- Mifugo

Mfugaji anaweza kuongeza pato kwa kufuga bata

Sambaza chapisho hili

Wafugaji wengi wa ndege wamekuwa wakikazana zaidi namna ya kufuga aina mbalimbali za ndege bila kujumisha bata. Aina hii ya ndege wanaweza pia kuwa chanzo kizuri cha kuongeza pato.

Wafugaji wengi wadogo wa bata nchini Tanzania hufuga bata chotara ambao wamechanganyika na aina mbalimbali za jamii ya bata. Aina nyingine inaweza kuwa bata bukini, bata maji, au bata mzinga.

Matumizi makubwa ya bata hawa ni kwa ajili ya kupata nyama, japokuwa huweza kutumika kwa ajili ya kupata mayai na pia kwa ajili ya mapambo nyumbani na kwenye sehemu za biashara kama vile bustani za mapumziko au hoteli.

Aina za bata

Aina maarufu ya bata wa nyama ambao pia hufugwa kwa wingi kibiashara ni Pekin. Asili ya bata hawa ni kutoka bara la Asia hasa China.

Unaweza kuwatambua bata hawa kwa rangi ambayo ni nyeupe. Aina hii ya bata wana sifa zifuatazo:

  • Pekin hukua haraka na wana umbo refu.
  • Wana vidari vilivyojaa na ngozi zao ni rangi ya njano.
  • Vichwa na miguu ya bata hawa huwa na nyekundu iliyochanganyika na njano.
  • Dume wa Pekin huwa na wastani wa kilo 4.5 na majike kilo 4 wakiwa hai.

Banda

Kama ilivyo kwa aina nyingine ya mifugo, bata pia wanahitajika kuwa na banda zuri kwa ajili ya kujisitiri na usalama wao. Mfugaji anaweza kutengeneza banda kulingana na mazingira yake, mahitaji na malighafi zinazopatikana.

  • Paa la banda linaweza kuwa la nyasi, makuti, vigae au bati mradi mvua, joto, na baridi kali visiruhusiwe kuwepo ndani.
  • Kuta zaweza kujengwa kwa kutumia miti, udongo, mbao, matofali au bati.
  • Sakafu inaweza kuwa ya saruji, zege au udongo.
  • Unaweza kuweka matandazo ya pumba ya mbao au maranda.
  • Unaweza kutengeneza sakafu ya nyavu za chuma au fito kama kichanja.
  • Banda liwe kavu na mwanga wa kutosha.
  • Banda liruhusu mzunguko wa hewa vizuri.
  • Kipimo kiwe ukubwa wa kuweka bata wakubwa watatu katika mita moja ya mraba.
  • Bata wanaokua wasizidi 6 wenye umri wa wiki 4 katika eneo la ukubwa huo huo.
  • Ni vizuri kuwa na kibwawa kwenye eneo la kufugia, ili kuwa na maji safi ya kutosha maana huongeza urutubishaji wa mayai, pia huongeza
    mazingira ya unyevunyevu unaohitajika kwa uhatamiaji wa mayai yao.

Uzalishaji

  • Majike ya bata yachaguliwe kutoka kwenye majike mama yenye uwezo wa kutaga mayai mengi, kuhatamia vizuri na kutotoa vifaranga wengi (15 hadi 20).
  • Madume yawe na uwezo wa kupanda yakiwa na umri wa miezi 6 na majike nayo huanza kutaga yakiwa katika umri huo huo.
  • Inashauriwa madume na majike ya ukoo mmoja katika upandishaji ili kuondoa kurithishwa kwa sifa mbaya katika kizazi kijacho. Kwa mfano, uwezo mdogo katika utagaji, uanguaji wa mayai, ukuaji hafifu, kushambuliwa kirahisi na magonjwa na kadhalika.
  • Dume moja la bata lina uwezo wa kupanda/kurutubisha majike 4 hadi 6.
  • Inashauriwa dume na majike wakae pamoja kipindi cha mwezi mmoja au zaidi kabla ya majike kutaga. Hii inasaidia mayai kupata muda wa kutosha wa kurutubishwa kabla ya kutagwa.
  • Majike yana uwezo wa kutaga, kuhatamia na kuangua vifaranga 15 hadi 20.
  • Uhatamiaji huchukua siku 28. Bata aina ya Muscovy kutoka Amerika ya Kusini wao uhatamia kwa muda wa siku 35.

Unaweza kmtumia kuku

Kuku pia anaweza kuhatamia na kuangua mayai ya bata. Ili hilo liwezekane, hakikisha ana mayai machache maana mayai ya bata ni makubwa kuliko ya kuku (mayai yasizidi 8).

Kwa kuwa kuku hana tabia ya kuoga mara kwa mara kama bata, inampasa mfugaji kuyawekea mayai ya bata unyevunyevu kila siku ili kuboresha joto na unyevunyevu unaohitajika katika uhatamiaji.

Unaweza kupata vifaranga vya bata na kuku kwa kuanza kumuhatamisha kuku mayai ya bata kwa muda wa siku saba, kisha inapofika siku ya nane unamwongezea mayai ya kuku ambapo inapofika siku ya 38 vifaranga vya bata na kuku vitaanguliwa.

Lishe ya bata

Lishe ya bata ni sawa na inayotumika kwa ajili ya kuku au bata mzinga.

Mahitaji ya vifaranga wa bata na vya kuku wa mayai pia hufanana. Vifaranga wa bata wapewe Chick au Duck mash katika wiki 3 za mwanzo na Growers mash kuanzia wiki ya nne mpaka umri wa kuanza kutaga.

Ni muhimu pia bata kupata mimea ya kijani, na ya jamii ya mikunde pia. Chakula bora cha ziada kwa bata wa umri wote ambayo huwapatia vitamini, protini na madini kwa ajili ya kulinda mwili vinahitajika wakati wote. Majani yanaweza kufidia asilimia 40 ya chakula.

Bata hasa vifaranga hupenda kula chakula chenye hali ya unyevunyevu au majimaji.

Bata wakubwa wana uwezo wa kula punje za nafaka kama kunde au mbegu za mafuta ambavyo huwapatia nguvu, joto na kujenga miili yao.

Punje za nafaka zinaweza kupondwapondwa na kuwa chenga ambazo bata wanaokua wanaweza kula kutokana na ukubwa wa midomo yao.

Mambo muhimu ya kuzingatia katika ufugaji wa bata

Katika uleaji wa vifaranga vya bata, hakikisha joto katika wiki ya kwanza linakuwa nyuzi joto 32.2°C hadi 35.5°C. Wiki ya pili 26.7°C hadi 29.3°C na katika wiki ya tatu na nne linakuwa 23.9°C hadi 26.7°C.

Vifaranga vya bata visiogelee kwenye maji wala kunyeshewa mvua ili kuwalinda kutokana na kuathiriwa na baridi (hadi wakifikisha umri wa wiki sita).

Bata hujisugua chini ya mkia na mgongoni ili kulifanya tezi lake litoe mafuta ya kujing’arisha baada ya kuoga.

Idadi ya bata inayofungiwa ndani haiwi kubwa kama ya kuku kwa sababu watu wengi hupenda zaidi ladha ya nyama na mayai ya kuku kuliko bata.

Hata hivyo bata ana uwezo wa kutaga mayai mengi na makubwa kuliko kuku.

Bata anakuwa haraka, ana uwezo wa kula chakula hata kile ambacho hakifai kwa mwanadamu na viumbe wengine bila kuudhuru mwili wake.

Wakati wa ukame kuku hana uwezo wa kushindana nao, lakini kuwepo kwa majani mengi mabichi bata hustawi zaidi.

Bata ana uwezo mkubwa zaidi wa kujilinda dhidi ya wanyama na wadudu adui na hustamili magonjwa ya aina mbalimbali mathalani Mdondo, Gumboro hata ndui.

Ugonjwa pekee unaoshambulia zaidi bata ni homa ya matumbo (typhoid) ambapo dawa aina ya Fluban (Enrofloxaxin) imethibitika kudhibiti ugonjwa huu.

Bata pia hushambuliwa na wadudu (parasites) mbalimbali ambao hupatikana ndani na nje ya mwili wake. Mfano wa nje ya mwili ni viroboto, utitiri, chawa, na ukurutu. Vilevile ndani ya mwili ni kama minyoo ya kwenye utumbo na maini.

Ni muhimu kuwashirikisha wataalamu wa mifugo unapoona tatizo kwa bata wako, ili kuweza kupata tiba sahihi.

Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana na mfugaji Bwana Ombeni Urio kwa simu +255 756 641 810

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *