- Mifugo

Fahamu changamoto zinazosababisha vifo vya samaki katika bwawa

Sambaza chapisho hili

Ufugaji wa samaki kwa sasa ni moja ya mradi mzuri kiuchumi, hapa nchini na nje ya nchi. Pamoja na ufugaji huu kuendelea kuna changamoto zinazoikabili ambazo ni muhimu wafugaji kutambua ili kuepuka hasara.

Elimu ya ufugaji wa samaki kwa miaka ya karibuni imekuwa ikiwafikia wengi na hii ni kutokana na usambazaji wa taarifa kwa haraka kwa wafugaji kupitia vyombo mbalimbali vya habari, kama vile redio, televishieni, magazeti na majarida, hivyo kuendelea kufanya miradi ya ufugaji wa samaki kuwa na tija zaidi.

Licha ya mafanikio mbalimbali baadhi ya changomoto zinaweza kujitokeza katika ufugaji huu ikiwa ni pamoja na uwepo wa vifo vya samaki katika bwawa.

Sababu zinazosababisha vifo vya samaki kwenye bwawa
Maji kuchafuka kupitiliza
Maji ni kitu kikubwa katika ufugaji wa samaki na huwezi kufuga samaki pasipo kufikiria suala la upatikanaji wa
maji.

Samaki kama viumbe wengine hutumia hewa safi (oksijeni) ya kwenye maji kwa ajili ya kupumua na hewa ikiwa safi kwenye maji husababisha ukuaji mzuri wa samaki. Kadri samaki anavyozidi kukua utoaji takamwili au vinyesi vyake huongezeka zaidi kuliko akiwa mdogo hivyo ubadilishaji wa maji wa samaki wakiwa wadogo ni tofauti kabisa na samaki akiwa mkubwa. Hali hii ya vifo kwa samaki hutokea zaidi kati ya miezi mitatu na kuendelea.

Mfugaji anaweza kujaza maji mara ya kwanza kwa kutumia maji ya kisima, mvua au maji ya kulipia kupitia mamlaka za maji kutokana na eneo husika hivyo samaki kadri anavyozidi kukua inabidi ubadilishaji wa maji ufanyike mara kwa mara ili kuzuia maji kuzalisha hewa chafu ambayo sio nzuri kwa samaki.

Maji yakiwa machafu sana husababisha hali ya ukijani kuwa mwingi uliopitiliza hivyo ukijani huo husababisha ushindani mkubwa wa hewa baina ya samaki na mimea (algae) hivyo samaki hushindwa kupata hewa ya kutosha.

Ulishaji wa chakula kupitiliza
Samaki wanapaswa wale ili wakue vizuri na kwa wakati ambao mfugaji amekusudia. Ulishaji wa chakula kupitiliza husababisha uchafukaji wa maji kwa haraka kwa kuwepo kwa mabaki ya chakula ambacho huzama chini ya bwawa.

Baada muda mabaki hayo ya chakula huaribika/kuoza na kutengeneza wadudu hatarishi kama vile bakteria ambao hushambuliwa samaki kwenye matamvua/mashavu (gills) ambapo ndio sehemu muhimu kwa samaki katika upumuaji.

Chakula kisichokuwa na mchanganyiko mzuri wa virutubisho
Samaki kama viumbe wengine wanahitaji chakula kilicho changanywa vizuri kulingana na aina ya samaki husika kwa kuwa kila samaki ana mchanganyiko pekee wa chakula kutegemea jamii ya samaki husika.

Katika mchanganyiko wa chakula kama mfugaji asipozingatia uwepo wa kirutubisho husika basi hupelekea
madhara kwa samaki.

Upandikizaji wa samaki uliopitiliza kiwango kwenye bwawa lako
Ili ufugaji samaki uweze kuwa wa mafanikio basi ni vema mfugaji azingatie kanuni bora za upandikizaji wa samaki kwa idadi maalum kwenye bwawa. Samaki wakiwa wengi huku eneo la bwawa likiwa dogo, basi watabanana na kusababisha kufa kwani hukosa hewa safi. Ulishaji huwa hafifu kwani wengine hushindwa kula na uchafuzi
wa bwawa kuwa mwingi.

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *