- Mifugo

Ni muhimu kutambua minyoo inayoshambulia mazao

Sambaza chapisho hili

Mara nyingi tumekuwa tukizungumza kuhusu wadudu rafiki na halikadhalika kuweka wazi kuhusu wadudu wanaoshambulia mazao. Katika toleo hili tutajifunza kuhusu minyoo inayoshambulia mazao.

Ipo minyoo ya aina nyingi ambayo inafaida katika urutubishaji wa udongo na mingine ambayo ina madhara kwa mimea, wanyama pamoja na binadamu.

Minyoo hutofautiana kwa ukubwa wa maumbile, mfano ipo inayoonekana kwa macho ya kawaida na ile midogo ambayo huonekana kwa msaada wa darubini.

Minyoo inayoshambulia mazao

Minyoo aina zote ipo katika kundi la wanyama wasio na uti wa mgongo. Inaweza kugawanywa katika vipande viwili vinavyofanana.

Maumbo yao hayajagawanyika pingilipingili (unsegmented). Minyoo inayoshambulia mazao au mimea ni midogo sana, haina rangi ya uhalisia (colourless) na huishi ndani ya udongo.

Aina za minyoo inayoshambulia mazao

Kufuatana na aina na dalili za dhahiri za uharibifu, minyoo hii tunaweza kuigawa katika makundi mawili.

Kundi la kwanza ni minyoo inayovamia mimea na kuingia ndani ya mmea na kuishi na kula ndani ya sehemu ya mmea mfano ndani ya mizizi. Aina hii huitwa “Endoparasitic Nematodes”.

Aina ya pili ni ile inayoishi kwenye udongo au sehemu ya nje ya mmea na hushambulia mmea ikiwa nje ya mmea “Exoparasitic Nematodes”.

Umuhimu wa kutambua minyoo

  1. Minyoo inayoshambulia mazao ipo mingi katika nchi yetu.
  2. Minyoo hushambulia mazao aina nyingi sana.
  • Mazao haya hushambuliwa sehemu mbalimbali kuanzia kwenye mizizi, majani hadi matawi.
  1. Ni vigumu kuzuia kwa kutumia njia moja.
  2. Vidonda vinavyosababishwa na minyoo hii huwa ni njia rahisi ya maambukizi mengine ya magonjwa ya mimea (bakteria, fangasi na virusi).
  3. Dalili za mashambulizi hufanana na magonjwa mengine.
  • Wakulima wachache ndio wenye ufahamu wa minyoo hii.

Mazao yanayoshambuliwa na minyoo

  • Mazao ya mboga – nyanya, pilipili hoho, ngogwe, mnavu, swisschard, bilinganya, lettuce, karoti, maboga, viazi mviringo, kabichi n.k
  • Mazao ya matunda – migomba, michungwa, michenza, madalansi, matikiti
  • Mazao mengine – tumbaku, miwa, ngano, viazi vitamu, viazi mviringo, mahindi.

Muhimu

Ni muhimu pia kutambua magugu mengi hushambuliwa na minyoo hivyo magugu yanahifadhi minyoo.

Usambaaji wa minyoo ya mazao

  1. Maji: Maji ya kumwagilia hubeba minyoo hii kutoka shamba lililoathirika sana na kuipeleka katika shamba lisiloathirika.
  2. Vipando: Miche iking’olewa na kuchukuliwa kutoka sehemu iliyoathirika hubeba minyoo hii katika udongo au miche yenyewe hadi sehemu isiyo na maambukizi.
  • Vifaa vya kufanyia kazi shambani kama majembe, reki, sururu, mabeleshi pia husambaza minyoo ya mazao.
  1. Mavazi: Viatu vya mvua au mabuti hubeba udongo pamoja na minyoo hadi shamba lisiloathirika na kuliambukiza.
  2. Trekta na zana zake za kulimia na palizi nayo pia husambaza minyoo ya mazao.
  3. Udongo wa kwenye viriba kama usipotibiwa vizuri husambaza minyoo kwa kiasi kikubwa.
  • Baadhi ya minyoo hii inaweza kuatambaa kwa kiasi kidigo (migratory nematodes) hadi kuifikia mizizi ya mimea.

 

Dalili za uharibifu wa minyoo ya mazao

Sehemu ya juu ya mmea

  1. Majani hubadilika rangi na kuwa ya njano
  2. Mmea hudumaa kwa sababu mizizi imeharibiwa na minyoo
  3. Mavuno huwa kidogo sana na yasiyo na ubora unaotakiwa
  4. Mmea huzeeka mapema kabla ya wakati wake kufika (early senescence)
  5. Mimea yenye matunda hudondosha yakiwa bado machanga
  6. Majani hujisokota na ncha zake huwa nyeupe au njano
  7. Vidonda vyenye rangi ya njano huonekana katika majani na mashina ya miche michanga.

Katika mizizi ya mmea

  1. Uvimbe katika mizizi (large galls). Husababishwa na aina ya minyoo fundo (root knot nematodes).
  2. Mizizi inakuwa michache katika mmea.
  3. Mizizi huwa katika hali isiyo ya kawaida.
  4. Mizizi huwa na muonekano wa vishungi vifupi vifupi.
  5. Vidonda vidonda huonekana kwenye mizizi michanga.
  6. Mimea huanguka kirahisi maana mizizi imeshambuliwa sana.

Muhimu

  • Baadhi ya minyoo hii huhitaji uchunguzi wa kimaabara na kitaalamu zaidi.
  • Minyoo fundo ni rahisi kuitambua kwa kuangalia vijiuvimbe katika mizizi.
  • Dalili nyingine hufanana na baadhi ya magonjwa ya mimea ya virusi, bakteria naya hali ya hewa na ukosefu wa virutubisho vya mmea.

Mbinu zinazotumika kudhibiti minyoo.

  1. Kwa kutumia mimea mitego kama marejea au aina ya maua yanayoitwa mabangi bangi (Tagetus erecta au Tagetus minuta) mimea hii huoteshwa sehemu iliyoathiriwa sana na minyoo.
  2. Palizi ya shamba ni muhimu, shamba liwesafi wakati wote wa msimu wa mazao (clean weeding)
  • Zana zinazotumika shambani ni vizuri zifanyiwe usafi mara tu kazi ya shamba inapoisha na kuhifadhiwa vizuri.
  1. Panda au otesha mbegu kinzani ya minyoo (resistant varieties)
  2. Sehemu ya kitalu udongo utibiwe kwa mvuke (steaming), kwa kuchoma moto au kutumia mwanga wa jua (solarization)
  3. Masalia ya mazao ya ng’olewe na kuchomwa moto sehemu maalumu iliyotengwa.
  • Kutumia vijidudu vingine vinavyo wadhuru minyoo hawa (vijidudu kama Bacillus thurigiensis)
  • Fuata mzunguko wa mazao kwa kupanda mazao ambayo haya shambuliwi na minyoo.
  1. Miche inayoanza kushambuliwa isihamishiwe shambani
  2. Tumia mbolea za asili – samadi na mboji kwa wingi ili mazao yawe na afya nzuri
  3. Tumia viuatilifu vilivyo pendekezwa na wataalam wa kilimo (Nematicides)
  • Pata ushauri wa maafisa ugani walio karibu na wewe.

Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana nasi au mtaalamu wa kilimo, Suleiman Mpingama +255 685 460 300.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *