- Mifugo

MAYAI YANAWEZA KUHIFADHIWA KWA MUDA MREFU BILA KUHARIBIKA

Sambaza chapisho hili

Wakulima wanaowekeza kwenye mradi wa kuku, hupata hasara pale ambapo hawatunzi mayai ipasavyo.

Mayai ni bidhaa hafifu na inayoharibika kwa haraka, hivyo, ni lazima ishikwe kwa uangalifu na kutunzwa vizuri baada ya kutagwa ili yasivunjike au kuharibika. Watu wengi wanaonunua mayai kutoka dukani watatambua mara moja kuwa mayai hayo yamevunjika au yameoza. Tatizo hili linaweza kutokana na utunzaji na uhifadhi wakati mayai bado yakiwa kwa mfugaji.

Ili kupunguza hasara, ni lazima mfugaji ahakikishe kuwa mayai yanafika sokoni yakiwa bado mapya na salama. Utunzaji sahihi wa mayai huyafanya yaepukane na madhara yanayoweza kutokana na viumbe wadogo wadogo kama vile bakteria, wanyama walao mayai, upotevu wa unyevu, au joto wakati wa uhifadhi na kusafirisha kwenda sokoni, jambo linaloweza kuyafanya yavunjike. Mayai kama ilivyo kwa viumbe hai wengine yanahitaji kupumua. Trei za kuhifadhia mayai ziwekwe kwenye sehemu yenye hewa inayozunguka, hasa hewa ya oxyjeni.

Trei zote za kuhifadhia mayai ni lazima ziwekwe katika hali ya usafi, zisiwe na harufu ili kuepuka kufishwa au kusababisha hali yoyote inayoweza kusababisha uharibifu. Mayai ni lazima pia yakingwe dhidi ya joto kali pamoja na unyevu.

Mayai yanahitajika kuwekwa katika trei kwa mpangilio

Weka sehemu yenye ubaridi

Mayai yanaweza kuharibika kwa haraka  kutokana na joto kali. Labda yahifadhiwe kwenye jotoridi la chini, vinginevyo mfugaji atapoteza idadi kubwa ya mayai kabla hayajafika sokoni. Ni lazima kuhakikisha kuwa mayai yanahifadhiwa sehemu yenye ubaridi, ambayo siyo kavu sana, vinginevyo yatapoteza unyevu kwa haraka endapo yatawekwa sehemu kavu. Hali ya mahali pa kuhifadhia inategemea na siku ambazo  mfugaji anahitaji kuhifadhi mayai.

Wafugaji wenye uzoefu wamekuwa na uwezo wa kuhifadhi mayai kwa kipindi cha miezi 6-7 kwa kutumia jokofu. Wafugaji wadogo pia wanaweza kuhifadhi mayai kwa siku kadhaa mpaka watakapopata mayai kwa ajili ya kuhatamiwa. Kamwe usihifadhi mayai unayokusudia kutumia kwa ajili ya kuhatamiwa kwenye jokofu.

Uhifadhi wa mayai kwa ajili ya kuhatamia

Wafugaji wadogo wote hutumia njia ya kiasili kuhatamisha na kuangua mayai. Hii ni njia ya kutumia kuku au ndege mwingine ambaye hupewa mayai na kuyahatamia hadi kuanguliwa. Kuku wa kienyeji ni wazuri sana wanapotumiwa kwa ajili ya uzalishaji wa vifaranga. Hata hivyo kwa uzalishaji mzuri ni lazima mfugaji ahakikishe kuwa kuku anapewa mayai yenye uwezekano mkubwa wa kuanguliwa.

Mbinu moja wapo ambayo mfugaji anaweza kuitumia kutambua mayai yenye uwezekano mkubwa wa kuanguliwa ni kwa kumulika kwa kutumia mshumaa. Mayai yanaweza kuwekwa kwenye mwanga mkali ambao utakuwezesha kuona ndani ya yai. Kifaa rahisi cha kumulika mayai  kinaweza kutengenezwa  kutokana na kuweka balbu ndani ya boksi dogo. Unakata tundu dogo kuruhusu mwanga. Hakikisha linakuwa na ukubwa wa kuweza kuruhusu yai kukaa juu yake. Shika yai kwa kulisimamisha kwa kutumia vidole vyako viwili, kisha liweke kwenye mwanga wa tochi au balbu. Zoezi hili linakupa uhakika kuwa mayai yenye uwezekano wa kuanguliwa ndiyo pekee yanayochaguliwa.

Tengeneza sehemu ya kuhatamia mayai

Mfugaji anaweza kuboresha uzalishaji wa kuku wa kienyeji kwa kuwajengea tabia ya kuhatamia mayai. Kuku wa kienyeji wakiwa wamelishwa vizuri, wanaweza kuhatamia kati ya mayai 10-14 kwenye mzunguko mmoja. Baada ya kuangua, mfugaji amruhusu kuku kukaa na vifaranga walau kwa wiki moja. Baada ya hapo vifaranga wanaweza kutengwa.

Kuku wakiwa bado katika hali ya kuhatamia, anaweza kupewa mayai ya bandia ambayo yanaweza kutengenezwa kutokana na sabuni, huku kuku wengine wakiwa wamehatamia mayai halisi ya kutosha. Mayai bandia yanaweza kuondolewa na kuku kuwekewa mayai halisi aendelee kuhatamia mpaka yatakapoanguliwa.

Kuku wanaohatamia ni lazima wapatiwe chakula na maji ya kutosha. Kuku ambao hawahitajiki kwa ajili ya kuendelea kutotoa, wanyang’anywe vifaranga na kuachiliwa walipo kuku wengine. Ni vizuri kuweka alama kila yai kuonesha ni tarehe gani lilitagwa, hii itamsaidia mfugaji kutokuchanganya mayai ya zamani na mayai mapya. Badala yake, mfugaji anaweza kuwatenga kuku ambao amewaandaa kwa ajili ya kutotoa na wale ambao ni kwa ajili ya kutaga tu ili asichanganye mayai yake

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *