- Mifugo

Je, unafahamu kwa nini asali huganda?

Sambaza chapisho hili

Asali ni moja ya mazao yanayotokana na nyuki wakubwa au wadogo ikiwa katika kimiminika na yenye ladha ya sukari. Nyuki hutengeneza asali hii kwenye mzinga kwa kuchukua malighafi toka kwenye maua au miti yam aua ya aina mbalimbali na yanayopatikana katika eneo lilipowekwa mizinga.

Asali hii huwa katika mfumo wa kimiminika yaani maji maji lakini wakati mwingine huweza kuganda bila mfugaji kufahamu nini hupelekea ugandaji huu.

Kutokufahamu hasa nini sababu za asali kuganda kumekuwa kukisababisha wafugaji wengi kuhofia kuipeleka asali sokoni pindi wanapogundua imeganda wakiamini kuwa kuganda huko kunaweza kuwa ni kuharibika.

Kwa kawaida asali inaweza kuganda kwa namna mbili, moja ikiwa ni asali yote ndani ya chombo ilimotunzwa na nyingine inaweza kuganda sehemu tu au nusu ya asali katika chombo.

Mfano ukichukua chupa ya asali ulimoweka na kukuta asali yako ikiwa imeganda sehemu ya chini na juu ikiwa haijaganda, basi asali hii itakuwa na dosari.

Kuganda kwa asali yote

Mfugaji anapaswa kufahamu kuwa nyuki anapotengeneza asali ndani yake hutokea sukari ambayo huipata kutokana na malighafi anazotumia kutengenezea asali hiyo.

Kitalaamu nyuki hutengeneza asali kwa kuchukua unga wa maua ujulikanao kama pollen (chavua) na majimaji matamu ya maua yaitwayo nectar (mbochi), kutoka katika vyanzo mbalimbali ambavyo ni mimea.

Nyuki anapochukua malighafi hizi kutengeneza asali, huzichanganya kwa pamoja (husindika) kwa ujuzi wake hivyo asali kupatikana na kuhifadhiwa ndani ya masega kama chakula cha akiba cha nyuki kwa ajili ya kuitumia katika kipindi cha njaa pale kunapokuwa na upungufu wa maua/chakula cha kutosha.

Kwa kawaida mchakato mzima wa nyuki unapokamilika na kuifanya asali kuiva ndani ya mzinga wake basi huzalisha asali yenye mchanganyiki wa sukari kuu za aina mbili ambazo ni;

  • Fructose
  • Glucose

Sukari hizi mbili ndiyo sababu ya kuganda kwa asali ya nyuki iwapo aina moja ya sukari itazidi zaidi. Lakini kuzidi kwa sukari hizo siyo jambo la makusudi linalofanywa na nyuki bali hutokea kutokana na upatikanaji wa maua mengi yenye aina moja ya sukari kwa wingi.

Ikiwa katika mchakato wa utengenezaji wa asali nyuki ametafuta malighafi zake kwa ajili ya kutengeneza chakula chake (asali) katika eneo alipo na kubahatika kupata au kuchukua chavua ya maua kwa ajili ya kutengenezea asali yenye kiwango kikubwa cha sukari nyingi aina ya Fructose zaidi ya glucose, basi asali hii haitokuwa na tabia ya kuganda.

Lakini ilitokea nyuki amechukua chavua yenye kiasi kikubwa cha sukari ya glucose kuliko ile ya fructose basi asali itakayozalishwa na nyuki hao mara nyingi itakuwa na tabia ya kuganda, hivyo baada ya kuvunwa ndani ya muda mfupi wa kutunzwa itaganda yote katika chombo ilimotunzwa.

Hivyo sasa ikiwa asali itaganda yote ndani ya chombo chako, siyo kwamba ina kasoro bali itakuwa imetokana na aina ya sukari iliyopatikana kwenye malighafi zake.

Asali hiyo pia ikiganda hutengeneza chengachenga nyingi ziitwazo Crystallize na humpasa mtumiaji anapotaka kuitumia, lazima aiweke kwenye jua au ndani ya maji ya moto ndiyo iyeyuke (siyo kuichemsha) kwa ajili ya kuitumia. Asali hii bado ni nzuri na bora kwa watumiaji.

Asali ikiganda nusu kuna kasoro

Ikitokea asali imeganda nusu na sehemu ikiwa haijaganda, asali hii itakuwa na dosari na mara nyingi inaweza kuwa imechanganywa na kitu kingine cha ziada pamoja na kuongezwa maji tofauti na kipimo cha nyuki.

Asali huganda nusu chini ya chupa ikiwa imeongezwa sukari ya ziada na hivyo kupoteza ubora na kukosa sifa ya kuuzika. Wakati mwingine hii huweza kusababishwa na uchafu hasa pale asali inapotunzwa katika chombo chenye mafuta, sukari na maji.

MUHIMU

Asali inapaswa kutunzwa katika chombo safi, kikavu na kisicho ma maji wala aina yoyote ya kitu kinachoweza kuchanganyikana na asali na kupelekea uharibifu.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *