- Binadamu, Kilimo, Kilimo Biashara, Kutuhusu, Mazingira, Mifugo, Mimea, Redio, Usindikaji

Miaka 10 ya huduma kwa wakulima wadogo

Sambaza chapisho hili

Maoni kutoka kwa wakulima yanaonyesha kuwa wakulima wadogo wana hamu ya kujifunza njia mpya na endelevu za kilimo ambazo zinaboresha mapato yao. Inaonyesha kwamba wanatambua na kuthamini mchango wa MkM katika kuendeleza na kupanua kilimo biashara na kutunza mazingira.

Tangu kuanzishwa kwa jarida hili mnamo Julai 2011, Mkulima Mbunifu, maarufu kwa wakulima kama MkM limejikita katika kuwaelimisha wakulima kuthamini msingi wa maliasili waliyonayo na kuweka kipaumbele usalama wa chakula na lishe kwa kutumia mbinu za kilimo endelevu.

Kwa muda huo MkM imepanua shughuli zake na kuwafikia wakulima wengi katika sehemu mbalimbali nchini, kutumia jarida (kutoka majarida 5,000 kila mwezi mwaka wa 2011 hadi majarida 15,000 kila mwezi wakati huu), redio, tovuti na mitandao ya kijamii. Hata hivyo, hatujawafikia wakulima wote na bado kuna uhitaji mkubwa.

Muamko wa wakulima

MkM imeandika mara kadhaa juu ya changamoto nyingi ambazo wakulima wadogo wanakabiliana nazo, kama bei ya chini ya bidhaa za kilimo, miundombinu mibovu, ukosefu wa umeme vijijini na vifaa vya mafunzo na kadhalika. Ingawa hatuwezi kufanya mengi tunafurahi kutambua kuwa, wakulima wadogo wanaamka na kupigania haki zao.

Vikundi vya wakulima ambavyo vinasoma jarida la MkM sasa viko tayari kushughulikia changamoto na kuboresha maisha yao. Wengine wamekusanyika pamoja na kuunda vikundi vya uuzaji na hata kutengeneza pembejeo kama chakula cha kuku.

Bado MkM litaendelea kuwapa wakulima wadogo sauti na jukwaa la kuelezea mahitaji yao, kutoa habari muhimu juu ya ufugaji wa wanyama na uzalishaji wa mazao kwa mbinu endelevu.

Tunatoa shukrani kwa washirika wetu Sustainable Agriculture Tanzania (SAT), Biovision Africa Trust (BvAT), na Biovision Foundation kwa kuwezesha ufanisi huu kwa wakulima wa Tanzania. Tuendelee kuchapa kazi!

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *