- Mifugo

Fahamu zao la sumu ya nyuki na uvunaji wake

Sambaza chapisho hili

Nchini Tanzania na maeneo mbalimbali barani Afrika, kumekuwa na ufugaji wa nyuki kwa ajili ya uvunaji wa mazao yake ili kujipatia fedha. Nyuki huvunwa mazao sita ambayo ni Asali(Honey), Nta (Wax), Chavua (Pollen), Gundi ya nyuki (Propolis), maziwa ya nyuki (Royal Jerry) pamoja na Sumu ya nyuki (Bee Venom). Lakini wafugaji wengi wamekuwa wakihagaika zaidi na zao la Asali na Nta hii ni kutokana na kukosa maarifa ya uvunaji wa zao la Sumu ya nyuki.

Wakati mazao ya asali na Nta huvunwa kwa nyuki mara mbili kwa mwaka katika mzinga mmoja, zao la sumu huvunwa mara mbili kwa wiki katika mzinga mmoja. Ili kuivuna sumu mfugaji hulazimika kuwa na mashine maalumu kwa ajili hiyo ambayo sehemu ya kifaa chake hutegeshwa katika mlango wa mzinga au juu yake baada ya kuondoa mfuniko wa mzinga kuwashawishi nyuki kutoka kushambulia wakiamini ni adui hivyo kuacha sumu hiyo ambayo baadaye hukusanywa kwa utaratibu maalum na kuhifadhiwa tayari kwa kuuzwa.

Katika mzinga mmoja mfugaji anaweza kuvuna kiasi cha 0.20 hadi 0.85 ya gramu lakini ikitegemea ukubwa wa kundi la nyuki waliomo ndani yake na namna ya uvunaji. Asali huuzwa kwa kipimo cha kilo moja (sawa na gramu 1,000), sumu huuzwa kwa kipimo cha gramu mmoja kwa zaidi ya bei ya asali.

Sumu ya nyuki ni nini

Sumu ya nyuki ni kemikali asili au tindikali isiyo na rangi, ambayo hutengenezwa na kuhifadhiwa ndani ya mwili wa nyuki na wao huitumia kwa kujilinda na maadui wao kwa kuwashambulia pale wanapohisi kuvamiwa.

Sumu hii hutolewa na nyuki kwa njia ya mwiba wake (Stingers) uliopo nyuma ya mwili wake wakati wanaposhambulia maadui baada ya kuvamiwa.

Sumu hii inapoingia kwenye mwili wa adui husababisha maumivu makali kutokana na vichochezi ilivyonavyo ambavyo ni Phospholipase A2, Enzyme na Allergen kuu ambayo husababisha huathiri kwa kushambulia seli za adui.

Hata hivyo kulingana na tafiti mbalimbali kiasi cha vichochezi vilivyomo ndani ya sumu licha ya kuwa na athari inayosababisha maumivu hasa kwa binadamu anapoumwa na nyuki, ilibainika vimekuwa mali ya faida kwa binadamu hivyo kuifanya sumu ya nyuki kuwa bidhaa muhimu kwa matumizi ya kibinadamu. Umuhimu huu pia umechochea kuongezeka kwa matumizi yake na hivyo kuwalazimu watalaamu kubuni teknolojia ya kuvuna sumu hiyo.

Uvunaji wa sumu ya nyuki

Ili kuvuna sumu ni lazima mfugaji awe na mizinga ya nyuki yenye makundi makubwa na waliokaa ama kuishi ndani yake muda mrefu walau isiwe chini ya miezi mitatu, awe na mashine ya kuvunia, chupa ya kutunzia pamoja na jokofu kwa ajili ya kuhifadhi sumu hiyo kabla ya kuiuza au kuipeleka sokoni.

Sumu hii pamoja na kwamba hutolewa ikiwa kimiminika lakini inapovunwa huwa katika unga ambao unapaswa kutunzwa kwa makini kwa kuukinga na joto kali, mwanga wa jua na maji, hivyo sumu hii hutunzwa kwenye chupa maalumu isiyoruhusu mwanga wa jua na huihifadhi kwenye jokofu kwa muda ambao hungoja kusafirishwa au kupelekwa sokoni.

Sumu hii ikitunzwa vyema kwa kuzingatia utaratibu huweza kukaa muda mrefu hata zaidi ya mwaka hivyo ni lazima kuzingatia kanuni na taratibu za utunzaji.

Sifa za sumu ya nyuki

Mfugaji anapoivuna sumu hii anapaswa kuhakikisha inakuwa safi na alazima ajiepushe na kuichanganya na kitu chochote na ili kuweza kuiuza ni lazima iwe na rangi nyeupe au brownish. Sumu ikiwa na rangi nyeusi wala majimaji huwa imeharibika hivyo kupoteza sifa sokoni.

Matumizi ya sumu ya nyuki

Hutumika katika tiba ya kuzuia magonjwa na maumivu (Apitherapy), ingawa hivi karibuni imepata umaarufu zaidi, tiba ya sumu ya nyuki imekuwa ikitumika katika mazoea ya dawa za jadi kwa miaka mingi.

Kwa sasa sumu hii hutayarishwa sindano za kinga za mwili kwa magonjwa ambazo zimekuwa zikisimamiwa na wataalamu wa huduma za afya na pia zimekuwa ikiongezwa katika utayarishaji wa bidhaa kama vile Moisturizers, Lotions na Lozenges ikiwa sehemu ya virutubisho na viboreshaji.

Angalizo kwa wavunaji sumu

Afisa Nyuki wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Deo Justus anaeleza kuwa wafugaji wanapaswa kuwa makini na uvunaji wake na ikiwalazimu kuanza uvunaji wanapaswa kutengenisha mizinga ya uvunaji huu na ile ya uvunaji asali.

“Zao la Sumu ya nyuki ni zao lenye fedha zaidi ya asali na upatikanaji wake ni tofauti na asali, lakini kitaalamu tunawashauri wafugaji nyuki wanapotaka kuanza uvunaji kwanza wawe na mizinga mingi na ikiwezekana waitege mara mbili ili kuwa na ile ya uvunaji asali pekee na sumu peke yake.”

Unapovuna sumu kila baada ya wiki unawasumbua nyuki kiasi cha kutosha hivyo hali hii huathiri upatikanaji wa asali, hivyo kusisitiza kuwa wafugaji wakiamua kuanza uvunaji sumu watarajie kupata mazao kidogo ya asali tofauti na awali.

“Kuna namna tofauti za kuvuna sumu, unaweza kuvuna kwa kipindi cha Dk. 30 hadi 50 kwa kila mzinga na kurejea kuvuna kila baada ya siku tatu, lakini njia nyingine unaweza kuvuna kwa muda wa saa 2-3 kwa mzinga mmoja na kurudia kuvuna baada ya siku 10, hii ya kila baada ya siku 10 ni njema lakini inahitaji kuwa na mashine za kuvunia zaidi kwa wenye mizinga mingi,” aliongeza.

Licha ya mavazi ya kujikinga na nyuki kuwauma kwenye sumu pia mvunaji anapaswa kuwa na mavazi ya kujikinga macho na mdomo na pua (mask) ikiingia machoni huwasha mithiri ya pilipili na kusababisha kuoona kwa muda.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *