- Mifugo

Namna ya kuandaa udongo kwa ajili ya kusia mbegu

Sambaza chapisho hili

Wakulima wengi hawaelewi ubora na umuhimu wa kuandaa udongo maalumu kwa ajili ya kusia mbegu za mazao mbalimbali kabla ya kuzipeleka shambani hasa mazao ya bustani.

Si kila udongo unafaa kwa ajili ya kusia mbegu. Kuna udongo maalumu unaostahili kutumika kwa ajili ya kusia miche, ambao mkulima yeyote anaweza kuutafuta na kuandaa mwenyewe kwa ajili ya matumizi hayo.

Bila kutumia udongo ulioandaliwa vizuri na maalumu kwa ajili ya kusia miche, ubora wa miche tarajiwa pamoja na uotaji unakuwa hafifu na hata miche ikipelekwa shambani, itakuwa imepoteza ubora wake na uzalishaji wa mazao utakuwa wa kiwango cha chini.

 

Huu ni udongo wa aina gani

Udongo mzuri ambao unafaa kwa ajili ya kusia miche na unapatikana kwa urahisi ni kutoka msituni au kutoka chini ya miti mikubwa, ambao umetokana na mazalia ya majani na vijiti vilivyo oza na kuwa odongo, ikiwemo vinyesi vya ndege.

Kwa maana hiyo, mkulima anapokuwa tayari kusia mbegu, ni lazima ahakikishe anatafuta udongo wa aina hii mahali unapopatikana tayari kwa ajili ya kusia mbegu.

Namna ya kuandaa udongo

Pamoja na kuwa udongo huu una ubora unaostahili kwa ajili ya kusia mbegu, lakini kuna namna inatakiwa uandaliwe ili kuua baadhi ya vijidudu ambavyo huenda vikawa na madhara kwa mbegu au miche, lakini pia kuufanya udongo uwe na ubora zaidi.

Vifaa na vitu vinavyohitajika kwa ajili ya kuandaa

Mchanga mwekundu, mfuko wa sulfate, sufuria au pipa, maji, ndoo/debe la lita ishirini (kwa ajili ya kupimia), jiko na beleshi/shepe.

Hatua za kuuandaa ni kama zifuatazo;

  • Pima udongo kiasi cha debe moja na pima mchanga mwekundu kiasi cha beleshi moja
  • Changanya vizuri udongo na mchanga huku ukiondoa takataka ngumu kama vile miti na mawe ikiwa udongo wako una taka hizo
  • Udongo ukishachanganyika vizuri, na taka zote ngumu zikiwa zimetoka, weka kwenye mfuko wa sulfate na funga vizuri
  • Chukua sufuria kubwa au pipa kisha jaza maji na injika jikoni, na uchemshe vizuri mpaka yaanze kufoka.
  • Maji yakiwa tayari, gawa nusu ili kuwepo na nafasi ya kuweza kutumbukiza mfuko bila maji kumwagika
  • Chukua udongo uliouandaa na tumbukiza kwenye maji yaliyoko kwenye sufuria au pipa kwa kusimamisha mdomo wa mfuko ukiangalia juu, na fungua mfuko huo huku ukishikilia udongo usimwagikie kwenye maji
  • Chukua yale maji uliyoyagawa, na anza kutilia kwenye mfuko taratibu huku ukihakikisha hayajai kwenye sufuria au pipa na kuanza kumwagika
  • Ukiona maji yamefika juu kabisa mwa sufuria, acha na funga mfuko wa udongo vizuri ukiwa bado kwenye pipa/sufuria kisha weka sufuria hiyo sehemu patulivu penye kivuli na cha kwa siku mbili hadi tatu mpaka utakapoona udongo umenyonya maji yote
  • Baada ya siku ya tatu, chukua na fungua mfuko kuangalia kama udongo bado una tope sana, na kama umekauka maji lakini kuna kaubichi kidogo, basi udongo wako uko tayari kwa ajili ya kutumia kusia mbegu
  • Udongo huo unaweza kutumika siku yeyote ama ata ukahifadhiwa kwa ajili ya matumizi ya baadaye maadamu tayari umeshatengenezwa kwa hatua hizo.

Namna bora ya kusia mbegu kwa kutumia udongo huu

Ili udongo huu uweze kuonyesha ubora zaidi katika usiaji wa mbegu na ukuzaji wa miche, mkulima hana budi kutumia trei maalumu zinazotumika kwa ajili ya kukuzia miche.

Trei za kukuzia miche ziko za aina nyingi na zimetofautia kulingana na idadi ya matundu ama idadi ya miche inayoweza kuchukuliwa na trei hiyo.

Namna ya kuandaa trei kwa ajili ya kutumia kusia mbegu

Vifaa

Maji, trei zenyewe, sabuni ya unga.

Hatua

Weka maji katika chombo kikubwa chenye uwezo wa kutumbukiza trei kama vile beseni kubwa, kisha changanya na sabuni ya unga kiasi kidogo.

Chukua trei zote unazotegemea kuzitumia kusia mbegu, moja baada ya nyingine na kisha tumbukiza kwenye maji hayo, huku ukihakikisha trei lote na tundu zote zinapata maji kisha toa na weka pembeni.

Kutumbukiza trei kwenye maji yenye sabuni husaidia kuua vimelea ambavyo si rafiki kwa mbegu au miche.

Namna ya kuweka udongo kwenye trei

Chukua turubai au mfuko kubwa wa nailoni na tandaza, kisha mimina udongo wako uliouandaa kwenye upande mmoja wa turubai na anza kujaza udongo kwenye matundu ya kila trei.

Hakikisha unapoweka udongo kwenye trei, udongo huo unajaa kwenye kila tundu lakini bila kushindiliwa kwani ukishindilia utakuwa mgumu, na itakuwa kazi kupandikiza mbegu na hata kupitisha maji wakati wa kumwagilia mbegu hizo au miche yako hapo baadaye.

Picha kuweka udongo kwenye turubai

 

Namna ya kusia mbegu kwenye trei

Kila baada ya kujaza udongo katika trei moja, weka punje za mbegu kwenye kila tundu la trei, na tumia kijiti chembamba kiasi kusukumiza mbegu kuzama kwenye udongo ndani ya tundu lakini mbegu isizame sana, wala isifike katikati ya tundu bali juu kiasi na iwe imefunikwa na udongo.

Fanya hivyo kwa trei zote mpaka utakapomaliza kusia mbegu zako, tayari kwa ajili ya kukuza miche.

 

Picha kuonyesha namna ya uwekaji wa mbegu na kutumia kijiti

 

Eneo la kukuzia mbegu kwa siku mbili hadi saba

Andaa kichanja kitakachotosheleza kuweka na kupanga trei zote zenye mbegu mahali penye kivuli. Unaweza hata kuweka ndani chini ya uvungu, lakini kuwe ni sehemu penye utulivu na giza.

Kama ni nje, chukua nailoni nyeusi kisha tandaza juu ya kichanja na panga trei zote juu. (Hakikisha kabla ya kupanga trei juu ya kichanja, umenyunyizia maji kidogo kulowanisha udongo kwa kutumia bomba la kupiga dawa au spray pump)

Kama trei ni nyingi, weka trei kwa kupandanisha juu ya zingine, huku ukipishanisha kuhakikisha hakuna trei inayokaa juu ya nyingine kwa mwelekeo mmoja kwani vitobo vikipandana mbegu itashindwa kuota kwa kukosa sehemu ya kutokea.

Baada ya kupanga trei zote, chukua nailoni nyingine nyeusi kisha funika trei zote vizuri tayari kwa kusubiri mbegu ichipue.

Nini cha kufanya baada ya kufunika mbegu

Katika siku ya pili jioni, anza kuangalia mbegu kama imeanza kuchipua kwani kuna baadhi ya mbegu huchipua haraka sana.

Fanya hivyo kila siku asubuhi na jioni. Ukishaona mbegu moja tu imejitokeza, ondoa nailoni na hamishia trei zote kupeleka kwenye eneo la kukuzia miche.

Eneo la kukuzia miche likoje

Eneo la kukuzia miche linatakiwa liwe ni kichanja ambacho kwa chini hakijazibwa bali kina viupenyo. Unaweza kutumia miti migumu kama nguzo (lakini zisiwe zile za kuliwa sana mchwa) na ukapigia mianzi kutengeneza kichanja.

Weka pia miti kidogo kwa juu kwa kuzikunja kutoa upande wa kuchoto kwenda kulia ili ikusaidie kufunika kwa kuweka nailoni juu ya miche yako hasa kipindi cha mvua kubwa kwani mvua huweza kufanya miche kuvunjika na hata udongo kudondoka kwenye matundu na mwisho miche kufa.

Nini cha kufanya kwenye kichanja cha kukuzia miche

Baada ya mbegu kuanza kuchomoza, hamisha na panga trei zako zote kwenye eno la kukuzia miche kisha anza kunyunyizia mji kwa kutumia spray pump kila siku mchana. (Usinyunyizie maji asubuhi wala jioni ili kukwepa barafu na pia kushamirisha kuwepo kwa wadudu).

Hakikisha wakati wa kunyunyiza maji, huruhusu kuingia maji mengi kwani kutafnya udongo kupotea kwa kudondoshwa na maji kidogo kidogo na mwisho udongo wote kuisha na hatimaye mbegu kunyauka na kufa.

Mara unapoona kuna magugu yanajitokeza, ondoa mapema yakiwa bado madogo sana kwasababu zikikomaa ni ngumu kuondoa.

Endelea kutunza bustani yako kwa muda ambao utaona miche iko tayari kupelekwa shambani, kulingana na aina ya zao ulilosia.

Faida ya kusia kwa kutumia trei

  • Njia hii ni rahisi sana kwa mkulima kutunza miche yake bila usumbufu .
  • Miche inayokuzwa kwenye trei, mara ni vigumu sana kushambuliwa na wadudu pamoja na magonjwa kutokana na kuwa udongo uliotumika umetibiwa wakati wa ule ulipowekewa maji yaliyochemka.
  • Mkulima anakuwa na uhakika wa kiasi cha miche ama idadi ya miche aliyonayo kwa ajili ya kupeleka shambani kwake. Hii ni kutokana na kuwa kila trei linakuwa na matundu idadi fulani.
  • Miche inayokuzwa kwenye trei haiwezi kufa na kila mbegu huota ilimradi tu mbegu iliyowekwa.
  • Miche inayokuzwa kwenye trei, hushika chini haraka na kukua kwa haraka sana shambani kwani wakati wa kuhamisha, mizizi haikatwi na miche huhamishwa au kuoteshwa pamoja na udongo wake wa kutoka kitaluni.
  • Halikadhalika, miche inayokuzwa kwenye trei, mara nyingi haishambuliwi na magonjwa na wadudu kwa haraka baada ya kuhamishiwa shambani kwani kupitia kwenye udongo ule huwa na ukinzani mzuri.

Mimea inayoweza kusiwa kwenye trei

Si mimea yote yanayoweza kusiwa kwenye trei, isipokuwa ni baadhi ya mazao ya bustani kama vile nyanya, pilipili hoho, kabichi, matango, matango.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *