- Mifugo

Boresha kundi lako la kondoo kwa kuzalisha chotara

Sambaza chapisho hili

Njia ya haraka zaidi ya kuboresha kundi lako ni kuzalisha kondoo chotara. Inashauriwa utumie kondoo wa kienyeji kama wanyama wa kuanzia mpango wa kuzalisha kondo bora zaidi.

Unaweza kutumia kondoo jike wa kienyeji aina ya Red Maasai na dume wa kigeni aina ya Dorper.

Kondoo wanaozaliwa watabeba sifa za aina hizi mbili za kondoo (Red Maasai na Dorper).

Njia hii ya kuboresha kondoo ni ya gharama ya chini ikilinganishwa na kununua wanyama waliokwisha kuboreshwa, ambao mara nyingi huuzwa kwa bei ya juu.

Mifugo wa kienyeji wamezoea hali ya hewa ya Tanzania. Wana nguvu na uwezo wa kustahimili mazingira magumu.

Wanaweza kutembea muda mrefu kutafuta malisho hata wakati wa joto,malisho yakiwa hadimu na hayana ubora.

Wanajua ni vichaka gani vya kuliwa na ni vipi vyenye sumu. Pia hukabiliana vyema na magonjwa na wadudu, kama minyoo, kupe na nzi wanaouma.

Mpango wa uzalishaji

Weka mpango mzuri wa ufugaji ambao ni pamoja na kumbukumbu za wanyama zilizohifadhiwa vizuri ili kuzuia kuzaliana kondoo wenye uhusiano wa karibu.

Kondoo wa kienyeji wanaweza kuboreshwa zaidi kwa muda mfupi ikiwa kuna mipango thabiti, usimamizi bora na uzalishaji wa hali ya juu.

Chagua kondoo jike walio na maumbile mazuri, mwili mrefu na mifupa yenye nguvu. Kwa njia hii unapata kondoo wenye mwili mkubwa na nyama nyingi.

Tumia kondoo jike na dume wenye ubora wa hali ya juu kuzalisha. Usitumie kondoo wafupi na wenye mwili ndogo.

Vigezo vingine vya uteuzi ni pamoja na ukuaji wa haraka, afya njema na uwezo wa kuzaa mapacha.

Uza Kondoo wasio na ubora na tumia pesa kununua kondoo jike wengine ili uweze kuongeza idadi ya kondoo haraka. Pia, tumia pesa kununua dawa za kudhibiti magonjwa na wadudu.

Ufugaji ulioboreshwa

Kuboresha kondoo kwa kuzalisha chotara huenda sambamba na ufugaji ulioboreshwa; lishe, makazi, na udhibiti wa magonjwa.

Bila usimamizi bora, kondoo walioboreshwa wanaweza wasifanye vizuri; wanaweza kufanya vibaya zaidi kuliko wale wa kienyeji, kinyume na matarajio ya mfugaji.

Wanyama waliolishwa vibaya hawahimili magonjwa na vimelea. Hawaingii kwenye joto haraka, uzalishaji wao wa maziwa ni duni na wana-kondoo wao ni dhaifu na hukua taratibu.

Mabanda safi, maji safi, malisho bora na virutubisho vya madini ni muhimu.

Kondoo wanakula nyasi iliyo karibu na ardhi tofauti na ng’ombe na mbuzi.

Mbuzi wanapendelea vichaka. Hivyo basi, kuwa makini na idadi ya kondoo kwenye malisho. Ikiwezekana, zungushia maeneo ya malisho ili kutoa nafasi kwa malisho muda wa kupoa na kukua tena.

Unaweza kuwalisha kondoo nyasi iliohifadhiwa wakati wa jiioni wanapopumzika.

Tumia dume wa Dorper

Kondoo wa Dorper ni mseto kati ya kondoo wa Blackhead Persian (uzao wa Kiafrika) na Dorset Horn (uzao wa Uingereza), uliozalishwa Afrika Kusini. Ni kondoo mwenye mafanikio makubwa na ameuzwa kwa nchi nyingi. Kuna aina mbili: ‘Dorper’ mwenye kichwa cheusi, na ‘White Dorper’ mwenye kichwa cheupe. Wafugaji wengi wamemzoea ‘Dorper’ mwenye kichwa cheusi.

Kondoo wa Dorper hufanya vizuri katika maeneo mengi kutoka nyanda za juu hadi maeneo yenye ukame. Wana uwezo mkubwa wa kuzaliana na wanaweza kuzaa kila baada ya miezi 8. Wana-kondoo huongeza uzito haraka, hukomaa mapema na huweza kupandishwa ndani ya  miezi 9.

Kondoo wa kienyeji (kama kondoo wa Kimasai) hupandishwa kondoo dume wa Dorper. Kondoo wa kike wanaozaliwa pia wanapandishwa tena dume wa Dorper wasiohusiana. Kwa kufanya hivyi, unachanganya sifa nzuri za kondoo wa kienyeji na kondoo wa kigeni. Unazalisha angalau mara mbili ili kupata kizazi kizuri chotara.

Utafiti umeonyesha kuwa chotara kati ya Dorper na Red Maasai wana kiwango cha juu cha kuzaliana. Kiwango hiki cha juu kinapatikana kwa kupadisha Red Maasai na Dorper, kisha kumpadisha kondoo aliyezaliwa na dume wa Red Maasai; yaani unatumia dume wa Dorper mara ya kwanza na kurudi kwa dume wa Red Maasai mara ya pili. Unapata kizazi chenye 75% sifa za Red Maasai na 25% sifa za Dorper.

Zuia kuzaliana ndani

  • Kondoo-dume hapaswi kupandishwa kwa dada zake, binti, wajukuu, mama au bibi/nyanya.
  • Weka rekodi na utumie mfumo ambao unaruhusu kutambua kila mnyama na wazazi wake, angalau mama na baba, bibi na babu.
  • Kondoo-dume hapaswi kutumika katika kundi moja ya kondoo-jike zaidi ya mwaka mmoja.
  • Kondoo dume wanapaswa kuzungushwa mara kwa mara kati ya watumiaji na vikundi vya wakulima.
Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *