- Mifugo

Nguruwe wanahitaji kupata chakula chenye virutubisho sahihi

Sambaza chapisho hili

Nguruwe huhitaji kulishwa vizuri ili waweze kukua haraka na kufikia uzito wa kuchinjwa mapema. Ikiwa watatunzwa vizuri watafikia uzito wa kilo 60 hadi 90 wakiwa na umri wa miezi sita hadi tisa.

Nguruwe wakila chakula chenye mchanganyiko wa makundi yote muhimu

Nguruwe ana uwezo wa kula vyakula vya aina mbali mbali ikiwa ni pamoja na mabaki ya vyakula vya nyumbani, shambani na viwandani.

Pamoja na vyakula hivyo, ni muhimu kumlisha chakula cha kutosha, bora na chenye viinilishe vyote vinavyohitajika mwilini. Hata hivyo ili kupunguza gharama mkulima anashauriwa kumlisha vyakula vinavyopatikana katika mazingira yake.

Mfugaji anaweza kuchanganya chakula mwenyewe au kununua kutoka kwenye maduka yanayouza vyakula vya mifugo. Mchanganyiko huo uwe na makundi muhimu ya vyakula kwa ajili ya nguruwe.

Makundi ya Vyakula Kuna makundi makuu matatu ya vyakula ambavyo ni;

Vyakula vya kujenga mwili

Hivi vinahitajika mwilini kwa ajili ya kuimarisha misuli na kujenga mwili kwa mfano maharage, soya, mashudu ya pamba, alizeti, ufuta na nazi. Vyakula vitokanavyo na wanyama kama mabaki ya nyama, damu, dagaa au samaki na maziwa yaliyokaushwa.

Vyakula vya kutia nguvu na joto

Vyakula vya nafaka kama vile ulezi, ngano, mahindi, mpunga, pumba na mabaki ya vyakula mbali mbali kama mikate, viazi, mihogo na machicha ya pombe.

Vyakula vya kulinda mwili (madini na vitamini)

Kundi hili linajumuisha madini kama mifupa iliyosagwa, chokaa, unga wa maganda ya mayai, chumvi na vitamini kama majani mabichi, mchicha, maboga na matunda.

Maji

Pamoja na kupewa chakula, maji safi na ya kutosha ni muhimu ili chakula kiweze kutumika vizuri mwilini. Nguruwe anahitaji maji wakati wote.

Mahitaji kwa ajili ya kutengeneza chakula cha nguruwe;

  • Chumvi paketi tatu (3)
  • Pumba ya mchele kilo 110
  • Unga wa soya kilo 16.5
  • Mashudu kilo 11
  • Karboni gramu 3.3 (ina Kalsiamu, inasaidia mmengenyo wa chakula na kuondoa gesi)
  • Molasis mililita 440 (ina kinga magonjwa na kuzuia harufu mbaya)
  • Maji lita 46.5
  • Molasis mililita 440
  • EMAS – (Effective Micro-organisms) mililita 440
  • FFJ- (Fermented Fruit Juice) au
  • FAA- (Fish Amino Acid) lita 3, hii ina omega 3.

Jinsi ya kufanya

Changanya vizuri mahitaji tajwa na hifadhi mahali pakavu kwenye mfuko tayari kwa matumizi ya nguruwe.

Muhimu:

Hakikisha unazingatia uwiano sahihi wa chakula kwa kila hatua ya ukuaji wa nguruwe.

Aina ya chakula

Hakikisha nguruwe wanapata chakula chenye wanga (65%-75%,) protini(17% – 20%), madini (2% – 3%), vitamini na chumvi(0.5% – 1%).

Kwa maelezo zaidi kuhusiana na makala hii wasiliana nasi au Mr. Martini Mhando, wa shamba la kilimo hai ST. Joseph Mwanga, Kilimanjaro, kwa simu namba +255 (0)762675234

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

7 maoni juu ya “Nguruwe wanahitaji kupata chakula chenye virutubisho sahihi

  1. Hongereni sana kwa elimu hii muhimu, sijui ni kwa kiasi gani inawafikia wakulima wa wadogo. Mkiweza kuongeza video za kuonyesha jinsi ya kupima na kuchanganya vyakula vya mifugo n.k . itapendeza zaidi. Pia kwenye makala ya nguruwe sijaona maelezo kuhusu kiwango cha kulisha kwa hatua tofauti.

    1. Ndio. Unaweza kutumia mihogo kulisha nguruwe.

      Sileji inatengenezwa kutokana na matawi ya mhogo yaliyokatwakatwa na kuchanganywa na kiasi kidogo ya mizizi iliyosagwa. Mchanganyiko huu unawekwa kwenye kwenye chombo kisichoruhusu hewa kuingia ama inafukiwa kwa muda wa siku tisini (miezi tatu), hadi inachacha. Inakuwa tayari kulishwa nguruwe. Chakula cha nguruwe chenye kumi na tano (15%) ya sileji ya mihogo inaweza kutumika.

      Kutengeneza sileji ya mihogo inasaidia kupunguza kemikali ya hydrocyanic acid ambayo ina madhara kwa mifugo. Kemikali hii huwa juu wakati mihogo ni mbichi. Ili kuipunguza saga mizizi, weka chachu, na kukausha.

      Kumbuka, mihogo ina protini kidogo sana, kwa hivyo, chanzo kizuri cha protini kinahitajika. Unaweza kuchanganya na soya au dagaa iliyosiagwa.

      Utumbo wa nguruwe una bakteria ambao husaidia kusaga na kutumia virutubisho vilivyomo kenye mihogo.

    1. Ulishaji wa nguruwe huongezeka kulingana na ukuaji wake (umri). Uwiano huu ambao hutokana na mchanganyiko wa vyakula vyote kwa kiwango (madini,wanga,protini na vitamini) hutakiwa kupewa nguruwe mara mbili kwa siku.

      Mfano, Wiki 8 hadi 12 anakula kg 1, Wiki 12 hadi 18 anakula kg 1.5, Wiki 18 hadi 23 anakula kg 2.0, Wiki 23 hadi 30 anakula kg 3.0

      Kiwango hichi i kwa siku na unakigawa mara mbili kwa siku, asubuhi na jioni

    1. Ndiyo lakini yawe safi na salama wala hayajaoza. Ni muhimukuhakikisha unachambua ili kutoa vitu vigumu ama venye kuumiza kaa vile mifupa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *