- Mifugo

Fahamu namna magonjwa makuu ya mifugo yanavyoambukizwa na namna ya kukabiliana nazo

Sambaza chapisho hili

Magonjwa ya mifugo ni moja kati ya matatizo yanayokabili maendeleo ya tasnia ya mifugo nchini.

Kumekuwepo na kuenea kwa magonjwa ya mifugo nchini kama vile magonjwa ya mlipuko yasiyokuwa na mipaka, magonjwa yanayoenezwa na wadudu, magonjwa ya mifugo yanayoambukiza binadamu na magonjwa yanayojitokeza ambayo ni changamoto kubwa kwa maendeleo ya tasnia ya mifugo.

Kwa kuwasaidia wafugaji waweze kutunza afya ya mifugo, kuongeza kipato, na kudumisha afya zao pia ni vizuri kuzingatia na kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa hayo.

Mambo yanayochangia ongezeko la magonjwa ya mifugo;

Mabadiliko ya tabia nchi

Joto katika nchi za Afrika Mashariki, kama ilivyo katika sehemu nyingine nyingi ulimwenguni, linazidi kuongezeka taratibu. Licha ya hivyo, mabadiliko ya hali ya hewa unasababisha ongezeko la matukio ya hali mbaya ya hewa, ukame kutokea mara kwa mara zaidi, lakini pia mafuriko kutokea mara nyingi zaidi inaponyesha mvua.

Mifugo inapodhoofika kwa kukosa malisho au maji, uwezo wa mifugo  kustahimili magonjwa unapungua, na baada ya kupata magonjwa, uwezo wa kustahimili ukame pia unapungua.

Aidha, joto linapoongezeka na mvuke hewani kubadilika, wadudu wasambazao magonjwa huenea kwenye maeneo mengi zaidi na kusababisha mifugo kupata magonjwa hasa katika maeneo ambayo hapo awali hayakuwa na magonjwa.

Kupungua kwa ardhi

Matumizi ya ardhi iliyokuwa malisho kwenda kwenye kilimo kunasababisha wafugaji kubanana kwenye maeneo madogo kuliko hapo awali, na kuwanyima uwezo waliokuwa nao wa kuhamahama kufuatana na majira ya mvua na malisho mazuri. Hali hii hupelekea pia miingiliano na wanyamapori kuwa mikubwa.

Magonjwa ya mifugo na namna ya kukabiliana nazo

Kimeta (Anthrax)

Ugonjwa wa kimeta hushambulia mifugo au wanyama walao majani. Vimelea vya ugonjwa huu vinaweza kuishi kwenye udongo kwa muda mrefu na kuna uwezekano wanyama wakapata ugonjwa wa kimeta mwanzoni mwa majira ya mvua, wakati majani wanayokula yanapokuwa mafupi.

Aidha, kutokana na mabadiliko ya matumizi ya ardhi, wakati mwingine mifugo na wanyamapori kukaa pamoja kwenye eneo dogo na kupelekea matukio ya kimeta kuongezeka. Binadamu wanaweza pia kuupata ugonjwa huu, kwa kushika au kula nyama ya mifugo iliyoambukizwa.

Dalili za kimeta

  • Kifo cha ghafla
  • Uvimbe kwenye shingo, kifua, tumbo, na/ au miguu ya mifugo inayougua lakini haifi.

Kuzuia na kudhibiti

Chanja mifugo kwa miezi kati ya tisa na kumi na mbili na chanjo hiyo iwe imehusisha juhudi ya jamii au serikali ikilenga kuwachanja ng’ombe wote. Dawa dhidi ya bakteria (Antibiotics) zinaweza kuwa dawa sahihi iwapo matibabu yataanza mapema.

Homa ya Bonde la Ufa (Rift Valley Fever)

Ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa unaenezwa na panya na mbu. Hii hutokea pale ambapo mbu wanang’ata panya walioambukizwa, na mbu hao wanasambaza ugonjwa kwa mifugo pale wanapowang’ata.

Maambukizi ya ugonjwa yanaongezeka zaidi wakati wa kipindi cha mvua kwani panya huongezeka na mbu wengi huzaliwa hasa kutokana na maji yanayojikusanya kwenye madimbwi kutokana na mvua.

Mabadiliko ya tabia nchi wakati mwingine yanapelekea kuwepo kwa majira ya mvua nyingi au inayonyesha kwa vipindi virefu zaidi hivyo  huleta milipuko ya ugonjwa wa huu hivyo wafugaji wanatakiwa kuchukua tahadhari mapema.

Dalili

  • Kwa mifugo: Mara nyingi dalili kuu ni mimba kuharibika kwa ng’ombe, mbuzi au kondoo.
  • Kwa binadamu: Dalili zinazoonekana ni mafua, homa ya ghafla, kuumwa kichwa, na maumivu ya misuli na mgongo. Kama mwili umebadilika na kuwa wa manjano na unatapika, nenda hospitali haraka la sivyo kupungukiwa damu, upofu au kifo vyaweza kutokea mara moja.

Kuzuia na kudhibiti

  • Kwa mifugo: Chanja mifugo kila mwaka ili kuzuia na ufanya hivi kama wanajamii au kwa masaada wa serikali kutoa chanjo kwa mifugo kwa wakati mmoja kunasaidia zaidi.
  • Kwa binadamu: Tumia chandarua kuzuia kuumwa na mbu na jiepushe kugusa mimba ya mifugo iliyotupwa. Pia jikinge kwa kuvaa mikononi glovu au mifuko ya plastiki na fukia mzoga kwenye shimo refu kiasi ambacho mbwa na wanyama wengine walao nyama hawawezi kufukua.

Ugonjwa wa Miguu na Midomo (Foot and Mouth Disease (FMD)

Huu ni ugonjwa unaoathiri ng’ombe, kondoo, mbuzi, mbogo, swala na wakati mwingine tembo. Ugonjwa huu husambaa haraka kwenye kundi hasa ukisababisha vifo vya ndama na wanyama wengine kupoteza uzito na kupelekea uzalishaji kupungua.

Ugonjwa huu unaambukiza kwa kugusana kati ya mnyama mmoja na mwingine na unaweza pia kusambazwa na upepo kwenye umbali hata wa kilometa 250.

Dalili

  • Mifugo kuonyesha dalili za mafua, na kuchechemea kwa wakati huo huo.
  • Ndama kufa kwa ghafla kutokana na ugonjwa wa moyo.

Kuzuia na kudhibiti

  • Chanjo dhidi ya ugonjwa huu itolewe kwa wafugaji kushirikiana kwani zinapatikana nje ya nchi na gharama zake ni kubwa kiasi.
  • Ugonjwa huu ni hatari, hasa pale ambapo mifugo inatumia ardhi ambayo pia inatumiwa na mbogo na nyumbu.

Ndorobo (Trypanosomiasis)

Ugonjwa wa ndorobo hushambulia wanyamapori, mifugo kama ng’ombe, kondoo, mbuzi, punda na mbwa pamoja na binadamu. Mbung’o ndio huambukiza ugonjwa kutoka kwa mnyama au mtu ambaye amekwisha shambuliwa kwenda kwa mwingine.

Ugonjwa huu unaposhambulia binadamu hujulikana kama “homa ya malale”.

Kwa miaka iliyopita, watu walikwepa maeneo yenye mapori ambapo kwa asili ndiko mbung’o wanakozaliana lakini kutokana uhaba wa ardhi wafugaji wanalazimika kusogea zaidi kwenye maeneo hayo kwa ajili ya malisho. Ugonjwa huu ni hatari kwani huweza kumrudia mnyama kwa mara kadhaa.

Dalili

  • Kwa mnyama; Homa zisizoisha, kuvimba, na kuharibika kwa mfumo wa mishipa ya fahamu. Kupungua kwa uzito, damu kupungua na hata kupelekea vifo.
  • Kwa binadamu; ugonjwa wa homa ya malale husababisha homa, kichwa na viungo kuuma, na mwili kuwasha. Aidha, kuharibika kwa mishipa ya fahamu na kupelekea kuchanganyikiwa, na hali isiyokuwa ya kawaida ya kusinzia.

Kuzuia na kudhibiti

  • Kuweka mpango mzuri wa matumizi ya ardhi unaowahakikishia wafugaji kuwa na ardhi ya kutosha isiyokuwa na mbung’o.
  • Kutandaza kwenye miti au vichaka vipande vya nguo nyeusi, bluu au nyeupe, ambavyo vinakuwa vimetumbukizwa kwenye dawah ii husaidia kuwavuta na kuua.
  • Zipo dawa za kutibu ndorobo, lakini vimelea vya ugonjwa huu vinaweza kuwa sugu kwa dawa hivyo pangaji mzuri wa matumizi ya ardhi upewe kipaumbele katika kudhibiti.

Mambo muhimu ya kuzingatia

  • Magonjwa ya mifugo yanaweza kupunguzwa kwa kupanga vizuri na kugawana matumizi ya ardhi, ili kuhakikisha kuwa wafugaji hawasukumwi kufanya shughuli za ufugaji kwenye maeneo yanayosifika kwa kuwa na magonjwa.
  • Wafugaji wanahitaji nafasi ya kutosha, kiasi cha uwezo wa kuhamahama na uwezo wa kufanya mabadiliko yanayoweza kuruhusu mifugo kubaki na afya inayostahili.
  • Wakulima na wafugaji kushiriki pamoja katika kupanga matumizi ya ardhi kunaweza kuwa kwa manufaa.
  • Kuweka mikakati ya kupunguza athari za matukio ya ukame yanayoweza kutokea kwa mfano; kuhifadhi malisho, kuvuna maji ya mvua na kuendeleza mabwawa ya asili na yale yaliyochimbwa.
Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

2 maoni juu ya “Fahamu namna magonjwa makuu ya mifugo yanavyoambukizwa na namna ya kukabiliana nazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *