- Mifugo

Jifunze kuhusu kiwavijeshi vamizi na namna ya kumdhibiti kwa kutumia dawa za kilimo hai

Sambaza chapisho hili

Jinsi ya kuzuia waharibufu wa mahindi kwa kutumia dawa ya kilimo hai

Mahindi ni zao muhimu na tegemezi kwa jamii nyingi barani Afrika. Nchini Tanzania zao hili hulimwa mikoa yote kwani ni zao tegemezi kwa chakula. Hata hivyo, zao hili lina changamoto, kwani hushambuliwa na  visumbufu mbalimbali vya mimea ikiwamo  viwavijeshi vamizi (Fall armyworm).

Viwavi hawa hula sehemu zote za mmea – majani, bua, mbegu, gunzi; pia hula aina nyingine za mimea. Umakini mkubwa unahitajika katika kuwadhibiti sababu huingia ndani ya bua na gunzi la mhindi.

Mdudu huyu amekuwa tatizo kubwa katika Nchi za Kusini Mashariki ya Asia, uangamizwaji umekuwa changamoto. Wakulima wengi wamepata hasara kutokana na uvamizi wa mdudu huyu, kwani si wote wanaweza kumudu gharama za kununua dawa kumuangamiza mdudu huyu.

Hatua za ukuaji na uharibifu

Mdudu huyu huanzia hatua ya mayai na ni vyema kuanza kupambana nae katika umri wa lava kama ufunguo wa kudhibiti mashambulizi yao shambani.

Mdudu huyu hukua na kugeuka Nondo (kipepeo), ambae hutaga mayai na muda wake wa kuishi ni siku 30 huku akiwa kama buu kwa siku 6.

Jike la Nondo hutaga mayai 200 hadi 250  kwa mara moja katika jani la mmea wa hindi. Katika maisha yake yote hutaga mayai yasiyo pungua 1,000 – 1,500.

Ndani ya siku 5 baada ya mayai kutagwa huanguliwa viwavi na kuanza kushambulia mahindi machanga. Viwavi hawa huwa wadogo na wenye rangi ya Kijani na huning’inia kwa utando wa nyuzi kama buibui ambao huwa na vichwa vyeusi na badae vichwa hivyo hubadilika na kuwa vya rangi ya chungwa (Orange) na mara ya tatu hugeuka na kuwa rangi ya kahawia. Katika hatua hii huanza kula katika sehemu ya chini ya mmea wakati.

Hatua inayofuata huanza kula sehemu ya juu ya mmea hasa katikati ya mmea na katika hatua hii huweza kutambulika kwa madoa manne meusi kwa nyuma, na umbile la ‘Y’ usoni iliyogeuka chini juu.

Baada ya muda mdudu huyu huanguka chini udongoni na kujizika mwenyewe katika udongo na huingia kiasi cha  urefu wa sentimita 2.8 udongoni na huwa anageuka na kuwa pupa.

Baada ya siku saba (7) – kumi  (10) hubadilika na kuwa Nondo na hii ndio hatua ya mwisho katika kukomaa.

Mdudu huyu hushambulia zaidi ya aina za mimea 80. Lakini hupendelea sana kula Mahindi, Mtama, Majani aina ya Bermuda, Solighum n.k.

Dalili za uharibifu wa mdudu huyu kwenye mahindi

Ishara za uharibifu wa mdudu huyu ni majani kuwa na madirisha madirisha – kwa kuwa lava mdogo huwa na urefu wa mm 1. Huanzia uharibifu wake katika kuyakwangua majani akiyala na kuacha utando mithili ya nailoni nyeupe ndipo anapoelekea sehemu ya kati ya mmea linapoanzia jani kuota yaani katikati ya jani changa na jipya.

Hivyo mara baada ya kubaini uvamizi wa mdudu yafaa kuwa makini haraka, tembelea shamba kwa mtindo wa ‘W’ ili kubaini mashambulizi kila mara.

Njia za kudhibiti mashambulizi ya mdudu huyu

Kupanda mazao mapema, fanya mzunguko wa mimea, utumiaji wa mitego (pheromone traps), na wadudu wenye faida shambani wanao dhibiti wengine.

Unaweza kutumia dawa ya Kilumagio kuangamiza na kuwa huru na tatizo la usumbufu wa wadudu ndani ya masaa 8 na kwa kawaida hutumika jioni.

Kilumagio huuwa mdudu anapokuwa akiila katika majani yaliyo komaa, majani machanga, na katikati ya mmea ili kuzuia ua dume lisitoke na hatimae anaposhambulia uwa jike.

Kilo  mbili na nusu (2 ½ Kg) huweza kutumika kwa hekari moja na hukaa kwa takribani wiki 4 kama hakuna mvua. Dawa hii ni ya unga nayo hutumika kwa kumwagia sehemu ya kati ya mmea.  Huvutia wadudu kuila kwakuwa kwao huwa mlo wa mwisho wa usiku katika maisha yao.

Wadudu hawa hupenda kutafuta chakula usiku wakati hali ya hewa imetulia hakuna joto na wanauwezo wa kuinusa dawa hii na kuifuatilia hata wanapo kuwa ndani ya mmea au katikati ya mwanzo wa mbegu za hindi.

Dawa ya kuwaua wadudu waharibifu wa mahindi – Kilumagio

Dawa hii ni rafiki wa mazingira kwa kuwa haiuwi wadudu rafiki au kuvuruga mfumo wa ikolojia katika udongo, bali humvuta na kumuangamiza  mdudu huyu muharibifu anaetoboa mahindi tangu yangali madogo.  Dawa hii ya Kilimo hai hutumika mara moja na kufanya kazi kwa wiki nne (4) iwapo kama mvua haijanyesha kupita kiasi hivyo huweza kutumika mara mbili kabla ya kuvuna mahindi.

Jinsi ya kutengeneza dawa ya kilumagio

Mahitaji

  • Unga wa mahindi ya njano au mahindi ya kawaida kilo tano (kilo 5)
  • Sukari kilo 1 (kilo 1)
  • Amira au bicarbonate of soda gramu 70
  • Maji lita mbili (lita 2)

Jinsi ya kufanya

Weka unga wako katika ndoo au beseni, ongezea kilo moja ya sukari changanya vizuri, ongeza boksi moja la bicarbonate of soda au Amira changanya vizuri weka maji lita mbili changanya hadi mchanganyiko ukolee na kutoa harufu kama ya pombe.

Utumiaji

Nyunyuzia kidogo katikati ya hindi kabla halijatowa mbelewele, tumia mkono mmoja ulio jaa unga huu kwa mashina 35 – 40 hivyo inaweza kutumika kwa sehemu kubwa shambani.

Dawa hii inapotumika humvuta mdudu aifuate hata zaidi ya futi moja toka aliko jificha wakati wa usiku. Mdudu huyu huwa na tabia ya kutoka nje ya maficho wakati wa giza (usiku).

Dawa hii hufanya kazi ya maangamizi ndani ya masaa manane (8) ya usiku na kuliweka shamba lako huru na mashambulizi.

Kilo 2.500kgs unaweza kutawanya katika hekari moja ya mahindi iliyo pandwa 60 x 75cm.

Shamba la kilimohai st joseph pia wanatengeneza virutubisho mbalimbali vya kioganiki visivyo na kemikali ya aina yoyote. Unaweza kupata virutubisho kama busta za kiorganiki, NPK zitokanazo na mchanganyiko wa vyakula.

Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana na SJS ORGANIC FARM, Kwanyange, Mwanga, Kilimanjaro. WhatsApp: +255 715990308 / +255 626908639, Email: sjsorganic@gmail.com / Website: www.sjsorganic.org, Facebook/Instagram/YouTube: sjsorganic

 

Maoni kupitia Facebook
Sambaza chapisho hili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *