- Mifugo

Fahamu ugonjwa wa ukurutu na namna ya kuudhibiti

Sambaza chapisho hili

 

Ukurutu ni ugonjwa wa ngozi ambao huambukizwa kwa njia ya kugusana kati ya mnyama aliyeathiriwa na aliye mzima.

Kitaalamu ugonjwa huu hujulikana kwa jina la menji (Mange) na husababishwa na utitiri ambao kitaalamu wanaitwa mange mites.

Wadudu hawa hujikita kwenye ngozi na kufanya ngozi kuwa ngumu kama yenye magaga, kumfanya mnyama kuwashwa na mwisho manyoya kupukutika na kuondoka kabisa.

Aina za ukurutu

Kuna aina nyingi za ukurutu lakini aina kuu nne ndizo zinazojulikana na kushambulia wanyama kwa wingi hapa nchini. Aina hizo ni kama ifuatavyo;

Ukurutu Demodektiki (Demodectic Mange)

Hii ni aina ya ukurutu husababishwa na wadudu ambao hujikita kwenye vijishimo vya vinywelea na matezi na kusababisha kutokea kwa vivimbe ambavyo huwa na muwasho katika sehemu za shingoni, mabegani, usoni, mgongoni.  Aidha, husababisha kutokea kwa ute wenye rangi ya kijivu na huweza kuwa na wadudu. Ukurutu huu hushambulia mbwa, ng’ombe, kondoo, mbuzi, farasi, mbwa na nguruwe.

Ukurutu Sakoptiki (Sarcoptic Mange)

Ukurutu huu huenea kwa njia ya mgusano kati ya mnyama mwenye ugonjwa na asiyekuwa na ugonjwa na huenea kwa haraka sana. Aidha, imebainika kuwa, wanyama wanyonyeshao huambukiza watoto wao haraka sana hasa wakati wa kunyonyesha.

 

Ngozi ya mnyama mwenye sakoptiki huwa ngumu, huvimba na huwa na muwasho.

Ukurutu Soroptiki (Psoroptic Mange)

Aina hii ya ukurutu hushambulia ng’ombe, mbuzi, kondoo, farasi, nguruwe, mbwa na paka. Ugonjwa huu huenezwa kwa njia ya kugusana kati ya mnyama aliyeathirika na yule ambaye hajaathirika.

Ukurutu korioptiki (Chorioptic Mange)

Hii ni aina nyingine ya ukurutu ambao huenezwa kwa njia ya kugusana kati ya mnyama na mnyama (mwenye ugonjwa na asiyekuwa na ugonjwa). Huathiri wanyama kama ng’ombe, kondoo, nguruwe, mbwa, mbuzi, farasi.

Dalili za ugonjwa wa ukurutu

  • Mnyama ambaye tayari ana ugonjwa huu kujikuna sana na mara kwa mara na hii ni kutokana na muwasho unaokuwepo kwenye ngozi.
  • Kutokana na kujikuna mara kwa mara, manyoya huanza kunyofoka siku hadi siku.
  • Ngozi ya mnyama muathirika na ugonjwa huu huanza kutoa unga unga.
  • Ngozi ya mnyama pia huwa ngumu na hukakamaa.
  • Mnyama huwepa kupata vivimbe katika sehemu mbali mbali kama shingoni, kwenye mabega, mgongoni na hata usoni.
  • Ngozi ya mnyama pia huweza kuvimba na huwasha sana na ndiko kunakopelekea kujikuna.

Tiba

Mnyama aliye na ugonjwa huu huweza kutibiwa na kupona kabisa kwa kutumia aina mbili za dawa ambazo ni dawa za sindano au dawa za kuogesha.

Dawa ya sindano

Mnyama atibiwe kwa kutumia dawa aina ya Ivermectin na kwa kuzingatia utaratibu kutoka kwa mtaalamu wa mifugo kwani kila mnyama hupewa dozi tofauti na mwingine.

Dawa ya kuogesha

Dawa zinazotumika kwa ajili ya kuogeshea ni zile ambazo zina kiini tete kiitwacho Amitraz kama vile TIXFIX, BAMITRAZ na TWIGATRAZ.

Namna ya kukinga ugonjwa wa ukurutu

  • Kama mfugaji, hakikisha unafanya usafi wa banda mara kwa mara.
  • Ogesha mifugo kila wakati kulingana na utaratibu unaotolewa na wataalamu wa mifugo.
  • Pulizia banda la mifugo dawa zenye Amitraz ili kuua utitiri.
  • Ikiwa umegundua kuna mnyama ameanza kuonyesha dalili za ugonjwa huu, mpatie tiba mapema ili kuwakinga wengine na ikiwezekana wapatie na wanyama wengine wote ambao bado hawaonyesha dalili hiyo.

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

2 maoni juu ya “Fahamu ugonjwa wa ukurutu na namna ya kuudhibiti

  1. Naomba kuuliza nguruwe aliye na ugonjwa wa ukurutu unaeza kumuogesha na dawa za kuogeshea NG’OMBE
    Asant

    1. Habari, Karibu Mkulima Mbunifu na asante kwa swali lako. Kama nguruwe wako anau ugonjwa wa ukurutu ni muhimu pia kufahamu ni aina gani ya ukurutu kwani kuna aina mbalimbali za ugonjwa huu, hii itakusaidia kujua namna ya kupambana kuepuka kupata ugonjwa huu tena mara utakapowatibu. Kuna dawa zinazotumika kwa ajili ya kuogeshea, na dawa hizi ni zile ambazo zina kiini tete kiitwacho Amitraz kama vile TIXFIX, BAMITRAZ na TWIGATRAZ. Pia ugonjwa huu unaweza kutibiwa kwa dawa za sindano yaani dawa aina ya Ivermectin na kwa kuzingatia utaratibu kutoka kwa mtaalamu wa mifugo kwani kila mnyama hupewa dozi tofauti na mwingine.

      Ili kukinga nguruwe na ugonjwa huu, hakikisha unafanya usafi wa banda mara kwa mara, kuogesha mifugo kila wakati kulingana na utaratibu unaotolewa na wataalamu wa mifugo, kupulizia banda la mifugo dawa zenye Amitraz ili kuua utitiri.

      Ikiwa umegundua kuna mnyama ameanza kuonyesha dalili za ugonjwa huu, mpatie tiba mapema ili kuwakinga wengine na ikiwezekana wapatie na wanyama wengine wote ambao bado hawaonyesha dalili hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *