- Mifugo

Kilimo cha mahindi kwa kutumia mashimo na mbolea ya asili kimenihakikishia usalama wa chakula

Sambaza chapisho hili

“Miongoni mwa mafanikio niliyoweza kupata kutoka katika makala mbalimbali za jarida la Mkulima Mbunifu ni pamoja na; ufugaji wa nyuki, uanzishaji wa vitaru vya miti, kilimo cha mboga mboga  kwa kutumia mbolea ya asili, pia nimeweza kuboresha uzalishaji wa samaki kwa kutumia lishe ambapo imenisaidia kupata kitoweo. Kutokana na haya kipato changu kimeongezeka  na kumudu majukumu ya familia.

Hii ni habari ya Bwana Raphael Chinolo, mkulima na mfugaji kutoka mkoa wa Dodoma, wilaya ya kongwa, kijiji cha Mkoroma. Ni miongoni mwa wakulima wanufaika la jarida la Mkulima Mbunifu linalotoka kila mwezi. Raphaeli alianza kupokea jarida la Mkulima Mbunifu tangu mwaka 2014 mpaka sasa.

Yeye ni mkulima wa muda mrefu ila baada ya kuanza kupata majarida ya Mkulima Mbunifu amejifunza mambo mengi ambayo yameboresha uzalishaji wa mazao shambani.  Hapa anaelezea Kilimo cha mashimo yanayojulikana kama zai (Zai pits) ambayo amekua akitumia kuzalisha mahindi kwa mbolea ya asili alioipa jina la mapambano.

Shimo la Zai ni nini?

Zai ni neno linalotumiwa na wakulima kutoka Burkina Faso huko Afrika Magharibi kuelezea mashimo madogo ya upandaji au unyogovu katika shamba ambalo huchimbwa na kujazwa mbolea au mboji ambayo maji huvunwa ili kuhifadhi unyevu kwa uzalishaji wa mazao.

Kimsingi mashimo husaidia kutunza unyevu karibu na eneo la mizizi ya mmea. Shimo la Zai ni 20sm hadi 30sm kwa upana, 15sm hadi 20sm kirefu na urefu wa 60 hadi 80sm. Baada ya kuchimba shimo, mkulima hutumia mikono 3 hadi 4 ya samadi iliyoiva vizuri au iliyooza vizuri au mboji.

Baada ya kupanda mboga au mazao mengine yoyote, nyenzo kavu za mmea au mabaki ya mazao hutandazwa kwenye shimo kama mulch ambayo husaidia kuzuia uvukizi wa unyevu ambao mmea hutumia kukua. Shimo hilo huboresha utunzaji wa maji na kuzuia  mmomonyoko wa ardhi.

Jinsi anavyotengeneza mbolea ya asili “Mapambano”.

Bwana Raphaeli anaelezea jinsi anavyotengeneza mbolea ya asili ya Mambambano. Mbolea hii inatengenezwa kwa kutumia mimea ya asili, majivu, samadi mbichi na masalia ya mimea ya mazao yaliopita.

Mahitaji ya utengenezaji

  • Shimo lenye upana wa mita 2 hadi mita 3 na kina chenye urefu wa mita 2 kwenda chini ya aridhi.
  • Majivu
  • Masalia ya mimea, mfano mimea ya mahindi iliyokauka au nyasi kavu
  • Mbolea ya samadi, iwe mbichi(iliyotolewa bandani muda huohuo)

Namna ya kufanya:

Ujazaji wa mahitaji yote ndani ya shimo hutegemea zaidi urahisi wa upatikani wa mahitaji tajwa.  Mkulima akipata yote anaweza kujaza siku moja na kama ni ya kutafuta yanaweza kujazwa hata ndani ya wiki moja.

  • Hatua ya kwanza, baaada ya kuchimba shimo weka majivu kiasi cha kilo 5 kwenye shimo hilo.
  • Hatua ya pili, weka masalia ya mimea ya mahindi au nyasi kwenye shimo hilo, hakuna kiasi ni makadilio tu.
  • Hatua ya tatu, weka mbolea ya samadi mbichi kiasi cha ndoo 3 kubwa.

MUHIMU: Mtengenezaji wa mbolea ya mapambano anatakiwa kurudia mchakato huo kwa kufuata mfano wa hatua hizo kama zilivyo mpaka shimo lijae. Baaada ya shimo hilo kujaa mkulima ataacha kwa miezi 3. Kwa kipindi chote cha miezi 3 mtengenezaji wa mbolea ya mapambano anapaswa kumwagilia maji ili kuweka unyevunyevu unaorugusu mbolea kuoza haraka. Baada ya miezi 3 ambayo sawa na siku 90 mbolea ya mapambano inakuwa imeiva na tayari kwa matumizi shambani.

Kilimo cha Mashimo

Kilimo cha mashimo ni kilimo endelevu ambacho kinasaidia kuhifadhi rutuba ya udongo na  unyevunyevu. Bwana Raphael Chinolo hutumia mbolea yake ya asili ya mapambano katika kilimo chake cha mashimo hasa kwa zao la mahindi na mtama. Kilimo cha mashimo huacha nafasi ya maji kutuama, hata mvua ikinyesha kidogo mashimo yanaweza kuvuna maji.

Namna ya kulima kilimo cha mashimo

  • Chimba mashimo kwa vipimo, ukubwa wa shimo unatakiwa kuwa sentimita 20 hadi 30, kina ni sentimita 15-25sm. Umbali kati ya shimo moja na lingine ni mita 2.
  • Weka nusu lita ya mbolea ya mapambano katika kila shimo shamba zima, baada ya mbolea weka mbegu mbili mbili za mahindi kila shimo, kisha fukia mashimo kiasi na kuacha uwazi kidogo kwaajili ya kuvuna maji ya mvua. (hata kama mvua itanyesha kidogo maji yatatuama tu na kuweza kutunza unyevunyevu).
  • Baada ya kupanda, unasubiria muda wa palizi ambapo kulingana na utofauti wa maeneo, baadhi maeneo inaweza kuwa palizi mara 2 na wengine palizi mara 3, na baada ya hapo mkulima atakuwa anasubiria mavuno.
  • Kipindi cha kusubilia mavuno kinaweza kuwa kati ya miezi 4 hadi 5.

Faida

Mkulima anaweza kupata mazao mengi baada ya matumizi ya mbolea ya asili na ufuatiliaji sahihi wa kilimo cha mashimo.  Mmea unapopata mbolea na unyevunyevu hata mvua inapokua kidogo lazima utoe mazao bora. Shamba la hekari moja, kwa uzoefu wa bwana Chinolo katika kilimo cha mashimo, mkulima anaweza kupata gunia 25 mpaka 30 za mahindi, na kama amekumbana na changamoto kubwa  huweza kupata gunia.

Kutokana na faida anazopata kupitia jarida la Mkulima Mbunifu anasema  “Nimeweza kuisadia jamii inayomzunguka kwa kuweza kuwapatia badhi ya nakala za majarida mbali mbali ya Mkulima Mbunifu.  Pia nimeweza kusaidia taasisi na vikundi kwa kuwapatia majarida niliyopata na wao wamefanikiwa mfano; kikundi cha juhudi, kikundi cha jitolee, kikundi cha upendo kilichoko chini ya kanisa Anglikana kutoka kijiji cha Suguto, kanisa la Pentekoste, kanisa la Anglikana Chamkoroma”.

Changamoto

Kama ilivyo kwa miradi mingine, changamoto ni sehemu fursa kuwezesha mafanikio ya mradi.  Bwana Chinolo anaeleza changamoto anayokumbana nayo ni pamoja wakulima kutoamini uwezo wa mbolea ya mapambano inavyoweza kutoa mazao mengi hata kipindi ambacho mvua nichache. Hivyo kuhisi anatumia uchawi kuweza kufanikiwa, ila baadhi ya wakulima ambao ameweza kuwafundisha wameona faida yake.

Wito kwa wakulima

Bwana Raphaeli anawashauri wakulima kufanya kazi kwa bidiii. Kwanza wakulima kuzingatia misimu ya kilimo na kuandaa mashamba mapema kabla ya msimu wa kupanda kuanza. Pili ni muhimu kuzingatia mchakato mzima wa kilimo nini kinahitajika kwa mfano katika kilimo chochote rutuba ya udongo ni muhimu, hivyo ni kwanamna gani basi unaweza kurutubisha udongo wako. Mbolea ya asili ndio jibu la mafanikio yako, kwani ni rahisi kutengeneza mahitaji yanapatikana katika mazingira tunayoishi.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *