyasi aina ya Boma ni chakula kizuri kwa ng’ombe    

Sambaza chapisho hili

Nyasi ni rahisi kukua na endapo yatatunzwa vizuri, hukuhakikishia uzalishaji wa hali ya juu wa maziwa.

Nchini Tanzania, eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya malisho, bado ni dogo ikilinganisha na umuhimu unaoweza kuwepo kwenye uzalishaji wa maziwa kutokana na kuwa na eneo la malisho. Matete na nyasi ni moja ya malisho muhimu, yanayotoa kiasi kikubwa cha malisho kwa ajili ya mifugo, yanatumika kutengeneza hay au sileji. Aina zote za nyasi ni nzuri kuliwa na mifugo kama, mbuzi na ngamia, hata katika kipindi ambacho ubora wa malisho ni mdogo.

Utunzaji mzuri wa aina hii ya malisho hukuhakikishia uzalishaji mzuri wa maziwa katika kipindi chote cha mwaka.  Shamba la malisho linaweza kuanzishwa sehemu yoyote ili mradi kuna maji ya kutosha, pamoja na mbegu zilizothibitishwa.

Aina ya nyasi iliyozoeleka ni ile inayojulikana kama Boma. Wakulima wanaweza kutengeneza shamba zuri la nyasi endapo watafuata taratibu zifuatazo katika utunzaji:

Maandalizi ya shamba

Lima shamba mvua zinapokaribia kumalizika. Hili linafaa lifanyike sehemu ambayo mazao mengine yamevunwa. Lima tena wakati wa kiangazi na upitishe reki ili kudhibiti magugu. Kwenye ardhi ambayo haijatumika, inashauriwa kulima mara 3, na kupitisha reki mara mbili ili kupata sehemu nzuri ya kitalu.

Kupanda

Kupanda mapema msimu wa mvua zinapoanza ni muhimu. Sehemu ambayo ina misimu miwili ya mvua ni vizuri kupanda wakati wa msimu mfupi wa mvua, hii itasaidia kuondokana na kazi ya palizi ya mwisho. Wakulima walio wengi hupanda moja kwa moja, wakati nyasi aina ya Boma ikipandwa peke yake. Mbegu hupandwa zenyewe katika kitalu, sehemu ambayo haina magugu. Inashauriwa kupanda kwenye eneo ambalo limelimwa mara mbili kwa mwaka au zaidi. Inashauriwa kupanda mbegu kwenye tabaka la juu la ardhi ili iwe rahisi kupata unyevu na kuota kwa haraka.

Mbegu za nyasi lazima zipandwe juu juu kwa kuwa zinaweza kuwa dhahifu kusukuma udongo mzito ili kuota. Mbegu zinaweza kupandwa kwa kusambazwa au kupandwa kwa kuchimbiwa kwenye mistari yenye upana wa sentimita 20-30 kila mstari. Changanya mbegu na unga wa mbao, au mchanga wakati wa kupanda hata kama unapandwa kwa kutawanya. Endapo mbegu zitachanganywa na mbolea za viwandani ni lazima zipandwe mara moja ili kuepuka mbegu kuungua.

Wakulima wadogo wanaweza kupanda kwa mikono kwa uangalifu. Kwa wakulima wakubwa wanaweza kupanda kwa kutumia mashine ya kupandia ng’ano. Mara tu baada ya kupanda, inashauriwa kushindilia ili iwe rahisi kwa mbegu hizo kugusana vizuri na udongo, ili kuharakisha kuota. Hii inaweza kufanyika kwa kutumia kipande cha mti au kushindilia kwa miguu hasa sehemu ambayo shamba ni ndogo.

Matumizi ya mbolea

Tumia mbolea inayotokana na mifugo kiasi cha tani 10 kwa ekari moja (wastani wa tani 5 kwa hekari). Mbolea ni lazima isambazwe na kutifuliwa ardhini kabla ya kupanda. Tumia mbolea iliyo oza vizuri peke yake.

Udhibiti wa magugu

Magugu yanaweza kupunguza majani ya malisho, hasa sehemu ambapo yanapandwa kwa mwaka wa kwanza. Dhibiti magugu iwezekanavyo, kwa kupalilia kwa mikono au kwa kufyeka.

Utunzaji wa machungo

Wakati wa mwanzo nyasi aina ya Boma huchanua katika kipindi cha miezi 3 mpaka 4 toka kupandwa. Katika kipindi hiki, mizizi haijajishika vizuri kwenye udongo.  Wakati huu inashauriwa kukata majani na kutengeneza hay kuliko kuchungia wanyama ili kuepuka wasiyang’oe. Chungia au kata majani katika kipindi cha wiki 4 mpaka 6, yakiwa na urefu wa sentimita 5.

Kulisha

Ng’ombe mmoja anahitaji ekari 1 mpaka 2 za majani ya Boma kwa mwaka, kwenye eneo lenye wastani wa milimita 900 za mvua. Kwa ufugaji wa ndani, ng’ombe mwenye uzito wa kadri anahitaji kati ya kilo 80-100 za majani mabichi kwa siku.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

4 maoni juu ya “Nyasi aina ya Boma ni chakula kizuri kwa ng’ombe    

    1. Habari,

      Kwasas hatuna mtu wa uhakika anayeuza ama kampuni lakini tukifanikiwa kupta tutakujulisha. Karibu Mkulima Mbunifu

    1. Habari,
      Karibu Mkulima Mbunifu na tunashukuru kwa kuendelea kuwa mfuatiliaji na msomaji wa makala zetu kwa njia ya mtandao. Kuhusu majani haya wasiliana na Charles Bonaventure kutika ECHO Arusha kwa simu namba 0754 992 079

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *